Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Klabu hazijatumia vizuri Ligi Kuu U-20

ZENGWE Pict
ZENGWE Pict

Muktasari:

  • Timu zote, kama Atletico Madrid, Barcelona, Girona, Sevilla na Real Madrid hushiriki katika ligi hiyo inayohusisha watoto wenye umri wa chini ya miaka 12. Hizi ni shule za mchezo wa mpira wa miguu, au kwa jina lililozoeleka mitaani, Soccer Academy.

KUNA raha kila mwaka kuangalia watoto wa Hispania wakipambana katika mashindano ya umri wao ya timu zinazomilikiwa na klabu za Ligi Kuu ya Hispania, maarufu kwa jina la La Liga.

Timu zote, kama Atletico Madrid, Barcelona, Girona, Sevilla na Real Madrid hushiriki katika ligi hiyo inayohusisha watoto wenye umri wa chini ya miaka 12. Hizi ni shule za mchezo wa mpira wa miguu, au kwa jina lililozoeleka mitaani, Soccer Academy.

Mashindano hayo ni ya kitaifa na yanajulikana kama LaLiga Futures FC, ambayo yanaendeshwa kwa ushirikiano wa La Liga, yaani Ligi Kuu ya Hispania na Mfuko wa Sevilla Jose Ramon de la Morena. Yalianza kama mashindano ya kombaini za mikoa yakifanyika wakati wa likizo ya katikati ya mwaka lakini sasa yamekuwa makubwa yakishirikisha timu za klabu za La Liga na wakati wa likizo ya mwishoni mwa mwaka hufanyika ya kimataifa yakishirikisha timu sita za nje ya Hispania kama Inter, Chelsea na La Palmas.

Raha ya mashindano hayo ni kuona jinsi timu za watoto zinavyotumia falsafa ya klabu zao uwanjani.

ZENG 01

Pale Barcelona inapocheza, vitu vingi vinavyofanywa na timu ya wakubwa, huonekana pia kwa watoto ingawa si kwa ufanisi unaolingana. Hali kadhalika, Atletico de Madrid inapocheza, unaona ile ari ya kufa au kupona na ile ya kutosalimu amri inayoonyeshwa na timu ya kwanza.

Timu hizi zimekuwa ndio chachu ya mafanikio ya klabu za Hispania na timu yao ya taifa, ambayo katika fainali za mwaka 2024 za Mataifa ya Ulaya, wachezaji 25 kati ya 26 wa Hispania walizalishwa na timu 11 za La Liga Futures.

Hii ni tofauti kabisa na hali inavyoonekana katika mashindano ya hivi karibuni ya vijana wa umri wa chini ya miaka 20 yaliyoshirikisha timu za vijana za klabu za Ligi Kuu Bara.

Kwa miaka ya hivi karibuni, Yanga imebadili ule mchezo wake wa mambo-yote-mbele, kwa kucheza mpira wa pasi zaidi usio na papara, mchezo ambao ni maarufu kwa klabu ya Simba ambayo miaka yote imekuwa ikitumia umiliki mkubwa wa mpira na kuwa na washambulizi wasio na huruma na nyavu.

ZENG 02

Yanga imekuwa na utamaduni wa kuwa na ngome imara ambayo wakati fulani ilipachikwa jina la Ukuta wa Berlin, wakati Simba imekuwa na utamaduni wa kuwa na makipa bora, ambao mara kadhaa wamekuwa tegemeo la timu ya taifa.

Mtibwa Sugar imekuwa ikijulikana kwa mchezo wa pasi na kumiliki mpira muda mwingi, huku wasaka vipaji wakiwa na uwezo mkubwa wa kung’amua wachezaji stadi wenye uwezo mkubwa wa binafsi. Hali kama hiyo ipo Azam FC, ambayo ina jicho zuri la wachezaji stadi na mchezo wake pia ni wa umiliki wa mpira.

Lakini ukiangalia mashindano ya Ligi Kuu ya Vijana ya U-20 huoni sifa za timu zao za kwanza, ingawa kwa hali fulani, Azam imeonyesha kulinda utamaduni wake wa kung’amua vipaji ingawa havionekani kama ni hazina ya baadaye kwa klabu hiyo tajiri.

