VIDEO: Kagere afunika atwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka Mo Simba Awards

Muktasari:

Ni awamu ya pili kwa Simba kuandaa hafla ya tuzo za MO Simba Awards ambazo zimekuwa zikitolewa kwa washindi wa vipengele tofauti ambavyo hupendekezwa na kamati inayoandaa tuzo hizo.

Dar es Salaam.Nyota ya mshambuliaji Meddie Kagere ndani ya klabu ya Simba imezidi kung'aa baada ya usiku wa leo kutangazwa mshindi wa tuzo ya Mchezaji Bora mwaka na Mfungaji Bora wa msimu katika hafla ya tuzo za MO Simba Awards 2019.

Kagere alishinda tuzo hiyo baada ya kuwapiku nahodha wa timu hiyo John Bocco na kiungo mshambuliaji Clatous Zambia anayetokea nchini Zambia.

Tuzo hizo mbili zimekuja siku chache baada ya Kagere kumaliza msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2018/2019 akiwa mfungaji Bora akipachika mabao 23, huku pia akishika nafasi ya pili kwa kufumania nyavu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa na mabao sita.

Utoaji wa tuzo hizo ulianzia katika kipengele cha Kipa Bora wa mwaka ambayo mshindi kama ambavyo wengi walitegemea alikuwa ni Aishi Manula ambaye amedaka zaidi ya 90% ya mechi zote za timu hiyo msimu huu akimshinda Deogratias Munishi 'Dida' ambaye waliwania naye.

Tuzo hiyo ilitolewa na Mtendaji Mkuu wa Benki ya Equity, Robert Kiboti na tuzo ambayo ilifuata ilikuwa ya Beki Bora iliyobebwa na Erasto Nyoni ambaye aliwashinda Pascal Wawa na Shomari Kapombe ambayo alikabidhiwa na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Ubashiri wa matokeo ya michezo ya SportPesa, Pavel Slavkov.

Kipengele kingine katika tuzo hizo kilikuwa cha Kiungo Bora ambayo kiungo wa Ghana, James Kotei aliinyakua baada ya kuwashinda Mzamiru Yassin na Jonas Mkude.

Kama kuna kipengele ambacho kilionekana kingeleta ushindani mkubwa ni kile cha Mshambuliaji Bora wa klabu hiyo ambacho mshindi wake alikuwa ni nahodha John Bocco ambaye aliwashinda Emannuel Okwi na Meddie Kagere mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu uliomalizika.

Baada ya Bocco, kinda Rashid Juma alitwaa tuzo ya mchezaji bora mwenye umri mdogo wakati Mwanahamisi Omary 'Gaucho'ambaye aliibuka mshindi wa kipengele cha mchezaji bora wa kike wa klabu hiyo.

Kulikuwa na tuzo ya Mchezaji wa wachezaji ambayo mshindi wake anapatikana baada ya kupigiwa kura na wenzake ambayo kwa mara nyingine ilienda kwa Erasto Nyoni na mshambuliaji Meddie Kagere alishinda tuzo ya Mfungaji Bora wa msimu.

Tuzo ya heshima ilikwenda kwa mdhamini wa zamani wa Simba, Azim Dewji ambayo ilifuatiwa na ile ya bao bora iliyokwenda kwa Clatous Chama kutokana na bao lake dhidi ya Nkana FC kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu unaomalizika.

Baada ya vipengele hivyo vyote kutajwa ndipo kikaja kile cha Mchezaji Bora wa msimu ambacho mshindi alikuwa ni Kagere.