Kagere yeye ni mabao tu afunga tena Rwanda

Sunday September 9 2018

 

By Charles Abel

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa Simba, Mnyarwanda Meddie Kagere ameendeleza makali yake ya kufumania nyavu baada ya kuifungia timu ya Taifa ya Rwanda 'Amavubi'  bao la kufutia machozi dhidi ya Ivory Coast walipochapwa mabao 2-1.

Huo ni mchezo wa sita mfululizo katika mashindano tofauti katika ngazi ya klabu pamoja na timu ya taifa kwa Kagere kufunga bao.

Jonathan Kodja ndiye alitangulia kuifungia Ivory Coast iliyokuwa ugenini kufunga bao  kabla ya Max Gradel kuongeza la pili na baadaye Kagere kupachika bao hilo pekee.

Matokeo hayo yameifanya Rwanda iendelee kuburuza mkia kundi H na haina pointi hata moja baada ya kucheza mechi mbili huku Ivory Coast ikikaa kileleni.

Katika kundi L, ambalo Taifa Stars ipo, wenyeji Lesotho walibanwa mbavu baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Cape Verde.

Matokeo hayo yameifanya Lesotho kuendelea kuwa nafasi ya pili ikiwa na pointi mbili sawa na Stars wao wakibebwa na faida ya kuwa na matokeo mazuri dhidi ya Tanzania.

Uganda bado ipo kileleni ikiwa na pointi nne, Stars iko nafasi ya tatu wakati Cape Verde wanashika mkia wakiwa na pointi moja.

Advertisement