Vigogo Simba wakacha kesi ya kina Aveva

WAKATI rais wa zamani wa Simba, Evance Aveva na Makamu wake Geofrey Nyange'Kaburu' wakikwama kupata dhamana leo Ijumaa, hakuna kiongozi yoyote wa Sasa wa klabu hiyo aliyehudhuria kesi hiyo inayofanyika kwenye Mahakama ya Kisutu.
Aveva na Kaburu wamekutwa na kesi ya kujibu kwa makosa nane huku wakifutiwa makosa mawili ikiwemo kosa la utakatishaji fedha.
Hakimu Mkazi Mkuu, anayeendesha kesi hiyo Thomas Simba jana Alhamisi alisema mshitakiwa Aveva na Nyange dhamana ipo wazi hivyo, masharti ya dhamana ni kuwa na wadhamini wawili ambao  watasaini bondi ya Sh 30 Milioni.
Hata hivyo licha ya watu wengi kuhudhuria kesi hiyo wakiwemo Mashabiki na wanachama wa Simba lakini hakuna kiongozi  yoyote wa klabu hiyo aliyejitokeza kuhudhuria mpaka sasa .
Aveva na Kaburu walidumu katika uongozi Simba kwa muda wa miaka miwili kabla ya kukamatwa ambapo mpaka Leo wamekaa mahabusu kwa siku 814.
Hivi Sasa Simba inaendeshwa kwa mfumo mpya wa uongozi chini ya Bilionea Mohammed Dewji 'Mo'.
Hata hivyo hivi karibuni mwenyekiti wa Simba hiyo, Swedi Nkwabi alijiuzulu nafasi yake na kuwaacha  njia panda  wanachama na mashabiki  wa klabu hiyo ambao hawafahamu mpaka sasa sababu ya kiongozi huyo kujiuzulu akiwa amekaa madarakani kwa muda mfupi.