Huyo Meddie Kagere wala hapoi

Muktasari:

  • Kagere anayeongoza orodha wa wafungaji akiwa na mabao 22, akiyasaka manne tu kuifikia rekodi ya Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ aliyoiweka mwaka 1998 kwa kufunga mabao 26, aliliambia Mwanaspoti nia yake ni kumaliza kibabe msimu wake wa kwanza.

STRAIKA kinara wa mabao katika Ligi Kuu Bara, Meddie Kagere wa Simba amesema wala hapoi katika kufumaini nyavu licha ya kuwaacha mbali wapinzani wake, huku akipania kutupia tena wakati timu yake itakapovaana na Singida United mjini Singida leo Jumanne.

Kagere anayeongoza orodha wa wafungaji akiwa na mabao 22, akiyasaka manne tu kuifikia rekodi ya Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ aliyoiweka mwaka 1998 kwa kufunga mabao 26, aliliambia Mwanaspoti nia yake ni kumaliza kibabe msimu wake wa kwanza.

Alisema jukumu la mshambuliaji yeyote ni kufunga na yeye anafunga kwa kila nafasi anayoipata, akiwa na nia ya kuisaidia Simba na anakiri huwa anaumia roho pale akishindwa kufanya hivyo.

“Bila kuangalia rekodi zilizopo katika kufunga nilianza kujifikiria mwenyewe kuwa Simba ilinisajili ikiwa mabingwa na wanataka kutetea taji, hivyo kama mshambuliaji natakiwa kufunga mabao ili kuirahisishia timu yangu kufikia malengo yake.”

“Binafsi nataka tutetee ubingwa na kuna kila dalili ya kulitimiza hilo na baada ya hapo nitajifanyia tasmini nimefanya kazi yangu na kufikia yale malengo ya timu kama mshambuliaji ambavyo nilitakiwa kufanya,” alisema. Aliongeza katika mechi tatu zilizosalia dhidi ya Singida itakayopigwa Uwanja wa Namfua, na zile za Mtibwa Sugar na Biashara hawezi kukosa mabao ya kuiongeza hazina yake ya msimu wake wa kwanza.

Kagere alisajiliwa na Simba akitokea Gor Mahia ya Kenya na ameifungia timu hiyo jumla ya mabao 36.