Prime
Barker ‘amkomalia’ nyota Mamelodi Sundowns
KUNA hesabu za kusuka kikosi kwa ajili ya msimu ujao wa 2026-2027 anazipiga Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker na jambo la kwanza ni kuhakikisha baadhi ya nyota aliofanya nao kazi vizuri kipindi cha takribani miezi sita aliyokuwa klabuni hapo kuanzia Desemba 2025 hadi Julai 4,2026 walipocheza fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB, wanaendelea kubaki.
Mwanaspoti tayari limeripoti Anicet Oura haendi popote kutokana na Barker kuhitaji aendelee kuwa naye licha ya kuelezwa kuna ofa tatu kutoka klabu za Ulaya zikihusishwa na kiungo huyo raia wa Ivory Coast, Simba ikikamilisha usajili wa winga, Keletso Makgalwa raia wa Afrika Kusini anayetokea Sekhukhune United ya nchini humo.
Katika kile alichopendekeza kubakisha nyota anaohitaji kuendelea nao, tayari taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema, mshambuliaji aliyekuwa akicheza kwa mkopo kikosini hapo, Seleman Mwalimu, ataendelea kuwepo kwa msimu ujao wa 2026-2027.
Uamuzi wa Simba kuendelea kubaki na Mwalimu, umetokana na mapendekezo ya Barker kuhitaji huduma yake iendelee klabuni hapo, huku mshambuliaji mwingine, Jonathan Sowah akiondoka na kurejea Singida Black Stars.
Mwalimu ambaye alikuwa Simba kwa mkopo wa msimu mmoja akiwa ni mali ya Wydad AC ya Morocco aliyojiunga nayo Januari 2025 kwa mkataba wa miaka minne akitokea Singida Black Stars, sasa ataendelea kuichezea Simba hadi 2027-2028 baada ya kusaini miaka miwili.
Chanzo cha ndani kutoka Simba, kilisema viongozi wa timu hiyo walifanya mazungumzo mapya na Wydad, ambayo ililiridhia kumuachia mshambuliaji huyo.
“Wakati tunamchukua Mwalimu tuliambiwa akimaliza mkataba wa mkopo wa mwaka mmoja, tunatakiwa turudi mezani kuzungumza nao, tumefanya hivyo wamekubali aendelee kusalia na sisi,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;
“Lakini kwa sasa ni tofauti, tunabaki na Mwalimu baada ya kukubaliana na Wydad watuuzie moja kwa moja, hivyo tumempa mkataba wa miaka miwili hadi 2028.
“Kocha amesema Mwalimu ni mchezaji mzuri na alishaingia katika mfumo wake, hivyo alituambia anahitaji awepo katika kikosi chake cha msimu ujao.”
Ikumbukwe Mwalimu ambaye Mtandao wa Transfermarket unahusika na takwimu za mpira wa miguu, uhamisho, tetesi, thamani za wachezaji, makocha na klabu unaonesha amezaliwa Januari 19, 2006 akiwa na miaka 20 hivi sasa, alijiunga na Wydad Casablanca kwa uhamisho wa Euro 288,000 (Sh881.8 milioni) akitokea Singida Black Stars.
Uhamisho huo ulimfanya mshambuliaji huyo kuvunja rekodi ya Simon Msuva wakati akiondoka Yanga na kujiunga na Difaa El Jadida mwaka 2017 ambaye alisajiliwa kwa Dola 150,000 (Sh337 milioni) na wakati huo kiungo huyo alikuwa akishikilia rekodi ya mchezaji wa Kitanzania aliyesajiliwa kwa mkwanja mrefu zaidi Morocco.
Taarifa kutoka Morocco zinabainisha, awali wakati Simba inamchukua Mwalimu kwa mkopo, ilitoa kiasi cha Euro 50,000 (Sh153 milioni). Kwa sasa thamani yake sokoni inaonesha ni Euro 150,000 (Sh452.5 milioni za Tanzania).
