Fountain Gate, Tanzania Prisons kazi imeanza tena

Muktasari:
- Leo timu hizo zinavaana katika mechi ya kwanza ya play-off ya kusaka kubaki Ligi Kuu kwa msimu ujao kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, uliopo mjini Babati mkoani Manyara, Fountain ikiwa mwenyeji kabla ya kurudiana Juni 30 ili mshindi wa jumla kusalia katika ligi hiyo.
WAKATI watani wa jadi wa soka la Tanzania, Simba na Yanga zikiwa zimemalizana jana katika mechi ya kiporo cha Dabi ya Kariakoo, maafande wa Tanzania Prisons na Fountain Gate wanashuka uwanjani kuanza upya kazi ya kupambana kuepuka kushuka daraja.
Leo timu hizo zinavaana katika mechi ya kwanza ya play-off ya kusaka kubaki Ligi Kuu kwa msimu ujao kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, uliopo mjini Babati mkoani Manyara, Fountain ikiwa mwenyeji kabla ya kurudiana Juni 30 ili mshindi wa jumla kusalia katika ligi hiyo.
Timu hizo zinakutana baada ya Fountain kumaliza nafasi ya 14 kwenye ligi na pointi 29, ikishinda mechi nane, sare tano na kupoteza 17, huku Prisons ikimaliza ya 13 na pointi 31, kufuatia kushinda minane, ikitoka sare saba na kupoteza 15.
Fountain mechi ya mwisho ya ligi msimu huu 2024-2025 ilicheza Juni 22 na kuchapwa 3-2 ikiwa nyumbani na Azam FC, huku Prisons ikilazimisha sare ya 3-3 ugenini dhidi ya Singida Black Stars.
Rekodi zinaonyesha timu hizo zilipokutana katika mechi ya mwisho ya Ligi Kuu msimu huu iliyopigwa kwenye uwanja huo, Februari 26, 2025, wenyeji Fountain walishinda 1-0 lililotokana na penalti ya dakika ya 28 iliyopigwa na beki Amos Kadikilo.
Hata hivyo, mechi ya kwanza baina ya timu hizo iliyopigwa Uwanja wa Sokoine Mbeya, Prisons ilishinda 3-2 Oktoba 1, 2024, jambo linaloongeza mvuto na msisimko mkubwa wakati miamba hiyo inapoenda kukutana leo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha wa Fountain Gate, Mohamed Ismail ‘Laizer’, alisema anatambua presha iliyopo kutokana na uhitaji wa kila timu, ingawa amejipanga kukabiliana na hali hiyo huku akiwataka wachezaji kucheza kwa tahadhari kubwa.
“Mechi yoyote ya mtoano (play-off) unayoanzia nyumbani hubeba sana presha kuanzia kwa benchi la ufundi na wachezaji kiujumla, japo nimejaribu kukaa nao chini na kuwajenga kisaikolojia ili tutumie vizuri uwanja wetu wa nyumbani,” alisema Laizer.
Kwa upande wa Kocha wa Tanzania Prisons, Amani Josiah alisema kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wa timu hiyo katika mechi iliyopita na Singida Black Stars ndicho anachotaka kuona kikiendelea kufanyika, licha ya ugumu wa wapinzani wao.
“Kutoka nyuma mabao 3-0 hadi 3-3 dhidi ya Singida Black Stars sio jambo jepesi kuona likitokea, wachezaji wote pamoja walionyesha kujituma sana na kutokata tamaa, hali hiyo tunahitaji kuitumia kwa mechi zetu zote mbili,” alisema Josiah.
Mechi ya marudiano kati ya timu hizo itapigwa Jumatatu ya Juni 30, kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, ambapo mshindi wa jumla atacheza Ligi Kuu Bara msimu ujao, huku itakayopoteza itajiuliza tena katika play-off dhidi ya Stand United. Kama timu ya Ligi Kuu itafungwa na Stand itashuka daraja ikiungana na KenGold na Kagera Sugar zilizotangulia mapema na Stand kupanda daraja.
Stand iliyoshiriki Ligi ya Championship msimu huu, ilipata nafasi hiyo baada ya kuitoa Geita Gold katika mechi ya mtoano kwa jumla ya mabao 4-2.