Kagere: Niliichagua Yanga, Simba wakapindua meza

Muktasari:

Kagere anasema mfanyakazi yeyote anapenda masilahi mazuri na mchezaji ni mfanyakazi kama walivyo wengine, kwa maana hiyo inapokuja ofa nzuri hakuna ambaye anaikataa labda awe tajiri ambaye ana mali nyingi na ameridhika katika maisha.

UNAKUMBUKA lile picha ambalo Simba walikutana nalo mwaka 2012? Ndio hilohilo wakati wanataka kumsajili kiraka Mbuyu Twite. Unaambiwa vigogo wa klabu hiyo walikwenda hadi nchini Rwanda ambako alikuwa akiichezea APR.
Wakati wakiwa na asilimia 60 za kumnasa beki huyo, Yanga waliizidi Simba kete kwa kwenda na mzigo wa maana kulekule na kukamilisha usajili wake huku vigogo wa Wekundu wa Msimbazi wakipigwa butwaa kwa meza ilivyopinduliwa.
Sakata lake lilishtua sana.

Sasa Simba nao hawakutaka kuremba kwa Meddie Kagere, ambaye ni Mnyarwanda kama ilivyo kwa Twitte licha ya kuwa asili yake ni DR Congo, walimalizana naye fastafasta baada ya kumalizika kwa mashindano ya Sportpesa nchini Kenya alikokuwa akitesa na Gor Mahia. Kagere amefunguka mambo kibao katika mahojiano yake na Mwanaspoti wakati alipotembelea Makao Makuu ya Mwananchi Communications Limited, Tabata Relini, Dar es Salaam.

YANGA MBONA
FRESHI TU
Kabla ya kuondoka kwa aliyekuwa kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera alieleza kuwa miongoni mwa nyota ambao kama atapata nafasi ya kuwasajili kutokea Simba ni Kagere kwani ni mmoja wa wachezaji mahiri na wenye kutambua kazi na majukumu yao.
Kagere anasema mfanyakazi yeyote anapenda masilahi mazuri na mchezaji ni mfanyakazi kama walivyo wengine, kwa maana hiyo inapokuja ofa nzuri hakuna ambaye anaikataa labda awe tajiri ambaye ana mali nyingi na ameridhika katika maisha.
“Kama Yanga wanakuja na ofa kubwa nzuri zaidi ambayo naipata Simba, kwa maana ya mshahara na kunipa mahitaji yote ya msingi ambayo nitayataka basi nipo tayari kwenda kwani ukweli hakuna mchezaji anayependa timu kuliko masilahi yake binafsi,” anasema Kagere.
“Labda leo nizungumze ukweli kabla ya Simba kunisajili nilikuwa nimekubaliana kila tu na Yanga, lakini viongozi wa Simba wakataja na ofa nzuri ambayo ilibadili mawazo na nikaamua kusaini kwao na nilifanya hivyo kutokana na mpira kuwa ndio biashara yangu ambayo inanipatia ugali na pesa ya kuendesha familia.”
Anasema, “Simba walikuja wakiwa na kila kitu na walikuwa tayari kunipatia, wakati huohuo tofauti na Yanga walinipa ahadi ya kunipatia huku nikiwa tayari nimeshakubaliana nao. Nilifanya maamuzi ya kugeuka na kuachana nao kwenda Simba ambao walikuwa na zaidi ambacho nataka.
“Baada ya maisha ya mpira watoto wangu wataniomba pesa ya maziwa hawataniomba timu ambayo naipenda, kwa maana hiyo wakati huu ambao nacheza ni sahihi kuangalia masilahi mazuri na kwenda kutumikia huku  kama Yanga wataweza kunipa zaidi ya vile ambavyo napata Simba wakaoongee na uongozi. Nina imani watakubali kuniachia kwani watakuwa wanapata pesa ya usajili kwani, bado nipo na mkataba wa muda mrefu.”

