Mastaa WANANE waitikisa Simba

Muktasari:

Mpaka kufikia leo, Kagere ametimiza siku 118 ambazo ni sawa na saa 2,808 bila kufunga bao lolote kwenye mechi za mashindano. Mara ya mwisho alitupia mabao manne dhidi ya Singida United timu yake ilipoibuka na ushindi wa mabao 8-0.

SINTOFAHAMU kubwa imeibuka katika benchi la ufundi la Simba baina ya Kocha Mkuu, Sven Vandenbroeck na mastaa wanane wa timu hiyo akiwemo straika namba moja, Meddie Kagere.

Mpaka kufikia leo, Kagere ametimiza siku 118 ambazo ni sawa na saa 2,808 bila kufunga bao lolote kwenye mechi za mashindano. Mara ya mwisho alitupia mabao manne dhidi ya Singida United timu yake ilipoibuka na ushindi wa mabao 8-0.

Kagere aliyemaliza msimu uliopita katika Ligi Kuu akiwa na mabao 23, licha ya kushindwa kufunga bao lolote tangu kurejea kwa msimu wa ligi amekuwa hachezi kikosi cha kwanza mara kwa mara.

Taarifa za ndani ya Simba zinasema kuna hali ya sintofahamu baina ya locha na mastaa hao, ingawa amekuwa mgumu kuzifafanua.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, mbali ya Kagere, kocha na benchi lake hawapo vizuri na Ibrahim Ajibu, Deo Kanda, John Bocco, Yusuph Mlipili, Beno Kakolanya, Sharaf Shiboub na wikiendi iliyopita ameongezeka kwenye idadi hiyo Mohammed Hussein ‘Tshabalala.

Mwanaspoti limedokezwa kwamba ishu ya Kagere imefikia hatua mbaya kwani amewadokeza marafiki zake kwamba hafurahishwi na uamuzi wa kumsotesha benchi huku akiwa hana tatizo la kiafya.

Tangu ligi irejee Simba imecheza mechi tano dhidi ya Ruvu Shooting ambayo alicheza dakika 90, baada ya hapo zilifuata mechi mbili dhidi ya Mwadui ambayo hakuwepo hata benchi wakati dhidi ya Mbeya City alisota benchi.

Kwenye mechi ya Tanzania Prisons, Kagere alicheza dakika zote wakati ile na Ndanda waliyocheza juzi Jumapili Uwanja wa Nangwanda aliingia kipindi cha pili.

Taarifa hizo zinasema hali ya kukaa benchi wakati anataka kutetea ufungaji bora wake inamkera Kagere ambaye amekuwa akiwaambia marafiki zake kuwa anafikiria kufanya uamuzi mgumu.

Kwa upande, Ajib inadaiwa alianza kutibuana na kocha baada ya kuchelewa kambini timu iliporipoti awali, lakini tangu hapo mwalimu amekuwa hafurahishwi na uwajibikaji wa mchezaji huyo na ndio sababu kumtupa jukwaani.

Katika mechi dhidi ya Prisons alicheza dakika 45, huku zingine akibahatika sana husotea benchi kama ilivyo kwa Shiza Kichuya.

Naye Kanda ambaye juzi alianza dhidi ya Ndanda, amekuwa akisota benchi huku mechi ya mwisho kuanza ikiwa ni dhidi ya Yanga ambayo alitupia bao moja katika sare ya mabao 2-2. Inaelezwa kwamba kocha amewaambia wenzake kwamba hayupo fiti ndio maana hamtumii.

Kwa upande wa Bocco inadaiwa ishu yake na kocha ilianza kwenye kikao cha kujadili kikosi kilichoivaa Coastal Union, ambako alikereka na kauli ya mwalimu aliyewaambia yeye na Kagere watacheza wanavyojua, na baadaye alimfuata na kutaka kujua kisa, ndipo kukaibuka kutoelewana na picha zikawa haziendi.

Yusuph Mlipili amecheza mechi moja akiingia dhidi ya Mwadui FC huku benchi likisisitiza kwamba hatatumika kwa vile hayupo fiti ilhali mlinda mlango, Kakolanya, amekuwa akisota jukwaani kwa kile ambacho kocha wa makipa, Mwarami Mohammed alichodai kwamba hayupo fiti.

Ingawa na Sven mwenyewe ameamua kumkaushia na kumsogeza benchi Ally Salim ambaye ni chipukizi.

Shiboub ambaye amerejea kambini hivi karibuni akitokea nchini kwao, Sudan inadaiwa kwamba hana uhusiano mzuri na kocha kwa madai kuwa amekuwa hamwamini huku akimfundisha vitu ambavyo haviendani na mchezaji wa kiwango chake. Kabla ya corona alikuwa akicheza pia kwa nadra. Kasheshe jipya kutokea ni lile la juzi dhidi ya Tshabalala ambaye alizuiwa kupanda basi kwenda mazoezini siku moja kabla ya mechi na Ndanda FC kwa madai kwamba alichelewa na katika mchezo huo hakutumika wala kukaa benchi.

Mmoja wa vigogo wenye ushawishi mkubwa ndani Simba, aliliambia Mwanaspoti kuwa Kocha Sven amekuwa na uamuzi mgumu kwa baadhi ya wachezaji ingawa mara kadhaa umekuwa ukigharimu ubora wa timu uwanjani.

“Unajua Kagere ni moja ya wachezaji wakubwa kuanzia Simba na Afrika Mashariki akiweka rekodi mbalimbali za kufunga na kuongoza mbio za ufungaji msimu huu, sasa anamuweka vipi benchi mchezaji kama huyo ambaye hata akicheza huwa anafanya vizuri?” alihoji.

Mwanaspoti lilimpata Kagere mwenyewe aliyesema anachojua kuhusu kutocheza katika kikosi cha kwanza ni uamuzi wa kocha mkuu ambaye huwa anachagua wachezaji kulingana na staili anayotaka kwa siku husika.

“Nipo fiti kwa ajili ya kuipigania timu kupata mafanikio mengi zaidi, lakini hata kutimiza malengo yangu ya kufunga mabao kuliko niliyonayo wakati huu, jambo la kutoonekana katika michezo mingine au kuingia kipindi cha pili hayo ni mambo ya benchi la ufundi,” alisema Kagere.

Kocha Sven alipotafutwa na gazeti hili simu yake iliita bila kupokewa huku msaidizi wake, Suleiman Matola akisema mambo yote ya kiufundi wamekubaliana atazungumzia bosi wake.

“Ni utaratibu tu ambao tumejiwekea, masuala yote ya kiufundi yanayowahusu wachezaji anaongea Sven, siwezi kuzungumzia suala hilo la Kagere au mchezaji yeyote yule kutokana na maagizo ambayo nimepatiwa na mkubwa wangu,” alisema.