Simba yapata mapokezi makubwa Kigoma

Muktasari:

Viingilio katika mechi ya Mashujaa na Simba ni Sh 5,000 kwa viti vya kawaida na VIP Sh10,000.

Kigoma. Kwa mara ya kwanza baada ya miaka 18, mashabiki wa soka mkoani Kigoma wataishuhudia Simba kesho ikicheza mechi ya kirafiki dhidi ya Mashujaa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika.

Simba imewasili Kigoma leo mchana na kupokelewa na mamia ya mashabiki wake mkoani hapa ambako itaanza kwa kucheza mechi yake ya kwanza kirafiki dhidi ya Mashujaa fc kesho Oktoba 14, kabla ya kuivaa Aigle Noir ya Burundi Oktoba 16, 2019. 

Akizungumza baada ya kuwasili Kigoma, kocha wa Simba Patrick Aussems alisema amefurahi kufika mkoani humo wamejipanga kupata ushindi katika michezo hiyo.

Aussems alisema mechi hizo za kirafiki ni maandalizi ya kujiweka tayari na mchezo unaofuata dhidi ya Azam fc katika Ligi Kuu.

Katibu wa Chama Soka mkoa wa Kigoma (KFA), Omary Gindi alisema viingilio katika mechi ya Mashujaa na Simba ni Sh 5,000 kwa viti vya kawaida na VIP Sh10,000.