MECHI ZA DABI
Kagere kabla ya kusajiliwa na Simba alikuwa Gor Mahia ya Kenya ambapo huko wakikutana kati ya timu hiyo na AFC Leopards, mchezo wa upinzani wa aina yake ambao ulipachikwa jina la Mashemeji Dabi.
Lakini, hapa Tanzania, Kagere pia amecheza mechi mbili ya Kariakoo Dabi kati ya Simba dhidi ya Yanga ambazo zote zilikuwa msimu uliopita ambapo mchezo wa kwanza ulimalizika kwa suluhu kabla ya ule wa pili kushinda bao 1-0 ambalo alifunga.
Kagere anasema tofauti ya Mashemeji Dabi huwa mechi inayoonekana ya kawaida kwani Kenya wala haina msisimko na mashabiki ni walewale wachache ambao hushangilia kila siku ndio wanaofanya hivyo.
“Mashemeji Dabi hata ukiingia uwanjani unakuwa kama mchezo wa kawaida, mashabiki wenyeji hawajitokezi kwa wingi na kuujaza uwanja jambo ambalo naona mechi ya kawaida kama zilivyo nyingine,” anasema.
“Lakini Kariakoo Dabi ni mechi kubwa ya aina yake ambayo nimewahi kucheza, mashabiki nchi nzima wanaizungumzia na kuilezea hata kama si mpenzi wa soka, pia wanakuja kwa wingi na kuujaza uwanja,” anasema.
“Inapofika mechi ya Simba na Yanga hamasa inaongezeka kila eneo na jambo la kuja kwa mashabiki wengi uwanja huwa nalipenda na linanipa moyo wa kufanya zaidi ya kile ambacho ninacho, kwa maana hiyo Dabi ya Tanzania ni nzuri kuliko ya Kenya.”

MAPENZI NA MUZIKI
Kagere anasema kwa kawaida huwa anapenda muziki kwa maana vitu hivi viwili vina uhusiano wa karibu kwa kuwa mchezaji mpira mzuri, basi atakuwa pia anajua kucheza muziki.
“Ukiwa unajaribu kufanya mazoezi ya kucheza muziki, basi ni kama yale ambayo unafanya kwa ajili ya mpira au kuwa unacheza mpira kabisa ndio maana nimekuwa nikipenda mpira,” anasema nyota huyo wa Simba.

TOFAUTI YA LIGI
Kagere anasema vitu ambavyo anaweza kutofautisha ligi ya Kenya na Tanzania ambazo zote amecheza, soka la Bongo lina mashabiki wenye mzuka na wanapenda kweli soka tofauti na Kenya ambako kuna mashabiki wa kawaida. “Hapa Tanzania watu wamekuwa wakipenda ligi yao na hata wachezaji, kwa maana ukifanya vizuri unakuwa shujaa kwao na kila mahala ukipita wanakushangilia, lakini unapofanya vibaya mambo huwa kama hayo.”

MWENDELEZO
WA UFUNGAJI
Kagere anasema mwendelezo wake wa ufungaji mabao katika kila mashindano kuanzia Kenya akiwa na Gor Mahia ni suala la kujiamini tu.
“Kwangu huenda nikafanikiwa kufunga kutokana na malengo yangu niliyojiwekea katika kila mechi. Natamani kufunga na huwa napenda kufanya vizuri zaidi ya msimu uliopita, ndio maana naonekana mpya mara kwa mara,” anasema Kagere, ambaye msimu uliopita alifunga mabao 23, kwenye Ligi Kuu Bara na kuwa mfungaji bora. “Bado natamani kufanya zaidi ya sasa, hayo ndio malengo kwani nafasi yangu ni ushambuliaji na hata Simba wamenileta kufanya kazi hiyo tu.”

