Aveva, Kaburu wana kesi ya jibu, wapewa dhamana

Muktasari:

Washtakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka kumi yakiwemo ya kula njama, kughushi, kuwasilisha nyaraka za kughushi, kutoa maelezo ya uongo na utakatishaji wa fedha.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemkuta na kesi ya kujibu aliyekuwa Rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva na wenzake katika mashtaka 8 isipokuwa mawili ya utakatishaji fedha.

Mbali na Aveva washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Godfrey Nyange (Kaburu) aliyekuwa Makamu pamoja na aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya usajili Zachariah Hans Poppe.

Washtakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka kumi yakiwemo ya kula njama, kughushi, kuwasilisha nyaraka za kughushi, kutoa maelezo ya uongo na utakatishaji wa fedha.

Uamuzi huo umetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba alisema mshtakiwa Aveva na Nyange dhamana ipo wazi hivyo masharti ya dhamana kuwa na wadhamini wawili ambao watakaosaini bondi ya Sh30 milioni.

Kutokana na hatua hiyo washtakiwa hao wamepatiwa masharti ya dhamana kwa sababu mashtaka ya utakatishaji fedha yaliwanyima dhamana na yameondolewa.

Simba alisema jukumu la kuthibitisha shtaka kwa washtakiwa ni la upande wa mashtaka, pia kwa kosa moja moja na sio kwa kutegemeana.

Hakimu Simba alisema baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi 10 wa upande wa mashtaka ambapo amewakuta na kesi ya kujibu washitakiwa hao katika shtaka la kwanza, pili, tatu, nne, saba, nane na tisa isipokuwa katika shitaka la tano na sita ambayo ni ya utakatishaji fedha.

"Mashitaka ya utakatishaji fedha ambayo yaliyokuwa yanawanyima dhamana washitakiwa hayapo, je upande wa mashtaka wana pingamizi na dhamana?,"alisema Simba

Baada ya kueleza hayo, Wakili wa Takukuru, Leornad Swai amedai hawana pingamizi ndipo Hakimu Simba aliwapatia masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili watakaosaini Bondi ya Sh30 milioni kwa kila mmoja.

Hata hivyo washtakiwa Aveva na Nyange wameshindwa kutimiza masharti ya dhamana hivyo wamerudishwa rumande na shauri hilo limeahirishwa hadi Septemba 20, 2019 kwa ajili ya washtakiwa kuanza kujitetea.

Katika shtaka la kwanza, Aveva na Kaburu walikula njama ya kutenda kosa la matumizi mabaya ya madaraka.

Shtaka la pili la Aveva na Kaburu wanadaiwa kutumia vibaya madaraka yao kwa kuandaa fomu ya kuhamisha fedha Dola za Kimarekani 300,000 kutoka kwenye akaunti ya Simba iliyoko benki ya CRDB Azikiwe kwenda kwenye akaunti binafsi ya Aveva iliyoko benki ya Barclays.

Shtaka la tatu linalowakabili Aveva na Kaburu inadaiwa kwa pamoja walighushi nyaraka iliyokuwa ikionesha Simba inalipa mkopo wa Dola za 300,000 kwa Aveva kitu ambacho sio kweli.

Katika shtaka la nne Aveva katika banki ya CRDB anadaiwa kutoa nyaraka ya uongo ikionesha Simba wanalipa mkopo wa Dola za Kimarekani 300,000.

Shtaka la tano, Aveva anadaiwa kuwa katika Benki ya Baclays Mikocheni alijipatia Dola za Kimarekani 187,817 wakati akijua zimetokana na kughushi.

Shtaka la sita, Kaburu anadaiwa kumsaidia Aveva kujipatia Dola za Kimarekani 187,817 kutoka kwenye akaunti ya Simba wakiwa wanajua fedha hizo zimetokana na zao la kughushi.

Shtaka la saba linawakabili Aveva, Kaburu na Hans Poppe ambao wanadaiwa kughushi hati ya malipo ya kibiashara wakionesha kwamba nyasi bandia zilizonunuliwa na Simba zina thamani ya Dola za Kimarekani 40,577 huku wakijua kwamba siyo kweli.

Katika shtaka la nane, Aveva anadaiwa kuwasilisha hati ya malipo ya kibiashara ya uongo kwa Levison Kasulwa kwa madhumuni ya kuonyesha kwamba Simba wamenunua nyasi bandia zenye thamani ya Dola za Kimarekani 40,577.

Shtaka la mwisho Aveva, Kaburu na Hanspope wanadaiwa kuwasilisha nyaraka za uongo kuonyesha kuwa Simba imenunua nyasi bandia zenye thamani ya Dola za Kimarekani 40,577.