Kile chuma hiki hapa! Ni straika Mserbia, atambulishwa Simba

Kile chuma hiki hapa! Ni straika Mserbia, atambulishwa Simba

SIMBA hawatanii, kwani baada ya kumtambulisha nyota mpya kutoka Nigeria, Nelson Okwa ambaye jana aliungana na wenzake mazoezini, mabosi wa klabu hiyo wamewasapraizi mashabiki wao kwa kumleta straika wa mabao kutoka Serbia, Dejan Georgijevic.

Straika huyo aliyekuwa akikipiga timu ya NK Domzale iliyopo Ligi Kuu ya Slovania, ndiye ambaye Mwanaspoti liliripoti mapema wiki hii kwamba alikuwa mbioni kufunga usajili wa Msimbazi sambamba na Okwa aliyesajiliwa kutoka Rivers United ya Nigeria.

Dejan aliyewahi kukipigia Bosnia & Herzegovina, Hungary, Serbia na Kazakhstan ni kati ya nyota watakaotambulishwa kwenye tamasha la Simba Day litakalofanyika Jumatatu akiletwa ili kuziba nafasi ya Cesar Manzoki aliyekuwa kwenye mipango ya mabosi wa Simba, lakini dili lake limebuma.

Manzoki ambaye leo atakuwa Uwanja wa Mkapa na kikosi cha Vipers ya Uganda ili kuvaana na Yanga kwenye Kilele cha Wiki ya Mwananchi, atajiunga na Simba kwenye dirisha dogo baada ya klabu yake kukaza kumuachia licha ya kusaliwa na mkataba wa miezi miwili.

Kutokana na hali hiyo ndipo mabosi wa Simba wakaamua kumvuta straika huyo wa Serbia ambaye rekodi zinaonyesha ana umri wa miaka 28 na amewahi kubeba ubingwa wa Ligi ya Serbia na kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na timu ya Partizan Bergrade ya nchini kwao, huku akisifika kwa kufunga na kutoa asisti. Licha ya kucheza kama straika, lakini Dejan ambaye ni chaguo la Kocha Zoran Maki aliyemleta pia beki wa kati Mohamed Ouattara anamudu pia kucheza kama winga wa kulia na kushoto kutokana na uwezo wake wa kutumia miguu yote, akisifika kwa mipira ya vichwa.

Japo mabosi wa Simba wamekuwa wagumu kuweka bayana dili hilo, lakini Mwanaspoti lilipenyezewa mapema tangu timu ikiwa kambini kwamba Dejan ndiye atakayefunga usajili wa timu hiyo na huenda akakabidhiwa jezi kati ya 7, 8 ama 14 zilizokuwa zikivaliwa na Chris Mugalu, Rally Bwalya na Meddie Kagere ambao wametimka klabuni hapo.

Bwalya aliuzwa Afrika Kusini, wakati Kagere na Mugalu walitemwa hivi karibuni na kocha Zoran. Kagere ameibukia Singida Big Stars.

Rekodi zinaonyesha katika miaka 12 iliyopita mshambuliaji huyo amekipiga katika timu kama 12, akifunga jumla ya mabao 52 katika mechi 226 za ligi tofauti, pia amewahi kuzichezea timu za vijana za Serbia za U19, U18 na U17 alikoichezea mechi 16 na kufunga mabao nane.

Kutua kwa mchezaji huyo kunaifanya Simba kwenye eneo la ushambuliaji kuwa na Pape Ousmane Sakho, Okwa, John Bocco, Clatous Chama, Kibu Denis na Peter Banda.