Prime
Simba v Berkane ngome mpya, historia mpya ugumu uko hapa!

Muktasari:
- Mchezo huo utakaochezeshwa na mwamuzi wa kati Dahane Beida kutoka Mauritania, utakuwa wa kihistoria kwa pande zote mbili, Simba na RS Berkane, lakini pia Zanzibar kwa ujumla.
NI Jumapili ya kihistoria Mei 25, 2025. Macho na masikio ya Afrika yapo Zanzibar kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, ambako kutapigwa fainali ya marudiano ya Kombe la Shirikisho Afrika kati ya Simba na RS Berkane.
Mchezo huo utakaochezeshwa na mwamuzi wa kati Dahane Beida kutoka Mauritania, utakuwa wa kihistoria kwa pande zote mbili, Simba na RS Berkane, lakini pia Zanzibar kwa ujumla.
Simba inataka kubeba ubingwa wa michuano ya CAF na kuweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kutoka Tanzania kufanya hivyo.
Kwa Berkane, inahitaji kulibeba kwa mara ya tatu baada ya kufanya hivyo 2019-20 na 2021-22, huku msimu uliopita 2023-24 ikipoteza fainali dhidi ya Zamalek kwa bao la ugenini ambapo nyumbani ilishinda 2-1, ilhali ugenini ikifungwa 1-0.
Upande mwingine, hii ni kwa mara ya kwanza katika historia ya michuano hii, fainali inachezwa katika ardhi ya Zanzibar na kwa mara nyingine tena, Simba SC inavuta pumzi yake ya mwisho katika mbio za kulisaka taji la CAF.
Baada ya kufungwa mabao 2-0 ugenini katika mechi ya kwanza iliyofanyika Morocco wikiendi iliyopita, Jumapili hii Simba inalazimika kushinda kwa tofauti ya mabao matatu iwapo inataka kutwaa taji hili kwa mara ya kwanza.
Hata hivyo, kibarua hicho si kigeni kwa Simba kuamka kutoka kwenye maumivu na kujibu kwa kishindo, ilishawahi kutokea msimu huu hatua ya robo fainali ilipokuwa nyuma dhidi ya Al Masry ya Misri na kupindua kipigo cha mabao 2-0 na kusonga nusu fainali kwa ushindi wa penalti 4-1 nyumbani. Hiyo ni baada ya kushinda 2-0 ndani ya dakika 90 na kufanya matokeo ya jumla kuwa 2-2.
Katika hali ya hewa ya joto inayotabiriwa hadi jioni, Simba si tu inacheza dhidi ya Berkane inapambana na historia, na pia inapigania hadhi ya taifa.
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, katika maandalizi kuelekea mchezo huo, amekazania maeneo matatu akiamini yanaweza kufanya wabebe ubingwa. Fadlu ameweka mkazo mkubwa kwenye mazoezi ya kushambulia kwa kasi na upigaji wa penalti, bila ya kusahau kuimarisha eneo la ulinzi. Mazoezi hayo yamefanyika kwa siku tatu mfululizo kambini Zanzibar.
Katika hilo, kocha huyo amekuwa akiwasuka vijana wake kwa mazoezi ya mashambulizi ya kushitukiza, akitumia mifumo mbalimbali kama 4-3-3 na 3-4-2-1 ili kuziba kila mianya ya RS Berkane. Lengo kuu ni kuwashambulia Waarabu kwa kasi mara tu mpira unapotoka kwenye eneo lao la ulinzi.
Wachezaji kama Ellie Mpanzu, Leonel Ateba, Steve Mukwala, Joshua Mutale, Kibu Denis na Jean Charles Ahoua, wamepewa majukumu ya kushambulia kwa mtindo wa ‘pasi chache mpira uwe golini’.
Mazoezi hayo yamejikita kwenye kuvuka haraka nusu ya wapinzani na kutengeneza nafasi za haraka kabla ya Berkane kujipanga.
Kwa kutambua kwamba mechi hii inaweza kuamuliwa kwa penalti kama Simba itapindua matokeo, timu hiyo pia imeweka mkazo kwenye upigaji wa mikwaju hiyo.
Tunaingia uwanjani si kama waathirika wa mechi ya kwanza, bali kama wapiganaji wanaotafuta haki yao,†alisema Fadlu na kuongeza.
“Tunacheza kwa ajili ya historia, si kwa ajili yetu tu bali kwa ajili ya mamilioni ya Watanzania. Tutaanza kwa kasi, kwa nidhamu, na kwa moyo wa Simba halisi,” aliongeza.