KUKWAMA
KWA MABAO
Kagere anasema anaonekana kushindwa kufunga mabao katika mechi nne kati ya kumi ambazo kikosi cha Simba kimecheza msimu huu, lakini imekuwa hivyo kutokana na sababu mbalimbali ambazo amekuwa akikutana nazo.
“Kwanza nimekuwa sina muda wa kutosha wa kupumzika kwani nacheza dakika zote tisini nikiwa Simba na hivyohivyo nikiwa katika timu ya taifa, kwa maana hiyo inakuwa ngumu kuweza kufunga katika kila mchezo,” anasisitiza Kagere.
“Lakini kila timu ambayo Simba tunakutana nayo kila mchezaji au mabeki wa timu pinzani akili zao zote muda mwingi zinakuwa kwangu, kwa maana hiyo nalazimika kutumia nguvu nyingi ili kuwazidi na kupata nafasi ya kufunga.
“Ndio maana kuna muda nashindwa kufunga lakini natamani kutoa pasi ya goli kwa mwenzangu aweze kufunga na limeonekana hilo katika baadhi ya mechi ambazo sikufunga, lakini kuna muda nalazimika kupambana nje ya uwezo wangu wa kawaida.
“Lakini pia nami ni binadamu kuwa muda naweza kupanda na kushuka, hilo ndiol limenikuta wakati huu, lakini nimelichukulia kama changamoto ambazo nina imani muda mfupi nitazishinda na mambo kuwa mazuri kwa upande wangu.”

CHANGAMOTO
Kagere anasema katika maisha ya Tanzania tangu ameanza kuishi hapa nchini, hakuna changamoto kubwa ambayo amewahi kukutana nayo kwani muda mwingi amekuwa si mtembeaji wa maeneo mbalimbali, bali akitoka katika mechi au mazoezi huwa anawaza kula na kupumzika.
“Labda changamoto ambayo naweza kueleza nakutana nayo hapa Tanzania ni hali ya hewa ya joto kwa muda mwingi, lakini tofauti na hapo kila kitu kwangu kinakwenda sawa na nafurahia kuishia na Watanzania kwani muda mwingi ni watu wenye upande na furaha kuliko sehemu nyingine ambazo nimeishi,” anasema.

NJE YA UWANJA
Kagere anasema kwa watu wasiomfahamu na wamezoea kumuona akiwa uwanjani maisha yake ya nje ya uwanja ni mtu wa kawaida ambaye anaweza kuishi na mtu yeyote na mazingira yoyote ambayo anakutana nayo.
“Kingine muda wote nimekuwa ni mtu wa furaha ambayo inanisababisha kuipenda kazi yangu kwani nafahamu ikiwa hivyo nitaweza kufanya vizuri, kama nikiwa nanuna mara kwa mara siwezi kufanya vizuri kazi nitakuwa naichukua,” anasema Kagere ambaye msimu uliopita katika Ligi ya Mabingwa Afrika alimaliza akiwa na mabao sita.
“Kwa maana hiyo kwangu nje ya uwanja ni mtu wa kawaida nisiyekuwa na mambo mengi kwani muda mwingi naishi kwa kuheshimu kazi yangu ambayo imenileta hapa Tanzania.”
 
MABEKI WAMPANIA
Kagere anasema hakuna beki ambaye amekuwa tatizo kwake, lakini kila timu ambayo amekuwa akikutana nayo mabeki wamekuwa wanamchunga muda wote kutokana kutambua kwamba wakimuacha hata sekunde moja anaweza kuwafunga.
“Kila beki ambaye nakutana naye anataka kunikaba mwanzo mwisho, hilo nalitambua lakini nimelichukulia kama changamoto kwangu ili kuweza kuwazidi, lakini mabeki kutoka hizi timu ndogo ndio nawaona changamoto kubwa kwani wanaonekana wakicheza huku wakipewa maelekezo ya kunikaba mimi muda wote.
“Muda mwingine bora kukutana na Azam au Yanga mabeki wao huwa wanacheza katika nafasi na inakuwa rahisi kwangu kuliko hawa wa timu nyingine, lakini nalitambua hilo lazima nitakutana nalo na linakuwa kama changamoto kwangu,” anasema Kagere.

