Prime
Aziz Ki amemaliza fungate la mpira, sasa anaingia kazini

Muktasari:
- Kuna siri huwa zinafichwa vizuri na ghafla kinachotokea huwa kinamshangaza kila mtu. Hili la Aziz kwenda Casablanca halijawahi kuwa siri sana. Mara mwisho siri kufichwa vibaya ni wikiendi ile iliyopita wakati Aziz KI alipokuwa nahodha pale Mkwakwani wakati Yanga wakicheza pambano la nusu fainali yetu dhidi ya JKT Tanzania.
WAZUNGU huwa wanasema 'The wrost kept secret'. Huku kwa waswahili huwa tunasema 'siri iliyofichwa vibaya'. Katika mpira kuna siri ambazo zinafichwa vibaya. Labda ni kama hii ya Stephane Aziz Ki kwenda Wydad Casablanca ya Morocco. Yanga hawajatangaza, lakini kila mtu anafahamu kwamba Aziz KI anakwenda Morocco.
Kuna siri huwa zinafichwa vizuri na ghafla kinachotokea huwa kinamshangaza kila mtu. Hili la Aziz kwenda Casablanca halijawahi kuwa siri sana. Mara mwisho siri kufichwa vibaya ni wikiendi ile iliyopita wakati Aziz KI alipokuwa nahodha pale Mkwakwani wakati Yanga wakicheza pambano la nusu fainali yetu dhidi ya JKT Tanzania.
Kwamba alipewa unahodha kwa ajili ya kuagwa. Dickson Job ambaye ni nahodha msaidizi wakati Bakari Mwamnyeto anapokosekana, alikuwepo uwanjani, lakini unahodha ukaenda kwa Aziz Ki. Ikawa wazi kwamba ilitokana na Aziz KI kuaga rasmi klabuni kwa sababu Yanga ilikuwa imekubali dau la Wydad.
Na juzi ni rasmi kwamba Aziz Ki amepewa 'Thank You' katika klabu yake ya Yanga. Ameuzwa rasmi kwenda Morocco. Aliondoka nchini usiku kama alivyowasili na kutangazwa misimu mitatu iliyopita. Binafsi ameniachia hisia mkanganyiko kuhusu kipaji chake na uwezo wake uwanjani.

Kitu cha kwanza kabisa ni kwamba ASEC Mimosas walituletea kijana mwembamba, mwenye kasi na akili ya mpira. Lakini Yanga wanawapelekea Wydad, Aziz KI kibonge kidogo na mwenye mke kutoka Tanzania. Kumekuwa na mabadiliko mengi makubwa kwa mtu yule yule ambaye Yanga walimchukua kutoka Abidjan na sasa wanamuuza kwenda Casablanca.
Ninachoona ni kwamba Aziz KI ana kazi kubwa ya kushinda mioyo ya mashabiki wa timu yake mpya, Wydad Casablanca. Vinginevyo tunaweza kuwa na Aziz KI hapa Temeke ndani ya miezi 12 ijayo. Inaweza kuwa hata kwa uhamisho wa mkopo. Anapaswa kupambana licha ya kupata uhamisho huu. Tanzania ilimpa fungate la kazi yake.
Aziz KI, akiwa na kipaji kama alivyo, sikumuona katika ubora wake ule aliokuwa nao na ASEC. Aziz alikuwa na matukio mazuri uwanjani. Kupiga mashuti makali langoni, kupiga frii-kiki nzuri, kupiga penalti, kupiga kona na kupiga pasi za mwisho. Vinginevyo hakujishughulisha sana na mpira hasa wakati timu yake ikiwa haina mpira. Katika mpira wa kisasa wachezaji wote wanapaswa kukaba kwa umakini uwanjani.
Aziz alikuwa na mambo mawili. Hakuwa na kasi sana uwanjani, lakini zipo nyakati nyingi ambazo alikuwa anapoteza mipira kiurahisi tu kwa sababu alikuwa anataka kukaa na mpira bila ya sababu. Haya yatakumbukwa zaidi hasa katika msimu wake wa kwanza alipowasili nchini ambapo nusura Yanga iachane naye.

Bahati nzuri kwa Aziz KI alikuja nchini na jina kubwa huku watu wakiwa wanajua kile alichokifanya ASEC Mimosas, hivyo kwa namna moja walimvumilia na kumsubiri arudi katika ubora wake. Angekuwa mchezaji wa kawaida wa Kitanzania sidhani kama angevumiliwa kwa kile alichokionyesha katika msimu wake wa kwanza Jangwani.
Majuzi nilikuwa nawatazama RS Berkane wakicheza dhidi ya Simba. Wana kasi ya ajabu na wanakuwa bora wakiwa na mpira na wasipokuwa na mpira. Hii ndio ligi ambayo Aziz anakwenda kule Morocco. Ili asirudi nchini kwa uhamisho wa mkopo basi Aziz anapaswa kuwa bora mara mbili ya alivyokuwa nchini na aongeze wepesi katika mwili wake.
Hadi leo huwa tunaulizana ni kwa namna gani Clatous Chama alichemsha katika Ligi Kuu ya Morocco. Wengi tunapata hisia kwamba huenda hakuendana na kasi ya Waarabu. Hapo ndipo tunapoweza kumtafakari kama Aziz anaweza kuwa tofauti na kufanya kile ambacho Chama alishindwa. Binafsi sioni sana. Anahitaji kubadilika zaidi ili aendane na kasi ya Waarabu.

