Simba yalazimishwa sare Amaan Complex, RS Berkane bingwa CAFCC

Muktasari:
- Refa huyo anayekumbukwa na mashabiki wa Yanga kwa kulikataa bao lililoonekana halali la Stephane Aziz Ki katika mechi ya marudiano ya robo fainali ya msimu uliopita dhidi ya Mamelodi Sundowns, kuna maamuzi aliyokuwa akiyatoa yaliyoonekana kama yanailalia zaidi Simba.
SIMBA imepoteza kwa mara nyingine fainali ya michuano ya CAF, ikiwa nyumbani baada ya kutoka sare ya 1-1 na RS Berkane ya Morocco na matokeo ya jumla kuwa 3-1, lakini mashabiki wa klabu hiyo wakionyesha kuridhika na soka lililopigwa, huku wakimnyooshea kidole refa Dehane Beida kutoka Mauritania.
Refa huyo anayekumbukwa na mashabiki wa Yanga kwa kulikataa bao lililoonekana halali la Stephane Aziz Ki katika mechi ya marudiano ya robo fainali ya msimu uliopita dhidi ya Mamelodi Sundowns, kuna maamuzi aliyokuwa akiyatoa yaliyoonekana kama yanailalia zaidi Simba.
Tukio la kadi nyekundu aliyomuonyesha kiungo mkabaji, Yusuf Kagoma dakika chache baada ya kipindi cha pili kuanza na kuidhohofisha Simba ilikuwa mbele kwa bao moja, kabla ya bao la kipindi hicho la Steven Mukwala kukataliwa na VAR kwa vile mfungaji alikuwa ameotea.
Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan, mjini Unguja visiwani Zanzibar, Simba iliwabana Berkane iliyoshinda ikiwa kwao kwa mabao 2-0 Jumamosi ya wiki iliyopita, Simba itajilaumu pia kwa kupoteza nafasi nyingi za wzi ambazo zingeweza kuwapa historia nyingine katika michuano ya CAF.
Beki Shomari Kapombe katika kipindi cha kwanza na lile la Mukwala pamoja na Mpanzu kipindi cha pili kiliikosesha Simba ushindi, licha ya Joshua Mutale kufunga bao mapema dakika ya 17 akiunganisha krosi ya chnini chini ya Ellie Mpanzu na kukoswa na Mukwala.

Hii ni mara ya pili Simba kupoteza nafasi ya kubeba ubingwa ikiwa nyumbani, baada ya ile ya mwaka 1993 ilipocheza fainali ya Kombe la CAF na kupoteza nyumbani mbele ya Stella Abidjan ya Ivory Coast iliyoshinda 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru) baada ya suluhu ya ugenini.
Michuano hiyo ya Kombe la CAF ndio iliyokuja kuunganishwa na Kombe la Washindi Afrika na kuwa Kombe la Shirikisho Afrika kuanzia mwaka 2004
Simba inakuwa timu ya pili ya nchini kucheza fainali ya michuano hiyo ya sasa baada ya Yanga kufanya hivyo msimu wa 2022-2023, ikilikosa taji kwa kanuni ya faida ya bao la ugenini kutokana na matokeo ya jumla ya sare ya 2-2, baada ya Jangwani kupoteza nyumbani 2-1 na kushinda ugenini 1-0.
MECHI ILIVYOKUWA
Licha ya Simba kuanza mechi hiyo kwa tahadhari kubwa ikipambana kupindua meza baada ya kupoteza mabao 2-0, Morocco, ila ilikosa nidhamu baada ya kufanya madhambi mengi zaidi tofauti na ilivyokuwa kwa wapinzani wao, RS Berkane.
Katika dakika 45 za kwanza, Simba ilitawala mechi kwa asilimia 63 tofauti na wapinzani wao RS Berkane iliyokuwa na 37, huku wenyeji wakipiga shuti moja lililolenga lango ambalo liliza bao la dakika ya 17 la Joshua Mutale akipokea pasi ya Mpanzu.

Bao hilo liliamsha morali ya Simba kuendelea kulisakama lango la Berkane, huku Moussa Camara akionekana shujaa dakika 45 za kwanza, baada ya kuokoa michomo mitatu, ukilinganisha na ilivyokuwa kwa kipa wa RS Berkane, Munir Mohamed El Kajoui.
Kipindi cha pili, Simba iliendelea kutawala mechi ikiwa na asilimia 59 kwa 41 za wapinzani wao, ingawa haikutengeza mashambulizi mengi ya hatari, kutokana na kucheza kwa tahadhari ya kuzuia na wakati huohuo ikishambulia kusaka mabao.
KADI NYEKUNDU ZATAWALA
Wakati Simba ikipambana kutafuta bao la pili litakalowapa matumaini ya kuwania taji hilo kubwa Barani Afrika, ilichukua dakika 50 ya kipindi cha pili kucheza pungufu baada ya kiungo nyota wa kikosi hicho, Yusuf Kagoma kuonyeshwa kadi nyekundu.
Kagoma alionyeshwa kadi hiyo ikiwa ni njano ya pili iliyozaa nyekundu baada ya kumfanyia madhambi, kiungo wa RS Berkane, Imad Riahi na kusababisha kikosi hicho kucheza pungufu na kukosa nguvu ya kuongeza mashambulizi kwa wapinzani wao.
Mbali na kadi hiyo, pia kocha msaidizi wa Simba, Darian Wilken alionyeshwa baada ya mzozo akiwa katika benchi la ufundi, huku Fadlu Davids akionyeshwa ya njano kutokana na kutokubaliana na maamuzi yaliyokuwa yanaendelea kwa refa, Dahane Beida raia wa Mauritania.