Katika kikosi cha Simba msimu wa 2025-2026, Mwalimu ndiye alikuwa kinara wa mabao akifunga tisa kwenye Ligi Kuu ya NBC, akifuatiwa na kiungo mshambuliaji Clatous Chama aliyamaliza na mabao manane.
Wakati msimu wa 2024-2025 akiwa na Fountain Gate aliyokuwa akiitumikia kwa mkopo, Mwalimu alifunga mabao sita, jambo ambalo staa wa zamani wa Simba, Yanga na Stars, Dany Mrwanda amesema:
“Ingawa amecheza kwa mkopo, lakini ni mzawa mwenye uwezo wa kufunga mabao mengi, kwa mtazamo wangu naona Simba imefanya vizuri kusalia na Mwalimu.”
Mwingine aliyeunga mkono hilo ni mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Malimi Busungu na amesema: “Mwalimu amepewa nafasi akaonyesha, hivyo anastahili kuendelea kuwepo Simba, wasichokijua wengi wao ni ukiona Simba na Yanga inakaa na mchezaji, ujue huduma yake ni muhimu, hizo klabu zipo kwa ajili ya kuwatumia wachezaji walio tayari, kutokana na ushindani na maono yao makubwa.”
ISHU YA GOLINI
Mbali na Mwalimu, imeelezwa kocha Barker ametaka kipa Djibrilla Kassali aendelee kusalia ndani ya kikosi hicho, huku Moussa Camara akikosa nafasi baada ya mkataba wake kumalizika, lakini kwa Hussein Abel ikitajwa ataondolewa na Yakoub Suleiman akipewa nafasi ya kuendelea kujiuguza majeraha ya mguu kutokana na kufanyiwa upasuaji takribani miezi miwili nyuma.
Camara aliyetua Simba msimu wa 2024-2025, alikumbwa na majeraha yaliyomuweka nje ya uwanja kwa takribani msimu mzima wa 2025-2026, hivyo nafasi yake akasajiliwa Kassali, huku raia huyo wa Guinea akiondolewa kwenye mfumo hadi mkataba wake ulipomalizika.
“Mchezaji mwingine ambaye viongozi tulipendekeza aondoke lakini kocha anataka aendelee kusalia ni Neo Maema, ila bado suala lake halijafikiwa mwafaka,” kilisema chanzo hicho.
Maema anayecheza nafasi ya kiungo mshambuliaji, naye ameitumikia Simba msimu wa 2025-2026 kwa mkopo akitokea Mamelodi Sundowns ya kwao Afrika Kusini. Mkataba wake wa mkopo umemalizika, hivyo ili abaki Simba, mazungumzo mapya yafanyike kama ilivyokuwa kwa Mwalimu.
SABA WAAGWA
Mchana wa jana, klabu ya Simba ilitangaza kuwaaga nyota wake saba ambao ni Chamou Karaboue, Naby Camara, Edwin Balua, Joshua Mutale, Awesu Awesu, Omari Omari na Moussa Camara.
“Wachezaji hawa hawatakuwa sehemu ya kikosi chetu kwa msimu wa 2026-2027. Tunathamini mchango wa wachezaji hao na kujitoa kwao kwa ajili ya kuipigania nembo ya klabu kwa kipindi chote walichokuwa wakiitumikia Simba.
“Ungozi wa klabu unawatakia kheri wachezaji hao katika maisha yao mapya ya soka nje ya Simba,” imebainisha taarifa hiyo.
Kuagwa kwa nyota hao, kunatoa nafasi kwa klabu hiyo kuendelea kuingia sokoni kusaka majembe mengine ya kukipambania kikosi hicho kilichomaliza msimu wa 2025-2026 kwa kutwaa Kombe la Shirikisho la CRDB ilipoifunga Azam bao 1-0 na Kombe la Muungano ikiichapa Yanga bao 1-0.