Bocco aanza mdogo mdogo

Muktasari:

Katika mazoezi ya leo asubuhi Bocco ambaye ni nahodha wa Simba,  alikuwa   karibu na kocha wa viungo Adel Zerane akimuelekeza baadhi ya mazoezi.

Mshambuliaji wa  Simba, John Bocco  amerejea  katika kikosi cha timu hiyo, ambacho kinautumia  Uwanja wa Gymkhana, Dar es Salaam kujiandaa  na mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mtibwa Sugar, Septemba 13.

Bocco alipata majeraha ya goti katika mchezo wa  Ligi ya   Bingwa Afrika dhidi ya Ud Songo, Agosti 25   na alilazimika kukaa nje kwa takribani wiki tatu.

Katika mazoezi ya leo asubuhi Bocco alikuwa yupo karibu na kocha wa viungo Adel Zerane akimuelekeza baadhi ya mazoezi.

Mshambuliaji huyu hakujichanganya na mazoezi ya wechezaji  wenzake bali alikuwa na programu za mazoezi ya viungo ambayo alikuwa akiyafanya kwa pembeni.

Urejeo wa Bocco katika kikosi hicho  unatoa taswira nzuri katika benchi la ufundi baada ya mara kwa mara kocha mkuu, Patrick Aussems kusema kukosekana kwa mchezaji huyo kunaweka pengo katika kikosi chake.

Katika upande wa Ligi Kuu, Bocco aliukosa mchezo mmoja ambao ni  dhidi ya JKT  Tanzania ambao Simba waliibuka na ushindi wa mabao 3-1, uwanja wa uhuru.