HISIA ZANGU : Kagere anavyokula pensheni yake kwa vigelegele msimbazi

Wednesday October 9 2019

 

By Edo Kumwembe

NANI kafunga? Unauliza. “Kagere huyo,” unajibiwa. Huwa nafurahi ninapopita katika makundi ya watu wanaotazama soka kupitia katika baa mbalimbali. Utakuta Wamachinga na bidhaa zao wamesimama kando ya baa wakifuatilia mechi ya Simba.

Unasimamisha gari unauliza “Nani kafunga?” Wote wanajibu “Kagere”. Unatabasamu. Unawasha gari unaondoka. Unamuonea wivu kidogo Kagere na bahati aliyopata. Bahati ya kuja kumalizia mpira wake Tanzania.

Pasipoti yake inaonyesha ana umri wa miaka 32. Utake usitake, ndivyo inavyoonyesha. Wengine wanasema ana miaka 40. Sidhani kama anajali. Kitu cha msingi ni kumuonea wivu kwa jinsi alivyopata chimbo zuri la kumalizia soka Tanzania.

Kwanza kabisa hakuna timu ya nchi jirani inayolipa vizuri katika soka kuliko sisi. Halafu sio ‘kuliko sisi’ tu, tunaweza kusema kuliko Simba. Si Rwanda, si Kenya, Si Uganda wala Burundi. Hapa kuna mambo yanayojitokeza kimsingi.

Kwanza anafaidi dola zake. Pili ana uhakika wa kuendelea kuwepo kwa miaka kadhaa. Namtabiria Kagere kuwa Simba na kung’ara kwa miaka mitano hivi tangu awasili. Kama nafasi yake itaweza kuwa hatarini basi ni kwa kumletea washambuliaji wa kigeni wa uhakika.

Angeenda mbali na nchi yetu wachezaji wa nafasi yake wangemsumbua. Wenzetu wanashinda. Sisi bado hatushindani. Ndio maana aliletewa akina Adam Salamba wenye umri mdogo, ambao damu inachemka, lakini bado akawa staa. Ni ngumu kwake kushindana na ‘Adam Salamba’ wa Senegal.

Advertisement

Lakini hili la ushindani lina mambo mawili. Kwanza kuna ushindani wa kumng’oa katika nafasi yake, pili kuna ushindani timilifu wa mabeki wa timu pinzani. Kwa sasa anafaidi yote mawili. Hana upinzani mkubwa kwa watu wanaoitaka nafasi yake, lakini pili hakuna walinzi wengi wanaoweza kumsumbua Kagere.

Mlinzi ambaye amesafiri kwa basi siku mbili kuja Dar es Salaam kucheza na Kagere aliyepumzika vyema katika hoteli ya kando ya bahari anaweza kumkabili vipi Kagere? Lakini pia kuna wachezaji ambao wanatinga Dar es Salaam wakiwa hawajala. Wapo pia walinzi masela ambao usiku mmoja kabla ya mechi walikuwa wanavuta bangi na kulewa.

Kwa hiyo pale alipo amejitengenezea ufalme mzuri tu wa kusogeza siku za kuelekea kustaafu. Na ufalme huu anaufanyia kazi ndani na nje ya uwanja. Anajua anachofanya. Hautamsikia Kagere katika matukio ya kijinga kama kutoroka kambini kwenda kunywa bia.

Analilinda chimbo lake la uzeeni vyema. Anajua bahati aliyonayo kuwa katika nchi jirani ambayo inamlipa vizuri na ambayo ina wachezaji ambao si tishio katika nafasi yake.

Zaidi ya yote, nadhani pia jana nilizungumzia mfumo wetu wa usajili. Unamfanya awe salama zaidi. Mabosi wetu wanaagiza tu wachezaji kutoka Brazil bila ya kuwaona na kuthibitisha ubora wao. Kagere anawatazama tu. Inahitahika skauti ya uhakika ya wachezaji kumng’oa Kagere katika nafasi yake.

Labda upate mtu mkali katika Ligi Kuu ya Ivory Coast, Mali au Senegal na kisha atue Msimbazi. Lakini kwa usajili wa kubahatisha kama wa kina David Molinga, basi Kagere tutaendeleza kumsindikiza sana kwa vigelegele.

Wengine watasema mzee, wengine watasema mchawi, wengine watasema chochote wanachojisikia lakini yeye amepata chimbo la kustaafia na hataki bugudha na mtu. Anajua bahati aliyonayo mkononi mwake.

Tayari ameshatupia mabao matano na ana mkataba wa miaka miwili Simba. Mwishoni mwa msimu huu atakuwa amebakiza mkataba wa mwaka mmoja. Natabiri kwamba msimu ujao atakuwa fiti zaidi kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Simba inamuongezea mkataba mwingine.

Kwa Afrika, heshima kwa hesabu hizi wanazo wachezaji wachache sana wa kulipwa ambao umri umesogea. Ulaya wamefundishwa kusaka mikataba tangu wakiwa watoto. Huku kwetu bado kuna wachezaji ambao hawajui kwamba soka ni kazi ya muda mfupi.

Na wala hawajui kwanini Kagere anaishikilia kazi yake mkononi kwa heshima kubwa. Angekuwa na umri wa miaka 24 si ajabu tungeweza kugongana naye katika disko lakini umri uliopo sidhani kama anaweza kuchezea kazi yake.

Namtabiria ataibuka kuwa mfungaji bora wa ligi yetu kwa msimu mwingine tena. Ni kitu anachostahili kwa sababu anakifanyia kazi. Na hata msimu ujao anaweza kuibuka kuwa mfungaji bora kama wachezaji wetu wa ndani wasipojirekebisha na pia viongozi wasipojirekebisha kutuletea washambuliaji wa ajabu ajabu ambao hawampi upinzani.

Usishangae kumuona Juma Kaseja amerudi katika lango la Taifa Stars na bado tunaimba jina lake. Siyo kwamba hatukuwapa nafasi wengine, lakini mambo waliyotufanyia ndiyo ambayo yamesababisha turudishe miaka nyuma ya kumpa Kaseja lango la Taifa Stars.

Tanzania mchezaji ukiwa fiti unaweza kucheza hata ukiwa na miaka 50. Kama unabisha nenda kamtazame Athuman China anapofanya mazoezi. Utatamani arudi kucheza timu fulani ya Ligi Kuu japo kwa dakika 45 kila mechi. Sio yeye anayetutamanisha zaidi, ni aina ya wachezaji ambao tunao kwa sasa.

Advertisement