Katika mtihani huo mzito ilionao Simba, kuna mambo ambayo yanaweza kuchangia kuibeba timu hiyo na kuibadilisha historia ya soka la Tanzania.
NGOME MPYA, HISTORIA MPYA
Simba imepata nafasi ya kucheza mechi kubwa ya fainali nyumbani lakini si Dar es Salaam, bali visiwani Zanzibar. Uwanja huu una uwezo wa kuingiza mashabiki zaidi ya 15,000 tofauti na Benjamin Mkapa wanaofika 60,000.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), pamoja na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), wamehakikisha maandalizi yamekamilika, teknolojia ya VAR iko tayari, miundombinu iko imara, na usalama umeimarishwa.
Kupata fursa ya kuanzia ugenini kisha kumalizia nyumbani ni nzuri kwa Simba kama itaweka vizuri mikakati yake kufuatia rekodi bora iliyonayo msimu huu katika mashindano hayo.
Kuanzia hatua ya pili hadi kuingia fainali, Simba imecheza mechi sita nyumbani na kushinda zote. Kati ya hizo, tano imecheza Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar, sehemu ambayo timu hiyo imeibatiza jina la ‘Kwa Mkapa Hatoki Mtu’. Moja ikicheza New Amaan Complex, ikiwa robo fainali dhidi ya Stellenbosch ya Afrika Kusini na Simba kushinda 1-0.
Simba inaisaka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kutoka Tanzania kubeba ubingwa wa CAF, wingi wa mashabiki wake watakaokwenda kuisapoti, inaweza kuongeza chachu ya kusaka ushindi.
MBINU NA ARI YA FADLU
Kocha Fadlu Davids ameibadilisha Simba kutoka timu ambayo ilikuwa ikiishia hatua ya robo fainali ya kimataifa hadi kufika fainali kwa kujenga kkosi chenye maelewano, nidhamu ya kimbinu, na uwezo wa kubadilika katika kushambulia na kulinda.
Katika mechi dhidi ya Berkane ugenini, licha ya kufungwa mabao mawili ya mapema, lakini Simba ilicheza kwa nidhamu ambayo iliirudisha mchezoni.
Fadlu ana nafasi ya kupanga kikosi bora kwa kila mchezaji kuwa na jukumu lake, kila mpira ukiwa na maana, na kila nafasi ikitumika kwa makini.
Kocha huyo raia wa Afrika Kusini, amekuwa akiwahimiza kucheza kana kwamba ni mechi ya mwisho kwenye maisha yao.
Fadlu amewahi kuwa kwenye benchi la ufundi la Orlando Pirates ya Afrika Kusini na Raja Casablanca ya Moroco akishiriki michuano ya CAF kama kocha msaidizi. Sasa ni kocha mkuu.
KIKOSI CHA KUFA AU KUPONA
Eneo la mwisho la ushambuliaji, Fadlu anawashambuliaji wawili wa kati ambao kila mmoja ameonyesha makali yake msimu huu, Steve Mukwala na Leonel Ateba kiasi cha kumpasua kichwa.
Ateba ni mshambuliaji mwenye uwezo wa kupenya kati ya mabeki wa aina yoyote, mwenye nguvu na nafasi nzuri ya kufunga kwa kichwa au mguu wowote. Mukwala ni mwepesi na mwenye kasi hivyo ni ngumu kutabirika.
Eneo la viungo washambuliaji ndio injini ya Simba ikiwa na Mpanzu, Ahoua na Kibu, utatu huo umeifanya timu hiyo kuwa hatari hasa inapokuwa nusu ya uwanja wa wapinzani wao, wanakasi na maarifa.
Nyuma ya utatu huo kuna viungo wengine wawili ambao kazi yao ni kuhakikisha usalama lakini pia kunganisha timu, Fabrice Ngoma na Yusuph Kagoma.
Kwa upande wa ukuta, Simba inajivunia kuwa na mabeki wa kati watatu ambao wameonyesha kiwango kizuri msimu huu hivyo kazi kwake Fadlu kufanya chaguo nani aanze nani asubiri benchi.
Kuna Abdulrazak Hamza, Chamoe Karaboue na Che Fondoh Malone, kwa mabeki wa pembeni ni Shomary Kapombe na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ hawa ni mabeki wa kisasa, wenye uwezo wa kusimama imara na kupandisha mashambulizi kwa kasi.
Kikosi hiki, kinachochanganya uzoefu na vipaji vipya, kina kila sababu ya kuiumiza Berkane ikiwa kitacheza kwa umoja, maelewano na nidhamu. Simba haihitaji kucheza kwa uwezo wa mchezaji mmoja mmoja bali icheze kama timu.