Bao la kuotea la Bocco gumzo, Simba yaichapa Polisi Tanzania

Muktasari:
Ushindi huo unaifanya Simba kufikisha pointi 50, kileleni mwa Ligi Kuu Tanzania ikifuatiwa na Azam (37), Yanga (31)
Dar es Salaam. Bao la mshambuliaji John Bocco akiwa katika eneo la kuotea pamoja na lile la Ibrahim Ajibu limetosha kuipa Simba ushindi mabao 2-1 dhidi ya Polisi Tanzania kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ushindi huo unaifanya Simba kufikisha pointi 50, kileleni mwa Ligi Kuu Tanzania ikifuatiwa na Azam (37), Yanga (31).
Bocco alifunga bao hilo katika dakika 57, akipokea pasi ya Clatous Chama akiwa katika eneo la kuotea na kutuliza mpira kabla ya kupiga shuti lililojaa wavuni.
Mwamuzi wa kati Hance Mabena alionyesha mpira kupelekwa kati kuashilia bao, lakini mwamuzi msaidizi Joseph Masija kutoka Mwanza yeye alisimama akiwa hajarudi kati kuonyesha kwamba goli limefungwa.

Hali hiyo iliwafanya wachezaji wa Polisi Tanzania kubaki wakishangaa kuona maluweluwe yaliyokuwa yamefanywa na Mwamuzi Mabena.
Kipa wa Polisi Tanzania, Mohamed Yusuf alionekana kumfuata mwamuzi msaidizi, Joseph Masija na kuzungumza naye kwa ukali wakati huo huo mwamuzi wa kati Mabena alimfuata na kumpa kadi ya njano.
Tukio la bao hilo ni muendelezo wa malalamiko ya wadau wa soka kwa waamuzi kushindwa kutafsiri vizuri sheria ya kuotea inayoonekana kuwapa faida zaidi Simba katika siku za karibuni.

Mshambuliaji Ajibu akiingia akitokea benchi alifunga bao la pili la Simba katika dakika 90+5 akiunganisha pasi Meddie Kagere huku Sixtus Sabilo akifunga bao la kufutia machozi kwa Polisi Tanzania katika dakika 22.
Polisi Tanzania ilianza vyema mchezo huo kwa kuumiliki na kuonyesha kandanda safi ndani ya dakika 15 za kwanza huku hatari nyingi zikishia mikononi wa kipa wa Simba, Benno Kakolanya.
Dakika ya 22, Sabilo aliiandikia timu yake bao baada ya kupokea pande safi kutoka kwa Mateo Antony na kuipita ngome ya ulinzi ya Simba kisha kukwamisha mpira kambani.

Bao hilo lilionekana kuwaamsha Simba na kuanza kusaka nafasi ya kusawazisha, lakini hadi timu zinakwenda mapumziko Polisi Tanzania ilikuwa kifua mbele kwa bao 1-0.
Kushindwa kuwaka kwa baadhi ya taa kutokana kukatika kwa umeme kulifanya mwamuzi wa mchezo huo, Hance Mabena kutoka Tabora kujadiliana na wenzake wakati timu zikiingia kipindi cha pili.
Mabena alitumia dakika mbili kufanya majadiliano na wenzake kabla ya kuanza kwa mchezo huo dakika 45 za kipindi cha pili.
Mabadiliko yaliyofanywa na kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck ya kumtoa Sharaf Shiboub na nafasi yake kuchukuliwa na Ajib yalizaa matunda dakika ya 57 baada ya Bocco kufunga bao.
Zikiwa zimesalia sekunde chache mchezo kumalizika, Ajibu aliipatia timu yake bao la ushindi baada ya kupokea mpira kutoka kwa Francis Kahata.

Polisi Tanzania yagoma kuingia vyumbani
Polisi Tanzania hawakutumia chumba cha kubadilishia nguo kama ilivyokawaida kwa timu, huku ikitumia chumba ambacho hutumiwa na waandishi wa habari kwa shughuli mbalimbali.
Vikosi
Simba: Beno Kakolanya, Haruna Shamte, Mohamed Hussein, Kennedy Juma, Tairone Santos, Gerson Fraga, Hassan Dillunga, John Bocco, Clatous Chama na Francis Kahata.
Polisi Tanzania: Mohammed Yusuf, Elias William, Yassin Salum, Mohamed Ally, Iddy Mobby, Pato Ngonyani, Sixtus Sabilo, Hassan Maulid, Mateo Anton, Marcel Kaheza na Jimmy Shoji.