BAO LA MUKWALA
Licha ya Steven Mukwala kufunga bao dakika ya 73 na kufufua matumaini ya kikosi hicho ya kupata la pili, ila ilijikuta ikiangukia pua, baada ya picha ya marudio kuonyesha mshambuliaji huyo aliotea wazi wakati anauzamisha mpira huo wavuni.
Kitendo cha bao hilo kukataliwa kutokana na kuonekana wazi kwa mshambuliaji huyo kuzidi, kilizidi kushusha morali ya timu hiyo iliyokuwa inasaka mabao kuanzia mawili, ili kutengeneza balansi kutokana na matokeo ya mwanzo yalivyokuwa.
NDOTO ZILIFIA HAPA
Bao la kuchomoa la Soumaila Sidibe, lilizamisha kabisa matumaini ya kikosi hicho kutwaa ubingwa baada ya kufunga dakika ya 90, ikiwa ni muda wa nyongeza na kupoteza fainali ya pili nyumbani baada ya ile ya michuano ya CAF mwaka 1993.
Nyota huyo aliyeingia dakika ya 78, akichukua nafasi ya Mamadou Camara, bao lake la kuchomoa lilikuwa mlima kwa Simba kwani ingewalazimu kushinda mabao 4-1, hali iliyokuwa changamoto kwao kutokana na upungufu wa wachezaji waliokuwa nao.
MUTALE KAJIPATA
Kiwango bora kilichoonyeshwa na kiungo mshambuliaji wa Simba, Joshua Mutale kinaonyesha jinsi nyota huyo anavyojitafuta taratibu baada ya kutokuwa na msimu mzuri tangu ajiunge na kikosi hicho akitokea Power Dynamos ya kwao Zambia.

Kiwango alichokionyesha katika mechi ya mkondo wa kwanza ya fainali akitokea benchi kule Morocco, kimemfanya Kocha Mkuu, Fadlu Davids kumuanzisha kikosi cha kwanza, huku akiendeleza pale alipoishia na kutoa matumaini ya kuendelea kuaminiwa.
KAMA 1993
Matokeo yameifanya Simba kurudia tukio la mwaka 1993 ilipopoteza fainali ya Kombe la CAF dhidi ya Stella Abdijan ya Ivory Coast iliyoibuka mabingwa kwa ushindi wa 2-0 na taji kukabidhiwa na Rais wa Awamu ya Pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, baba wa Rais wa sasa wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi aliyelikabidhi taji la Shirikisho kwa nahodha wa Berkane, Issoufou Dayo.
Tofauti pekee ni kwamba Simba imetoka sare ya 1-1 ikiwa nyumbani, lakini kipigo cha 2-0 ugenini kiliwatibulia, wakati fainali ya 1993 ilitoka suluhu ugenini na kupoteza nyumbani 2-0.
YAVUNA MABILIONI
Licha ya kushindwa kutwaa taji hilo ili kuweka rekodi ya kuwa klabu ya kwanza kwa Tanzania, lakini Smba imevuna mabilioni ya fedha kutokana na kumaliza ya pili katika michuano hiyo ya CAF kwani imevuna Dola 1 Milioni (karibu Sh 2.7 bilioni), wakati Berkane kwa kubeba ubingwa ikiwa ni mara ya tatu kwao ikilingana na CS Sfaxien, imekomba dola 2 Milioni (karibu Sh 5.4 Bilioni).
Hata hivyo, mastaa wa Simba wameikosa Sh 1 bilioni moja waliyoahidiwa kama wangebeba ubingwa huo, mbali na Dola 100,000 (zaidi ya 269 milioni) walizoahidiwa na Rais Mwinyi kama wangetwaa taji.
SIMBA: Camara, Kapombe, Tshabalala/Nouma, Chamou, Che Malone/Ateba, Kagoma, Mutale/Kibu, Ngoma, Mukwala, Ahoua na Mpanzu
RS BERKANE: Munis, El Moussaoui, Assal, Tahif, Dayo, Camara/Sidibe, Khairi, Mehri/Bassene, Lamlaoui/Zghoudi, Lebhiri na Riahi/El Mourabit