Molinga akata kilo tisa mabeki mjipange kweli

Muktasari:

Baada ya kupambana kufanya mazoezi binafsi gym, kukimbia na mpira pamoja na mpangilio mzuri wa chakula amedaia amepunguza kilo tisa, akisema awali alikuwa na Kilo 89, ila kwa sasa anacheza kwenye kilo 78-79.

Dar es Salaam. HIVI unajua mambo aliyofanya straika wa Yanga, Mkongomani, David Molinga?  Unaambiwa amepambana kukata uzito hadi sasa amekuwa ‘mtamu’ na kutupia mabao na kutengeneza pasi za mwisho.
Straika huyo mwenye mwili jumba na aliyegeuka kipenzi cha mashainiki wa Yanga alikuja nchini akitokea Congo akiwa na mwili mkubwa zaidi jambo lililompa wakati mgumu kuonyesha uwezo wake.
Baada ya kupambana kufanya mazoezi binafsi gym, kukimbia na mpira pamoja na mpangilio mzuri wa chakula amedaia amepunguza kilo tisa, akisema awali alikuwa na Kilo 89, ila kwa sasa anacheza kwenye 78-79.
“Nimepunguza kilo tisa kwa kipindi ambacho niliamua kutengeneza mwili wangu. Nilikuja Tanzania nikiwa na mwili mkubwa, hii ni kutokana na kutokucheza kwa muda, ila kwa sasa nimepungua kwa uzito huo,”alisema Molinga.
Molinga ambaye kwa sasa pangapangua amekuwa chaguo la kwanza ndani ya kikosi cha Yanga chini ya Kocha Charles  Boniface Mkwasa, ndiye kinara wa mabao kikosini mwao akiwa amefunga manne, akilingana na Patrick Sibomana waliyetua wote ndani ya msimu huu.