Aussems apangua kikosi cha Simba ikivaa Mashujaa

Mashabiki wa timu ya Mashujaa na Simba wakiwa uwanjani wakisubiria mechi ya kirafiki baina ya timu hizo itakayochezwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika leo

Muktasari:

Simba ipo mkoani Kigoma ikicheza mechi zake mbili za kirafiki kabla ya kurejea Dar es Salaam kuivaa Azam katika Ligi Kuu Tanzania Bara

Dar es Salaam. Kocha wa Simba, Patrick Aussems amefanya mabadiliko makubwa ya kikosi chake kutoka kile kilichocheza na Bandari FC na kilie kitakachoanza leo dhidi ya Mashujaa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika.

Katika kikosi kocha Aussems ameanzisha chipukizi wanne, Athumani Mtamilwa, Joseph Peter, Maulid Lembe na Dickson Mhilu.

Wakati katika mchezo uliopita dhidi ya Bandari Fc kocha huyu alimuanzisha chipukizi mmoja, Joseph Peter na kucheza vizuri katika nafasi ya beki wa kushoto na baadae kutolewa.

Kocha Aussems pia amemrejesha kikosini kipa wake namba moja, Aish Manula huku katika mchezo uliopita alicheza Beno Kakolanya.

Katika nafasi ya ulinzi amewaanzisha Athumani Mtamilwa, Joseph Peter, Yusuph Mlipili na Kennedy Juma huku katika mchezo uliopita wakicheza Haruna Shamte, Joseph Peter, Tairone Santos na Pascal Wawa.

Nafasi ya kiungo leo amewaanzisha Said Ndemla, Rashid Juma, Maulid Lembe na Francis Kahata huku katika mchezo uliopita walianza Gerson Fraga, Deo Kanda, Sharaf Shiboub na Francis Kahata.

Katika ushambuliaji mchezo na Bandari aliwaanzisha Wilker Da Silva na Ibrahim Ajibu lakini leo amewaanzisha Dickson Mhilu na Ibrahim Ajibu.

WADAU WAFUNGUKIA MECHI ZA KIRAFIKI

Mechi hizi za kirafiki kwa klabu za Azam na Simba zimeibua mijadala kwa wadau wa mpira kutokana na kucheza mechi hizo siku ambayo timu ya Taifa Tanzania inacheza.

Tanzania 'Taifa Stars' inacheza mchezo wa kirafiki na Rwanda leo saa moja jioni ikiwa ni kalenda ya Fifa, wakati huo huo kuna michezo ya kirafiki Azam vs African Lyon na Simba dhidi ya Mashuja ambayo inacheza saa kumi jioni.

Aliyekuwa katibu mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema TFF walipaswa kutoruhusu mechi za klabu kucheza leo ili mashabiki akili zao ziweze kuipa sapoti Stars.

"Kwa kuruhusu klabu ziecheze ni kuweka makundi ambapo mashabiki wataanza kuwaangalia wachezaji wa timu zao tu," alisema.

Aliongeza Stars ina wadhamnini ambao pia wanahitaji sapoti ya mashabiki, hivyo hizi mechi za Simba na Azam zingechezwa hata kesho ingawa ni muda tofauti na Stars watakaocheza.

Ofisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo alisema kuchezwa kwa mechi hizo hakuna shida yoyote kutokana na muda kuwa tofauti.