Molinga anadondosha moja moja mpo hapo

Muktasari:

Molinga anamiliki mabao manne, alifunga mawili dhidi ya Polisi Tanzania, moja JKT Tanzania na moja Alliance, hilo limewaibua makocha na wachezaji wa zamani kuzungumzia kiwango chake.

Dar es Salaam. STRAIKA wa Yanga, David Molinga ameendelea kuzifumania nyavu na kuzima kejeli za baadhi ya mashabiki waliokuwa wanamuona hawezi kufurukuta.
Akiwa chini ya Kocha Mwinyi Zahera mashabiki waliona kama anapendelewa kupangwa kikosi cha kwanza, lakini baada ya jukumu hilo kuwa mikononi mwa Kocha Charles Mkwasa bado anamtumia mchezaji huyo.
Molinga anamiliki mabao manne, alifunga mawili dhidi ya Polisi Tanzania, moja JKT Tanzania na moja Alliance, hilo limewaibua makocha na wachezaji wa zamani kuzungumzia kiwango chake.
Kocha wa zamani wa Yanga, Kennedy Mwaisabula alisema anayafananisha maisha ya Molinga na Simon Msuva ndani ya kikosi hicho kwa namna wana nyota ya kuzomewa na kushangiliwa kwa nyakati tofauti.
Alirejea maisha ya nyuma ya Msuva akiwa Yanga kwamba licha ya kufanya mengi mazuri, mashabiki waliyapa nguvu makosa madogo na kumzomea, akifananisha na anavyoishi Molinga kwa sasa.
Alisema kabla ya Zahera kutimka walikuwa wanamuona anampendelea kumpanga, ajabu kaja Mkwasa bado anamtumia, hivyo aliwataka wawe watulivu juu yake.
“Kuna wakati Molinga anakuwa shetani kuna wakati anakuwa malaika, tafsiri ni kwamba anapopatia mashabiki wanamshangilia, akikosea wanamzomea, ninachopenda kwake haogopi kelele anafanya kazi,” alisema Mwaisabula na kuongeza;
“Kiufundi namuona Molinga ni mchezaji muhimu ndani ya Yanga, ni mwiba kwa mabeki wengi, akipunguza uzito akawa mwepesi kwenye maamuzi upepo utabadilika na hapo ndio tofauti yake na Msuva, ambaye alikuwa mwepesi.”
Nyota wa zamani wa Simba, Ulimboka Mwakingwe alisema akimwangalia Molinga anamuona ni straika mwenye kitu mguu kwake na kumshauri apunguze mwili wake ili awe mwepesi.