Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kocha Simba afichua dili la Camara wa Berkane

CAMARA Pict

Muktasari:

  • Katika mechi ya awali ugenini ambayo Simba ililala 2-0, kuna kiungo mmoja fundi wa RS Berkane aliwavuruga Wekundu wa Msimbazi na kufunga moja ya mabao hayo, lakini usichokijua ni kwamba kiungo huyo kama isingekuwa figisu angekuwa ni mali ya Msimbazi kitambo kirefu tu.

HUENDA hii isiwe taarifa nzuri kwa Wanasimba ambao jana waliishuhudia timu yao ikivaana na RS Berkane ya Morocco katika pambano la marudiano ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika lililochezwa kwenye Uwanja wa New Amaan, mjini Unguja Zanzibar.

Katika mechi ya awali ugenini ambayo Simba ililala 2-0, kuna kiungo mmoja fundi wa RS Berkane aliwavuruga Wekundu wa Msimbazi na kufunga moja ya mabao hayo, lakini usichokijua ni kwamba kiungo huyo kama isingekuwa figisu angekuwa ni mali ya Msimbazi kitambo kirefu tu.

Ndio. kocha wa zamani wa Simba, Abdelhak Benchikha amefichua kuwa, Mamadou Lamine Camara, alitakiwa kusajiliwa pale Msimbazi, lakini waliopewa kazi hiyo klabuni wakazembea na kuishia kuletwa kwa Babacar Sarr aliyeishia kucheza muda mfupi kabla ya kutemwa mwanzoni mwa msimu huu.

Camara, mmoja wa viungo warefu na wenye uwezo mkubwa wa kukaba, kusambaza mipira na kufunga, ndiye aliyeikatili Simba kule Berkane, kwa kufunga bao la pili, huku akiizimia safu ya kiungo ya Wekundu iliyokuwa na Yusuf Kagoma na Fabrice Ngoma.

Akizungumza na Mwanaspoti, Benchikha aliyekuwa kocha wa mwisho wa kigeni wa Simba kabla ya kuletwa kwa Fadlu Davids, alisema Simba ilipigwa kwa Camara, kwani ndiye mchezaji aliyekuwa akitakiwa aletwe msimu uliopita kwa vile alishapewa jina lake, lakini cha ajabu aliletwa Babacar Sarr.

Benchikha anayeinoa Modern Future ya Misri, alisema wakati anainoa Simba ilikuwa na uhitaji na kiungo mkabaji na mtu wa kwanza alikuwa Camara, lakini klabu hiyo ilichelewa kufanya uamuzi na mchezaji huyo kwenda Berkane, kisha Wekundu hao wakamleta Babacar Sarr aliyeshindwa kuwika.

“Wakati tunatafuta kiungo mkabaji kabla ya kusajiliwa kwa Babacar Sarr, nililetewa jina la Mamadou Lamine Camara, nilipoanza kufuatilia ubora wake nikapewa taarifa kwamba ameshauzwa Berkane. Kwa kweli Camara alikuwa chaguo la kwanza katika usajili wa wakati huo, ikabidi waende kumchukua Sarr, hao wote waliletwa na meneja wa Pape Ousmane Sakho,” alisema Benchikha na kuongeza;

“Kama Simba ingempata wakati ule ingekuwa imemaliza tatizo la kiungo mkabaji, japo haimaanishi waliopo kwa sasa ni wabaya ila angeongeza kitu, kwani Camara anajua sana mpira na anatekeleza majukumu yake kwa ufanisi uwanjani.”

Katika mechi ile Camara alicheza dakika 90 zote, huku akiwaachia kumbukumbu mbaya viungo wakabaji wa Simba, Fabrice Ngoma na Yusuf Kagoma sambamba na kipa, Moussa Camara ‘Spider’.

Kiungo huyo raia wa Senegali mwenye umri wa miaka 22, huenda angekuwa msaada kwa Simba, hasa msimu huu ambao wamesajili wachezaji wenye umri mdogo na uwezo mkubwa hasa kipindi hiki ikirudia kucheza fainali ya Afrika baada ya Kombe la CAF 1993.