Unataka kuwa kama Bocco basi zingatia haya

Muktasari:
Vitu vikubwa anavyovizingatia katika maisha yake ya soka ni idhamu, bidii, kutoizowea kazi na mazoezi kuwa sehemu ya maisha yake ya kila siku.
JE, unataka kuwa na mafanikio kama ya straika wa Simba, John Bocco? Ni rahisi endapo ukiamua kuzingatia misingi anayoiamini katika tasnia ta soka.
Bocco ni miongoni mwa wachezaji wanaotazamwa kama kioo hata na baadhi ya wachezaji wa Ligi Kuu Bara, huku madaraja ya chini ndio usipime, kwani asilimia kubwa wanapenda uchezaji wake.
Mwanaspoti limepiga naye stori za hapa na pale kwani namna anavyozungumza anaonekana ni mchezaji anayethamini kazi yake na kuzingatia miiko ya soka.
Vitu vikubwa anavyovizingatia katika maisha yake ya soka ni nidhamu, bidii, kutoizowea kazi na mazoezi kuwa sehemu ya maisha yake ya kila siku.
KWAKE NIDHAMU TU
Bocco anasema soka linachezwa sehemu za wazi akimanisha mchezaji kama anakosa nidhamu, basi uwezo wake unakuwa unajitafsiri ndani ya dakika 90 iwapo anajitunza au la.
“Nidhamu ya soka ni pana, mfano mzuri ule wa wachezaji wa Ulaya namna ambavyo maisha yao yanakuwa, mfano ndani na nje ya uwanja, mfano wanavyozingatia muda wa kufanya vitu vyao,” anasema na kuongeza:
“Lazima mchezaji awe anazingatia muda sahihi wa kufanya mazoezi, wa kula na kuupumzisha mwili ambao ndio kitendea kazi kikubwa cha soka, huwezi kucheza vyema kama haupo fiti.”
KUTOZOEA KAZI
Anasema siyo soka pekee ambalo mchezaji akileta mazowea nalo inakuwa ngumu kufika mbali, bali anaamini kila kazi inatakiwa kuiheshimu ili kuifanya kwa ubora kila mara.
“Mtu ambaye hana mazowea na kazi yake, basi anakuwa mbunifu kila anapofanya kitu, ndio maana unakuta wachezaji wa Ulaya wana vitu vya aina yake miguuni mwao vinavyofanya viwe na mvuto kwa mashabiki wao,” anasema.
KWAKE BIDII KWANZA
Anasema pamoja na kwamba amefanikiwa kuchezea timu kubwa, haimfanyi awe mchezaji wa kufanya vitu kwa ulegevu, bali anaongeza bidii kila wakati ili kuhakikisha kila anapoingia uwanjani anakuwa na jipya.
“Anayefanya kwa ulegevu basi hawezi kufanikiwa, bidii kwa kila kitu ni msingi mzuri wa kufikia ndoto yako, naamini waliopo madaraja ya chini wana uwezo wa kuishi kile wanachotamani kwa sharti la kujituma kwa bidii.”
MAZOEZI KAMA IBADA
Bocco anasema kama kuna kitu mchezaji anapaswa kukifanya, basi rafiki wa maisha yake ya kila siku ni kufanya mazoezi iwe kwenye timu ama mapumziko.
“Mazoezi yanamfanya mchezaji awe fiti, awe na pumzi na kasi, ndio maana anapaswa kuyapenda, ndio kitu ambacho ninaweza kuwatia moyo wale ambao wapo madaraja ya chini,” anasema.
Baadhi ya wachezaji wa Ligi Kuu Bara ambao wamewahi kukiri kupenda uwezo wa Bocco ni Miraji Athuman (Simba), Adam Salamba (yupo Kuwait), Blaise Bigirimana (Namungo) na wengine wengi.
Kwa ushuhuda huo Bocco anasema inampa faraja kuona kuna watu wanakikubali kiwango chake na kwamba inampa nguvu ya kujituma zaidi.