Yanga mpya huku Mayele kule Chivaviro
Muktasari:
- Iko hivi; Yanga inahitaji huduma ya mshambuliaji huyo aliyefunga mara sita mpaka sasa kwenye Shirikisho sawa na staa wao, Fiston Mayele ili aje kuimarisha zaidi safu yao ya ushambuliaji kwa msimu ujao.
YANGA inapambana kuinasa saini ya mshambuliaji wa Marumo Gallants, Ranga Chivaviro wakichuana na Azam FC lakini kuna eneo wamelainishiwa washindwe wenyewe.
Iko hivi; Yanga inahitaji huduma ya mshambuliaji huyo aliyefunga mara sita mpaka sasa kwenye Shirikisho sawa na staa wao, Fiston Mayele ili aje kuimarisha zaidi safu yao ya ushambuliaji kwa msimu ujao.
Akili ya Kocha Nasredeen Nabi ni Mayele acheze na Chivaviro kwenye ushambuliaji, lakini anajiandaa kisaikolojia pia kama itatokea tajiri akamnunua Mayele, Yanga ifanye biashara na kubakia kwenye ubora uleule.
Mwanaspoti ambalo lilikuwa Afrika Kusini wiki iliyopita, linajua kwamba Chivaviro hataki kubaki tena Marumo baada ya kikosi hicho kushuka daraja nchini Afrika Kusini na sasa ofa zake kubwa mbili ni zile za Yanga na Azam wote wakimfuata kwa ofa rasmi.
Yanga inaendelea na mchakato huo kiakili zaidi kupitia kwa injinia Hersi Said ambaye Mwanaspoti linafahamu bosi huyo yuko kwenye hatua nzuri ya kumnasa mshambuliaji alipokuwa nchini Afrika Kusini wiki iliyopita.
Mwanaspoti linafahamu kuwa Hersi mbali na kukutana na vigogo wa Marumo ambao nao hawakumwekea ngumu pia alikutana kwa siri na mshambuliaji huyo na meneja wake na kuweka kila kitu sawa.
Kabla ya Hersi kufikia hatua hiyo tayari Chivaviro ambaye ni raia wa Afrika Kusini akiwa na asili ya Zimbabwe ameliambia Mwanaspoti kwamba anatamani kujiunga na Yanga na sio klabu nyingine nje ya hapo kutoka Tanzania.
Chivaviro amevutiwa na vaibu la mashabiki wa Yanga lakini pia ubora wa kikosi chao akitaka kurudi nao kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao haswa baada ya kusikia mkakati wao mpya wa kufanya vizuri.
"Nimevutiwa sana na mashabiki wao sisi hatuna mashabiki kama hawa timu yetu ni ndogo lakini pia napenda kikosi chao naamini kwa ubora walionao inakupa imani ya kufikia malengo yako kama mchezaji,"alisema Chivaviro ambaye anahusishwa pia kujiunga na Kaizer Chiefs ingawa sasa ametulia sehemu na familia yake.
Mbali na Hersi Mwanaspoti linafahamu kuwa tayari mshambuliaji amezungumza kwa simu na kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi akimhakikishia kwamba endapo atakubali kujiunga nao ataendeleza moto wake wa kufunga.
Hesabu za Chivaviro Yanga inataka kujiweka mguu sawa endapo watampoteza mshambuliaji wao aliye kwenye moto Mayele ambaye tayari ameanza kutolewa macho na klabu kubwa Afrika zikivutiwa na kasi yake ya kufunga.
Mayele amebakiza dakika 180 za mechi mbili za fainali watakapokutana na USM Alger kufunga zaidi kumkimbia Chivaviro ambaye kwasasa analingana naye kwa mabao baada ya wote kufunga katika mchezo uliopita wa nusu nainali ya pili ambayo Yanga walishinda kwa mabao 2-1.