Usajili Simba wa kimkakati

SIMBA imeshtua wengi. Imefanya usajili uliozua maswali na hasa baada ya kuachana na mawinga na viungo wao wawili mafundi wa kucheza na mpira, Clatous Chama aliyeuzwa RS Berkane ya Morocco na Luis Miquissone aliyenyakuliwa na Al Ahly ya Misri.
Fasta, mabosi wa klabu hiyo wamesajili majembe mengine kutoka nje ya nchi wanaotajwa kama ndio watakaoziba nafasi za kina Chama na Luis, lakini na wengine wa kuimarisha kikosi chao kwa msimu ujao wa mashindano.
Usajili uliofanywa na Simba kwa kuchukua wachezaji wenye umri mdogo imetoa taswira ya kutengeneza kikosi chao cha kudumu muda mrefu na pia fedha kama zitatokea dili za kuwauza kama ilivyotokea kwa Luis na Chama ambao wamebebwa kwa fedha ndefu, japo inafanywa siri kubwa.
Mwanaspoti linakuchambulia maingizo mapya Msimbazi kwa data ili kuonyesha takwimu za umri wa kikosi cha sasa na kilichopita, na wadau wamekichambua wakiipa tano Simba kufanya usajili wa kimkakati.
KIKOSI KILICHOPITA
Msimu uliopita wa 2020-2021, Simba ilikuwa na wachezaji 13 wa kigeni katika Ligi Kuu Bara na wale wa kucheza michuano ya kimataifa.
Wachezaji hao walikuwa na wastani wa umri wa miaka 30, huku waliokuwa na umri mkubwa zaidi ni Meddie Kagere na Pascal Wawa waliokuwa na miaka 35.
Mbali na kina Kagere, lakini mchezaji aliyekuwa na umri mdogo kati ya hao alikuwa Taddeo Lwanga kutoka Uganda mwenye umri wa miaka 23, Rally Bwalya (26) na Junior Lokosa (27) ambaye hata hivyo hakutumika.
Wengine ni Bernard Morrison (28) na Francis Kahata (30) aliyetumiwa mwishoni kwenye mechi za kimataifa tu, beki Joash Onyango (28), Perfect Chikwende (28), Peter Muduhwa (28) ambaye naye hakutumika kabisa, Chama (30) na Chris Mugalu (31).
Katika msimu huu wachezaji wanne waliondoka ambao ni Chama aliyetimka baada ya kuuzwa katika klabu ya RS Berkane, Luis katimkia katika klabu ya Al ahly, huku Kahata akiondoka Simba baada ya mkataba wake kumalizika na Gerson Fraga pia aliondoka kutokana na kusumbuliwa na majeraha.
JESHI JIPYA
Simba imeingiza wachezaji wapya watano katika msimu wa 2021/22 ambao kwa pamoja wana wastani wa miaka 23. Wachezaji hao ni Peter Banda mwenye miaka 20 aliyekuwa anacheza kwa mkopo Sheriff Tiraspol ya Moldova kutokea Nyasa Big Bullets FC ya nchini kwao, Malawi.
Duncan Nyoni ‘Monster’ (23) kutoka klabu ya Silver Strikers ya kwao Malawi anakuwa ni mchezaji wa pili baada ya Banda na Henock Inonga 27 kutoka DC Motema Pembe ya DR Congo.
Wengine ni Papa Ousmane Sakho 24 aliyetokea klabu ya Teungueth ya nchini kwao Senegal na Saido Kanoute 23 kiungo mshambuliaji kutoka nchini Mali.
Ingizo jipya linafanya jumla ya wachezaji wa kigeni wa Simba kuwa 14 na wastani wa umri wao ni miaka 27.
Huu ni upungufu wa karibu miaka mitatu na wale wa msimu uliopita unaoashiria timu hiyo imedhamiria kuwa na vijana watakaodumu muda mrefu kwenye timu.
WANACHOSEMA WADAU
Beki wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa anasema usajili uliofanywa na vingozi wa klabu hiyo ni ule wa tija kwani waliokuwa nao ndani ya misimu minne umri wao umeenda, hivyo wanapaswa kuchanganywa na damu changa.
“Tayari Simba wametengeneza soko la wachezaji, kitendo cha kuwasajili kina Peter Banda kitaendelea kuwanufaisha kwa sababu ni wachezaji wazuri,” anasema Pawasa anayeinoa timu ya taifa ya soka la ufukweni.
Mchezaji mwingine wa zamani wa timu hiyo, Ulimboka Mwakingwe anasema timu hiyo kusajili vijana inatoa mwelekeo wa mwendelezo wa maendeleo ya muda mrefu kikosini, hivyo kuwa na manufaa zaidi sasa na siku zijazo.