Mkwasa amtega Molinga kimtindo Yanga

Muktasari:

Kaimu Kocha Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa amemtega kimtindo Molinga akisema atampa nafasi kwa vile anaona ana kitu

Dar es Salaam. UKISIKIA mtego ndio huu kwa straika David Molinga ‘Ndama’. Si mnakumbuka kipindi Yanga ikiwa chini ya Kocha Mwinyi Zahera ilielezwa alikuwa akishindwa kufanya vyema kwa vile alikuwa mzito kutokana na kuwa na kilo nyingi na kupangiwa mazoezi maalumu?
Hata hivyo, baadaye alianza kuonekana wamo kwa kufunga mabao matano, yakiwamo matatu ya mechi za kirafiki na mengine ya Ligi Kuu Bara, lakini sasa buana, Kaimu Kocha Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa amemtega kimtindo akisema atampa nafasi kwa vile anaona ana kitu.
Hata hivyo, Mkwasa alisema ni wajibu kwa straika huyo kutumia nafasi anazompa kuitumikia timu hiyo, vinginevyo asishangae akimpiga benchi kwa sababu Yanga ni timu inayohitaji matokeo ili kutoka eneo la chini kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.
Mkwasa aliliambia Mwanaspoti, hana wasiwasi na mshambuliaji huyo ila ni kama atafanya mambo ambayo anayohitaji.
Kocha huyo alisema hana tatizo na Molinga kuwa na mwili mkubwa au uzito, ila anachotaka kutoka kwake ni kutimiza majukumu yake ya kufunga kutokana na nafasi yake ambayo anacheza.
“Kama atakuwa anafanyia kazi vile itakavyo na tunavyomwelekeza na akafunga mabao mengi hilo la uzito au mwili wake kwangu sio ishu kabisa, naamini anajua kazi iliyomleta nchini, lakini kama ikiwa tofauti na hivyo hapo ndio naweza kufanya maamuzi mengine,” alisema.
Mkwasa aliongeza: “Nitakaa naye na kumweleza kila mechi kuichukulia kawaida na kuachana na presha itokayo nje kwa mashabiki ili afanye kazi yake vizuri, kwani nimemuona kwa muda mfupi mazoezini anao uwezo wa kufanya hilo.
“Ila kama atashindwa kutimiza majukumu yake katika nafasi ambayo anacheza hilo linaweza kuwa tatizo lingine na hapo naweza kufanya maamuzi ya kumpa nafasi mchezaji mwengine, ila ieleweke hili sio kwa Molinga tu, bali kwa wachezaji wote kama watashindwa kufanya vizuri kulingana na nafasi zao, nitatoa nafasi kwa mwingine,” alisema Mkwasa na kuongeza;
“Kwa muda niliokaa ndani ya timu nimeona uwezo wa kila mchezaji na nimekuwa nikizifuatilia timu zote kwenye ligi kwa maana hiyo kulingana na timu yangu ilivyo naimani tunaweza kufanya vizuri kutokana na maandalizi haya ambayo tunafanya,” aliongezea Mkwasa.
Molinga ndiye mchezaji wa mwisho msimu huu wa kigeni kusajiliwa na Yanga na mpaka sasa ameifungia mabao mawili akiwa ndiye kinara wa timu hiyo akifanya hivyo kwenye mechi dhidi ya Polisi Tanzania iliyoisha kwa sare ya 3-3.
Nyota wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Boniface Pawasa, alisema anamfahamu Molinga siku nyingi tangu kipindi anacheza aliwahi kukutana naye Rwanda na alikuwa na kiwango kizuri.