Simba ilivyokiwasha Amaan Complex

Muktasari:
- Bao la mapema la dakika 16 la Joshua Mutale liliipa nguvu Simba jana mbele ya wageni, huku bao lililofungwa na Steven Mukwala katika dakika ya 73 lilikataliwa na VAR kabla ya mtokea benchini, Soumaila Sidibe kufunga bao jiooni na kuwakatili mashabiki waliojazana kwenye Uwanja wa New Amaan.
SIMBA licha ya kushindwa kubeba ubingwa wa kwanza wa Afrika baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 nyumbani na RS Berkane ya Morocco, imeendeleza rekodi ya kutopoteza mechi yoyote nyumbani msimu huu katika mechi za Kombe la Shirikisho Afrika.
Bao la mapema la dakika 16 la Joshua Mutale liliipa nguvu Simba jana mbele ya wageni, huku bao lililofungwa na Steven Mukwala katika dakika ya 73 lilikataliwa na VAR kabla ya mtokea benchini, Soumaila Sidibe kufunga bao jiooni na kuwakatili mashabiki waliojazana kwenye Uwanja wa New Amaan.
Hata hivyo, Simba iliwapa raha mashabiki kwa soka ililopiga na kama sio umakini mdogo wa nyota wa timu hiyo, huenda habari ingekuwa nyingine na hapa chini ni takwimu za kikiosi cha Wekundu walivyokiwasha wakipewa alama chini ya kumi.
Moussa Camara 7.5
Alifanya kazi nzuri kipindi cha kwanza, hesabu zake ziliuweka salama ukuta na timu yake akicheza krosi na mipira ya vichwa, alifanya kazi bora kuokoa shambulizi la kichwa kwenye mstari licha ya kuruhusu bao.

Shomari Kapombe 6.5
Pengine Simba ingepata mabao mawili mapema mwanzo wa kipindi cha kwanza kama kichwa chake kingejaa wavuni, alipandisha mashambulizi lakini krosi zake hazikuonekana.

Momammed Hussein 5
Alipunguziwa jukumu la kupandisha mashambulizi, hakuonekana sana kama kawaida yake na bado Berkane wakapita kwake.
Chamou Karaboue 6.5
Alionekana eneo la kutumia nguvu ya mwili, bado hawakuwa na utulivu mkubwa eneo la nyuma hasa kipindi cha kwanza.
Che Malone Fondoh 6
Bado alikuwa na wasiwasi, kutokana na presha ya mechi, ilikuwa kama Chamou walijikuta wanajichanganya kwa presha kuingia miguuni.

Fabrice Ngoma 6.5
Alionekana sana wakati Simba inataka utulivu, kitu muhimu alikuwa na msaada wakati wa mashambulizi ya adhabu na kona akiruka vizuri.
Yusuf Kagoma 5
Alianza vyema mchezo, lakini kadi yake ya pili ya njano iliyozaa nyekundu dakika ya 49 kipindi cha pili, ilitibua saikolojia kwa Simba kwa kuacha pengo uwanjani.
Joshua Mutale 8
Alifunga bao muhimu la kwanza kwenye mazingira magumu, akapiga krosi kwa Kapombe ambaye alipaswa kuifunga bao la pili. Na kitu kikubwa ni namna alivyokuwa anaitengeneza kasi ya mashambulizi ya timu yake kwa kukimbia haraka na kumnyima utulivu kiungo Mamadou Camara.
Steven Mukwala 6.5
Kazi kubwa aliyoifanya ni kuwapa presha mabeki wa Berkane wakati wanaanzisha mashambulizi. Alidhani ameifungia Simba bao la pili kwa kichwa lakini likakataliwa na VAR.

Jean Ahoua 6
Bado hana kasi sana, anashindwa kuwa na msaada katika kuwaongezea presha wapinzani. Frii-kiki yake nusura iliipa Simba bao ambalo lilikataliwa na VAR.
Ellie Mpanzu 7
Kasi yake ilikuwa kitu muhimu kwenye eneo la mwisho la Simba, krosi yake yake ilitengeneza bao la kwanza, kipindi cha pili akapotea.
Walioingia Valentin Nouma 5
Aliingia kipindi cha pili, angekuwa na hesabu za haraka angeinusuru timu yake kuruhusu bao kama angeokoa kwa haraka.
Kibu Denis 5
Aliingia kipindi cha pili lakini bado hakuwa na nguvu kama kawaida yake.
Lionel Ateba 5
Aliingia kipindi cha pili lakini hakuwa na mengi ya kufanya kwani hakuletewa mipira mingi ya mbele wakati wote timu yake imebakiwa na wachezaji 10 baada ya kadi nyekundu ya Kagoma.