Timu nyingi ni kama zimeundwa na vijana waliokusanywa, kuwekwa kambini kwa muda mfupi na baadaye kuambiwa nendeni mkacheze. Huoni ustadi wa wachezaji wenye umri huo ambao kwa sasa wanapewa nafasi angalau ya dakika 10 katika vikosi vyao vya kwanza na wala huoni kama wapo watakaofikiriwa.

ZENG 03

Ni kama wameitwa “njooni mcheze, atakayebahatika ameula”. Ni wachezaji ambao wametafutwa bila ya kuzingatia falsafa za klabu kama kweli zipo, au miongozo ya wachezaji wanaotakiwa na klabu hizo ili wawe akiba ya baadaye.

Huku ni kutumia vibaya fursa zinazotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Kuu. Huku ni kutojali matumizi ya fedha ambazo klabu inazipata kutoka vyanzo mbalimbali. Huku ni kutokuwa na uchungu katika matumizi ya fedha na huku ni kutokuwa na mipango ya muda mrefu.

Na mipango ya muda mrefu si ile inayosemwa kila mara kuwa ni kujenga kikosi cha baadaye, bali kujenga utamaduni wa klabu na pia kuwauza muda wao unapofika au kuwapeleka kwa mkopo sehemu nyingine kwa ajili ya kupata soka la kikosi cha kwanza na baadaye kuwarudisha wakiwa wameshakomaa.

ZENG 04

Wale wanaoonekana wazuri na waliokolea utamaduni wa klabu huanza kutambulishwa taratibu katika mechi za vikombe au za Ligi Kuu kwa kupewa dakika chache ili wazoee na msimu unapoisha wanakuwa tayari kwa kiasi fulani kubeba majukumu ya klabu pale wanapohitajika. Kama Ethan Nwaneri alivyofanya wakati Bukayo Saka alipokuwa majeruhi ndani yaArsenal.

Kama mashindano hayo ya U-20 Tanzania yangekuwa yanafanyika leo hii kwa kuhusisha klabu za Ligi Kuu ya England, basi ungewaona kina Myles Anthony Lewis-Skelly, ambaye ndio kwanza ana miaka 18, Jeremy Monga wa Leicester (18) Chido Obi wa Manchester United (17) na Ethan Nwaneri wa Arsenal mwenye miaka 18.

Hawa ni wachezaji wanaoelewa falsafa za mchezo wa klabu zao na wamefikia kuaminiwa na makocha wa vikosi vya kwanza vya klabu zao kwa kuwa wamekuwepo klabuni kwa muda mrefu, wengine tangu utoto wao.

ZENG 05

Klabu zetu hazina budi sasa kuanza kujenga utamaduni huu wa kuwa na klabu za watoto, vijana wadogo na vijana. Mpango huu huandaa kundi la wachezaji walio na nidhamu fulani iliyojengwa ndani ya klabu na baadaye kuwa na ndoto za kucheza vikosi vya kwanza, ndoto ambazo hutimizwa kwa kufanya juhudi kubwa.

Mashindano hayo ya U-20 ni ya muda mrefu, lakini hakuna viongozi wa klabu wanayoyaangalia kwa jicho la maendeleo. Wengi wanaonekana kuyaangalia kama ni ya kutimiza wajibu ili ‘shetani’€  apite. Ni Azam pekee inayoona kuna umuhimu wa mashindano hayo katika kujenga timu bora.

Hali hiyo imesababisha timu hizo za U-20 kutokuwa na vijana ambao wanadumu katika klabu hizo kwa angalau misimu miwili. Maana yake ni kwamba klabu hizo husajili wachezaji wote wenye umri wa miaka 20 ambao mwaka ukipita tu, wanakuwa wamepoteza sifa za umri wa kushiriki.

Hiyo haiwezi kuwa kweli. Jukwaa ambalo TFF inalitoa kwa klabu zetu ni muhimu sana likatumiwa vizuri kwa maendeleo ya soka letu. Haiwezekani Ligi Namba Nne kwa ubora Afrika ikazidiwa na Afrika Kusini au Namibia ambazo zina mfumo mzuri wa mashindano ya vijana.

Macho ya viongozi yasikodolee vikosi vya kwanza kama ngazi za kujijenga kisiasa, bali waangalie nafasi walizonazo katika kuchangia maendeleo ya mpira wa miguu ya taifa kwa ujumla na wazitumie kwa kadri inavyotakiwa.