Aveva, Kaburu waachiwa kwa dhamana

Tuesday November 5 2019

Aveva- Kaburu -waachiwa-kwa dhamana- Godfrey Nyange- Evans Aveva-Klabu ya Simba

 

By Pamela Chilongola

Dar es Salaam. Waliowahi kuwa viongozi wa juu wa Klabu ya Simba, Evans Aveva na makamu wake Godfrey Nyange 'Kaburu' wameachiwa kwa dhamana baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwaondolea shtaka la utakatishaji wa fedha, huku maombi ya rufaa ya Serikali yakitupiliwa mbali.

Septemba 20, mwaka huu, mahakama hiyo ilitoa uamuzi wa kuwafutia mashtaka mawili ya utakatishaji wa fedha Aveva aliyekuwa rais wa simba na makamu wake Nyange, ambapo washtakiwa hao walitakiwa kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh30 milioni kila mmoja, lakini upande wa Serikali ulikata rufaa kupinga dhamana hiyo.

Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Thomas Simba aliyatupilia mbali maombi yaliyowasilishwa na Serikali ya kupinga uamuzi huo.

"Kitendo cha Serikali kukata rufaa kupitia mawakili wa Serikali haizuii washtakiwa kupewa dhamana, hivyo maombi yaliyotolewa nayatupilia mbali," alisema

Baada ya Hakimu Simba kutoa uamuzi huyo, Wakili wa Serikali Mkuu, Shadrack Kimaro alidai kuwa hawajaridhika na uamuzi uliotolewa na mahakama hiyo, hivyo wanakwenda kukata rufaa katika Mahakama Kuu ya Tanzania.

"Uamuzi yaliyotolewa sijaridhika nayo, hivyo naenda leo hii kukata rufaa katika Mahakama Kuu ya Tanzania," alidai Kimaro.

Advertisement

Baada ya Kimaro kueleza hayo Hakimu Simba alisema hata kama wanakata rufaa haitengui uamuzi wa mahakama hiyo na ndipo wakili huyo alipoieleza mahakama kuwa anajiondoa katika kesi hiyo, kisha Wakili Kimaro alinyanyuka na kutoka nje huku mahakama ikiwa inaendelea.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Novemba 12, 2019 itakapofikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa. Awali Wakili Wankyo alidai kuwa wamewasilisha hati ya kukata rufaa katika Mahakama Kuu sababu ya uamuzi uliotolewa na mahakama hiyo kuwaondolea mashtaka ya utakatishaji wa fedha washtakiwa hao.

 

Alidai kuwa masuala ya dhamana kwa washtakiwa hao yanapaswa kusimama hadi Mahakama Kuu itakapotoa uamuzi.

Katika uamuzi wake mahakama hiyo baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi 10 wa upande wa mashtaka, iliwakuta na kesi ya kujibu washtakiwa hao katika shtaka la kwanza, pili, tatu, nne, saba, nane na tisa isipokuwa katika shtaka la tano na sita ambayo ni ya utakatishaji fedha.

Advertisement