Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Fadlu amaliza utata, mastaa zaidi ya saba kufyekwa

Muktasari:

  • Hata hivyo, kuna jambo kubwa lililokuwa likizipasua nyoyo zao, juu ya mustakabali wa kocha mkuu wa timu hiyo, Fadlu Davids na wasaidizi wake, waliowapa burudani katika michuano yote iliyoshiriki ligi licha ya kushindwa kubeba taji lolote, lakini utata huo umemalizwa wakati kocha huyo akiwa mapumzikoni Afrika Kusini.


MASHABIKI wa Simba bado wanaendelea kutafakari namna chama lao lilivyoshindwa kufanya kweli katika michuano iliyoshiriki msimu uliomalizika hivi karibuni kuanzia katika Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho (FA) na Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kutoka kapa.


Hata hivyo, kuna jambo kubwa lililokuwa likizipasua nyoyo zao, juu ya mustakabali wa kocha mkuu wa timu hiyo, Fadlu Davids na wasaidizi wake, waliowapa burudani katika michuano yote iliyoshiriki ligi licha ya kushindwa kubeba taji lolote, lakini utata huo umemalizwa wakati kocha huyo akiwa mapumzikoni Afrika Kusini.


Utata uliokuwapo kuhusu ya hatma ya kocha mkuu wa Simba, Fadlu Davids umemalizwa baada ya kudaiwa amekubali kuongeza mkataba mpya wa kuendelea kuinoa timu hiyo aliyoiwezesha kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kumaliza nafasi ya pili katika Ligi Kuu Bara.

Inaelezwa kuwa, licha ya kocha huyo kuondoka nchini kabla ya kusaini mkataba mpya, mazungumzo yake na bilionea wa klabu hiyo, Mohammed ‘Mo’ Dewji yaliyofanyika juzi kati yameleta neema kwa Fadlu kukubali kurudi sambamba na benchi lote alilofanya nalo kazi msimu uliomalizika.

Chanzo cha ndani kutoka Simba, kimeijulisha Mwanaspoti kuwa, Fadlu pamoja na benchi lote la ufundi wamekubali kusaini mikataba mipya ya mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongezwa mwaka mwingine, baada ya kikao kizito kilichowahusisha viongozi wa juu wa klabu hiyo chini ya Mo Dewji.

Hatua hiyo imehitimisha sintofahamu iliyokuwapo juu ya hatma ya benchi la ufundi baada ya kushindwa kufikia mafanikio yaliyotarajiwa msimu uliopita ambapo ilikuwa ni pamoja na kufanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya Simba, benchi lote la ufundi lilikuwa limefikia ukomo wa mikataba yao mara baada ya msimu kumalizika, lakini kutokana na tathmini iliyofanywa kwa kina na viongozi, wakaamua kuwapa muda zaidi kwa imani bado wana mchango mkubwa wa kuipa mafanikio.

Chanzo chetu kilieleza kuwa kulikuwa na minong’ono ya timu kadhaa kutoka ndani na nje ya Afrika ambazo zilikuwa zimeonyesha nia ya kutaka huduma ya Fadlu, jambo ambalo lilimfanya Mo Dewji kuchukua hatua ya haraka kuhakikisha anamsainisha mkataba mpya kabla ya mambo hayajaharibika.

“Mo Dewji hakutaka kusubiri hata kidogo. Aliamua kukamilisha haraka suala la mkataba mpya kwa Fadlu baada ya kuona kuna mawakala wa timu nyingine wakianza kuwasiliana naye. Mo aliamini kuwa licha ya Simba kutotwaa taji msimu uliopita, kazi ya Fadlu inaonyesha dira sahihi ya mafanikio ya baadaye,” kilisema chanzo chetu cha uhakika kutoka ndani ya Simba.

Hii ni mara ya pili kwa Mo Dewji kuingilia moja kwa moja masuala ya kiufundi ndani ya Simba katika kipindi cha hivi karibuni, na mara hii akihimiza utekelezaji wa haraka wa ripoti ya kiufundi iliyowasilishwa na Fadlu kuhusu mabadiliko ya kikosi, falsafa ya timu na aina ya wachezaji awatakao.

Kwa sasa benchi hilo linasubiriwa kurejea kutoka katika mapumziko mafupi ili kuanza maandalizi ya msimu mpya, huku Fadlu akisema ameshawasilisha ripoti inayotaka usajili wa wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kushindana kimataifa, wenye uzoefu, wepesi wa kufuata maelekezo ya kiufundi.

Inaelezwa pia kocha huyo amependekeza kuwepo na ukaguzi wa kina kwa wachezaji waliopo kwa lengo la kuhakikisha kila mmoja anayebaki anakidhi vigezo vya benchi hilo lililoiwezesha Simba kumaliza katika nafasi ya pili kwa kuvuna pointi 78 kupitia mechi 30 na kufika fainali ya CAF dhidi ya RS Berkane ya Morocco iliyotwaa taji kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-1.

Inaelezwa Simba inaachana na wachezaji wasiopungua saba, akiwamo Fabrice Ngoma aliyeaga mapema, kipa Moussa Camara, Fondoh Che Malone, Augustine Okejepha na Hussein Kazi, huku kati ya Ladack Chasambi au Edwin Balua na kipa Ally Salim watatolewa kwa mkopo, wakati Aishi Manula amemaliza mkataba na kusaini Azam, ilihali Steven Mukwala ikielezwa yupo mbioni kuuzwa Afrika Kaskazini.

Kuondoka kwa mastaa hao kunafungua nafasi ya majembe mapya yaliyopendekezwa na Fadlu kutua Msimbazi kwa ajili ya kuanza mikakati ya msimu mpya ikiwamo kufika nusu fainali kama sio fainali katika Ligi ya Mabingwa Afrika inayorejea baada ya msimu uliopita kucheza Kombe la Shirikisho na kukosa ubingwa.