Kumbe Molinga kama Kagere tu

Muktasari:

Mwanaspoti limefanya uchambuzi na kubaini timu yenye safu nzuri zaidi ya ulinzi na washambuliaji kwa kutumia takwimu za Ligi Kuu Bara mpaka Februari, 02, 2020.

ACHANA na ushindani wa kuwania taji la Ligi Kuu Bara kwa timu za Simba, Yanga na Azam FC ambazo hata zikikutana kwenye mechi zao zinakuwa ngumu huku kila timu ikiwa inahitaji pointi, vita imehamia kwenye wastani wao wa kufunga mabao.

Mwanaspoti limefanya uchambuzi na kubaini timu yenye safu nzuri zaidi ya ulinzi na washambuliaji kwa kutumia takwimu za Ligi Kuu Bara mpaka Februari, 02, 2020.

SIMBA

Kila mechi ina wastani wa kufunga mabao mawili au matatu msimu huu kwa mujibu wa takwimu za msimamo wa ligi hiyo ambapo takwimu hizo ni sawa na mabao 40 katika mechi 18 iliyocheza. Safu ya ulinzi ya Wekundu wa Msimbazi imeonekana kuwa makini kwa kuruhusu bao moja pekee katika kila mechi mbili walizocheza msimu huu.Timu hiyo imefungwa mabao tisa pekee. Ukiachana na wastani wa mabao ya kufungwa na kufunga, Simba imevuna pointi 47 katika mechi 18, ikishinda 15, sare mbili na imefungwa mmoja.

AZAM FC

Takwimu za VPL inaonyesha Azam FC ilifunga angalau bao moja katika kila mechi, wakati safu yake ya ulinzi ikiruhusu bao moja pekee katika kila mechi mbili. Takwimu za msimamo zinaonyesha Azam imefunga mabao 24 na kuruhusu tisa. Hata hivyo, safu ya ushambuliaji ya timu hiyo inaonekana kuwa ya kawaida kwani hakuna hata straika wake aliyefunga angalau mabao sita. Azam inamiliki pointi 37 katika mechi 18, imeshinda 11, sare tatu, imefungwa mara tatu.

YANGA

Takwimu zinaonyesha ina wastani wa kufunga bao moja hadi mawili kila mechi kutokana na kucheza mechi 16 na kuvuna mabao 20.

Safu ya ulinzi ya timu hiyo sio imara kwani inaruhusu takribani bao moja kila mechi. Mpaka sasa imeruhusu mabao 15 kwenye nyavu zao. Ukiachana na wastani wa wa mabao Yanga inamiliki pointi 31 katika mechi 16 ilizocheza, imeshinda tisa, sare nne na imefungwa mechi tatu.

MOLINGA KAMA KAGERE TU

Takwimu za msimamo wa ligi mpaka sasa zinaonesha straika wa kigeni Yanga, David Molinga ana wastani wa kufunga bao moja katika kila mabao matatu yaliyofungwa na timu hiyo msimu huu. Molinga amefunga mabao sita kati ya 20 yaliyofungwa na timu hiyo.

Wastani huo wa Molinga unalingana kabisa na ule wa Mshambuliaji wa Simba Meddie Kagere ambaye naye ana wastani wa kufunga bao moja katika kila mabao matatu iliyofunga timu hiyo. Kagere amefunga mabao 12 kati ya 40 ya Simba mpaka sasa.

Kutokana na mwenendo wa timu hizo, straika wa zamani wa Simba, Emmanuel Gabriel alisema licha ya washambuliaji kuwa kwenye kiwango kizuri lakini wanatakiwa kuongeza bidii ili wawe na wastani wa kufunga mabao mawili kila mechi.

“Wastani wao sio mbaya, ila waongeze juhudi ndio itakuwa nzuri zaidi, naamini wanaweza kinachotakiwa ni kujitoa kwa bidii ili kufanya maajabu,”alisema.

Mchambuzi wa soka nchini, Ally Mayay alisema wastani huo una tafsiri kwamba wazawa bado wana mzigo mzito wa kushindana na washambuliaji wa kigeni ambao wanang’ara kwa sasa.

Alifafanua angalau Paul Nonga na Daruesh Saliboko wa Lipuli ambao wana mabao manane kila mmoja wangekuwa Simba, Yanga na Azam anaamini wangeweza kushindana na Kagere na Molinga wanaoongoza.