Prime
Panga TFF, DK msolla atoa ya moyoni

WAKATI Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ikimpitisha Wallace Karia kuwa mgombea pekee wa urais wa shirikisho hilo, mmoja wa wagombea waliofyekwa, Dk Mshindo Msolla ametoa ya moyoni kutokana na kukata jina katika uchaguzi huo.
Uchaguzi mkuu wa TFF unatarajiwa kuanza Agosti 16, mwaka huu.
Dk Msolla ni kati ya majina ya wagombea urais watano waliofyekwa waliotangazwa jana na Kamati ya Uchaguzi iliyombakisha mtetezi wa kiti, Karia, huku wajumbe wa Kamati ya Utendaji imeondoka na vichwa saba kati ya 19 vilivyojitokeza kuomba nafasi.
Wengine waliokuwa wakiwania urais ni Ally Mayay, Ally Thabit Mbingo, Mustapha Salum Himba na Shija Richard.
Akitangaza taarifa ya majina yaliyopenya kupitia usaili uliofanyika juzi, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa TFF, Wakili Kiomoni Kibamba alisema Karia ndiye aliyekidhi vigezo, huku wanne wakishindwa kukidhi kanuni za uchaguzi na mmoja hakutokea kwenye usaili.
Kibamba alisema kwa wagombea ujumbe kulikuwa na watu 19 ambapo 17 walihudhuria usaili, ilhali saba walikosa vigezo hivyo 10 kupitishwa na kamati kwa ajili ya hatua nyingine zinazofuata za uchaguzi huo. Hata hivyo, Kibamba alisema wagombea waliokosa sifa na kukatwa wana nafasi ya kukata rufaa Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi endapo wataona hawajatendewa haki.
“Sisi ni kamati ya uchaguzi na ni binadamu inawezekana wapo watakaoona wameonewa. Bado wana nafasi ya kwenda kukata rufaa kwenye Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi. Kutakuwa na siku sita za kukata rufaa na sisi (Kamati ya Uchaguzi) tutapokea orodha kamili ya wagombea kutoka kwa Kamati ya Rufaa ili tuendelee na hatua inayofuata.”
WALIOFYEKWA
Kocha wa zamani wa timu ya taifa aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Yanga, Dk Mshindo Msolla alipotafutwa na kuzungumzia ya jina lake kufyekwa alisema: “Ilichofanya kamati hiyo kuna siku Watanzania watakuja kuwahukumu. Watanzania sio wajinga wanafahamu wanafanya kwa ajili ya masilahi ya nani.”
NayeHimba alisema: “Ndio kwanza natoka msikitini sijapata taarifa rasmi, ngoja nipate muda wa kuzipitia nitakuwa na wakati mzuri wa kutoa msimamo wangu.”
Nyota wa zamani wa Yanga aliyewahi kuwa kaimu mkurugenzi wa Michezo, Ally Mayay alipotafutwa aliomba atafutwe muda mwingine kwa vile alikuwa kwenye mkutano mkoani Morogoro.