Kuumia Bocco kwa amnyima usingizi Aussems

Muktasari:

Bocco aliumia dakika ya 17 baada ya kugongana na Frank Domayo na nafasi yake kujazwa na Clatous Chama katika mchezo walioshinda mabao 4-2 na kutwaa Ngao ya Jamii kwa mara ya tatu mfululizo.

Dar es Salaam. Kocha wa Simba, Patrick Aussems amesema ana hofu baada ya nahodha wake John Bocco kuumia katika mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Azam.
Bocco aliumia dakika ya 17 baada ya kugongana na Frank Domayo na nafasi yake kujazwa na Clatous Chama katika mchezo walioshinda mabao 4-2 na kutwaa Ngao ya Jamii kwa mara ya tatu mfululizo.
Aussems alisema hana hakika Bocco ameumia kwa kiasi gani, lakini ameingia hofu kwa kuwa Simba ina mechi ngumu  ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya UD Songo, Jumapili wiki hii.
“Nina majeruhi Ajibu na Bocco sina mtu wa kusaidiana na Kagere wiki ijayo, lakini naamini tatizo la Bocco si kubwa ngoja tuone,”alisema Aussems.
Akizungumzia ushindi dhidi ya Azam, alisema alitarajia kupata mabao sita au saba katika mchezo huo, lakini washambuliaji wake walikosa umakini ndani ya eneo la hatari. Aussems alidai walimiliki mchezo dakika zote 90 ingawa kuliko na dosari ndogo alizosema atazifanyia kazi kabla ya kuvaana na Ud Songo ya Msumbiji.
Kocha alisema moja ya kasoro anayopaswa kuifanyia kazi ni mabeki wa kati Pascal Wawa na Erasto Nyoni aliodai walifanya makosa ya kimchezo dhidi ya Azam.