Ni wazi kwamba Aziz amemaliza fungate lake la mpira. Kucheza mpira wa Tanzania wakati mwingine ni rahisi hasa unapochezea Yanga. Muda wote timu inamiliki mpira na inashambulia. Sidhani kama maisha yatakuwa rahisi katika Ligi Kuu ya Morocco ambako kuna ushindani mwingi. Karibu kila timu ni ngumu ina kasi.
Ukiachana na mechi za kimataifa, mechi nyingine zilikuwa rahisi kwa Aziz kwa namna ligi yetu ilivyo. Na sasa anakwenda kupambana na kina FAR Rabat, Raja, Berkane, FUS Rabat na wengineo wengi. Tusidanganye Ligi ya Morocco ni bora kwa mbali kulinganisha na ligi yetu. Aziz anapaswa kujipanga kwa sababu kazi ngumu inaanza sasa katika maisha yake ya mpira.
Nini nitakikumbuka kutoka kwake? Jambo la kwanza kabisa ni ujio wake. Hakuna mchezaji aliyetua kwa mbwembwe nchini kama Aziz Ki. Ilionekana kama vile malaika anatua kuja kuipeleka Yanga katika matawi ya juu zaidi. Hata watani wao hawakuamini kama Aziz anakuja kucheza Yanga. Kwa ule mpira alioonyesha akiwa na ASEC ilikuwa ndoto ya kila timu kumnasa Aziz.

Kama sio Injinia Hersi Said kupambana kuinasa saini yake kupitia kwa familia yake na watu wa karibu basi jana Aziz angekuwa anacheza pambano la fainali la michuano ya Shirikisho akiwa na jezi ya Simba dhidi ya Berkane pale Unguja. Huu ni ukweli ingawa Simba wenyewe wanaweza kukana hilo kwa sababu halikutimia.
Bao ninalolikumbuka? Nadhani ni bao dhidi ya Club Africain ya Tunisia ugenini. Bao ambao liliwaondoa Watunisia katika michuano ya Shirikisho ndani ya ardhi yao wenyewe. Walikwenda moja kwa moja hadi katika fainali za michuano hiyo. Pambano la awali timu hizo zilitoka suluhu ya bila ya kufungana pale Temeke Dar es Salaam.
Nini kinafuata? Yanga wamepata fedha kwa mauzo ya Aziz. Nilisikia dili hili kwa muda mrefu. Lakini pengo la Aziz litatafakariwa kama Hersi Said atakosea kuchukua mchezaji mzuri katika nafasi yake. Katika mpira wa kisasa wachezaji ni bidhaa kama zilivyo bidhaa nyingine klabuni. Hakuna tatizo lolote Aziz KI kuuzwa. Hata hivyo, kama ameacha pengo au hajaacha hilo tutalijua pindi Injinia atakapokuwa amesajili mchezaji mwingine.

Siku za hivi karibuni Hersi amekuwa akikosea na kupatia katika masuala ya usajili. Ni kitu cha kawaida katika soka. Hatukuona sana pengo la Fei Toto kwa sababu alipishana mlangoni na Pacome Zouzoua ambaye naye ni fundi wa mpira kama ilivyo kwa Fei. Ndio maana Yanga waliendelea kutamba. Ndio maana Yanga wameendelea kuwa mabingwa. Na sasa tuone nani atakwenda kuziba pengo la Fei pale Jangwani.
Mzigo ni kwa Aziz KI na maisha yake. Anaweza kuingia katika historia kama miongoni mwa wachezaji bora ambao ligi yetu imewahi kuwapeleka nje kama ilivyo kwa Nonda Shabani 'Papii', Mbwana Samatta, Simon Msuva na Fiston Mayele? Jibu analo mwenyewe kama akiongeza bidii katika aina yake ya mchezo. Waarabu sio watu wazuri sana.
Waarabu hawaoni shida kukununua kwa bei kubwa kisha wakakulipa pesa ndefu, lakini wakaamua kuachana na wewe wakiona unawazingua. Ni kitu cha kawaida tu kwao kuachana na mchezaji kabla hata hawajamalizia awamu za malipo kwa timu iliyowauzia mchezaji. Ndivyo ilivyokuwa. Tazama pia kwa Jose Luis Miquissone. Hawana muda mwingi wa kusubiri. Wanashindana kila siku.