Sven kuifumua safu ya ulinzi wa Simba SC

Muktasari:

Simba vinara wa Ligi Kuu Bara wakiwa na pointi 44 katika michezo mitano iliyopita ukiwemo mmoja wa Kombe la FA dhidi ya Mwadui FC, wameruhusu kufungwa mabao saba.

Dar es Salaam. Tatizo la Simba SC kuruhusu mabao mfululizo kumeanza kuumiza kichwa kocha Sven Vandenbroeck akiweka bayana atapangua safu yake ya ulinzi katika mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Coastal Union.

Simba vinara wa Ligi Kuu Bara wakiwa na pointi 44 katika michezo mitano iliyopita ukiwemo mmoja wa Kombe la FA dhidi ya Mwadui FC, wameruhusu kufungwa mabao saba.

Kocha Sven alisema pengine wachezaji wake watakuwa wamechoka hivyo amepanga kutoa nafasi kwa wengine ili kuhakikisha wanaondokana na tatizo katika safu ya ulinzi inayowategemea Pascal Wawa na Erasto Nyoni.

“Kabla ya mchezo wa ujao, kuna mambo tutayafanyia kazi pamoja, lakini muda ni mdogo wa kujiandaa ninaimani kuwa kuingia kwa wachezaji wapya ambao hawakucheza mchezo uliopita kutaongeza kitu.

“Siwezi kusema nani ni tatizo kutokana na kuruhusu kwetu mabao ya aina moja kila siku, lakini naweza kusema hili ni tatizo la safu yote ya ulinzi, tunatakiwa kuzinduka,” alisema kocha huyo.

Tangu Simba waruhusu mabao mawili katika mchezo dhidi ya Yanga, Januari 4 mwaka huu, waliendelea kuruhusu mabao mengine katika michezo iliyofuata mbele yao ambayo ni dhidi ya Mbao na Alliance waliruhusu bao moja katika kila mchezo licha ya kuvuna pointi sita wakiwa Kanda ya Ziwa.

Kwa mara nyingine tena, Simba waliruhusu mabao mawili katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu dhidi ya Namungo ya Lindi.

Mbali na makosa ya hapa na pale ambayo yamekuwa  yakiwagharimu Simba  kupitia  safu yao ya ulinzi  inayoundwa na  Shomari Kapombe, Mohammed Hussein, Wawa na Nyoni, wekundu hao wa Msimbazi wameonekana kukosa kiungo mkabaji mwenye kutekeleza majukumu yake kwa zaidi ya asilimia 70.

Mkude amekuwa akicheza vizuri kama kiungo mkabaji   lakini sio aina ya mchezaji ambaye anaweza kupokonya mipira na kuifanya Simba kuwa imara katika safu yao ya ulinzi kama ilivyokuwa kwa James Kotei msimu uliopita.