PACHA SIMBA
Msimu uliopita Simba pacha wa Kagere walikuwa John Bocco na Emmanuel Okwi ambaye kwa sasa hayupo katika kikosi hicho, na walikuwa hatari zaidi katika mechi za ligi, Ligi ya Mabingwa Afrika na mashindano mengine ya ndani kutokana na kasi yao ya kufunga mabao. Msimu huu baada ya kuondoka Okwi, mambo yalikuwa tofauti kwani Bocco anakabiliwa na majeraha yaliyomuweka nje mpaka sasa, jambo ambalo linamlazimu Kagere kucheza na Miraji Athumani na Sharafeldin Shiboub, na muda mwingine Cletous Chama.
Kagere anasema msimu uliopita walikuwa na pacha nzuri, lakini yeye si mshambuliaji bora wa kucheza na mchezaji fulani, ndio maana yupo tayari kucheza na yeyote na ndivyo ilivyo hata msimu huu. “Mimi siyo straika wa kutafutiwa mchezaji fulani ndipo niweze kufanya vizuri, bali yeyote ambaye nakuwa naye namuangalia aina yake ya uchezaji, basi huwa nafanya vile ambavyo anaweza ili kuweza kuelewana na mwisho wa siku kama sijafunga, basi anafunga mwingine na hilo limeonekana msimu huu pia,” anasema.

TUZO ZA
MCHEZAJI BORA
Katika orodha iliyotolewa wiki iliyopita ya wachezaji 30 kutoka katika timu mbalimbali kumsaka mchezaji bora wa Afrika ambaye anacheza ndani Kagere, ni miongoni mwao.  “Ni jambo kubwa na la kushukuru kwangu kutokana na kuwa siyo kitu kidogo katika maisha yangu ya soka, kwani wametambua mchango (wangu) kutokana na kazi ambayo niliifanya msimu uliopita licha ya kwamba msimu huu tumeshindwa kufika mbali.”
Anasema: “Hata kama nisipofanikiwa kuchukua tuzo hiyo ni jambo kubwa ambalo hata timu yangu ya Simba imeweza kuingia katika orodha ya timu zilizotoa wachezaji wanaowania tuzo hiyo kubwa katika soka la Afrika.”

UD SONGO WATIBUA
Msimu uliopita Simba waliishia katika hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika walikoondolewa na TP Mazembe, lakini msimu huu mambo yamekuwa tofauti kwao kwani waliondolewa katika hatua ya awali na UD Songo.
Kagere anasema mchezo wa mpira huwa na matokeo matatu na baada ya kupata suluhu ugenini wachezaji wa timu yao wengi waliamini kuwa UD Songo hawawezi kupata matokeo mazuri  katika uwanja wao wa nyumbani.
“Morali na nguvu ambayo tulikuwa nayo kutokana na kuzifunga timu kubwa za AS Vita, Al Ahly na JS Soura tuliwachukua kama UD Songo ni timu ya kawaida na tunaweza kuwafunga katika uwanja wetu wa nyumbani ambao huwa tunapata nguvu ya kutosha kutoka kwa mashabiki wetu,” anasema.
“Lakini UD Songo walikuja kivingine na kutushangaza jambo ambalo wachezaji wanarudi katika hali ya kushindana muda umeisha na hatuna la kufanya zaidi ya matokeo ambayo tumeyapata ambayo mpaka leo yametuumiza kweli kweli.
“Lakini limekuwa fundisho ndani ya timu yetu kutambua kila timu ambayo tunacheza nayo ni sawa na sisi kwa maana hiyo hakuna kuichukulia kama ni ndogo mpaka hapo ambapo tutaweza kupata pointi tatu dhidi yao.”

AKUTANA NA
MATAPELI
Kagere anasema jambo ambalo hatalisahau ni pale alipokutana na matapeli hapa nchini ambao walitaka kumchukulia pesa kwa kutumia simu, ingawa baadaye alikuja kushtuka na kuachana nao.
“Kuna siku nilitumiwa ujumbe katika simu kuwa hiyo pesa tuma kwa namba hii, kutokana na mkataba wa nyumba kuwa umeisha na unatakiwa kulipa, jambo ambalo baadaye nilishtuka na kuona kuwa ni wezi hawa,”  anasema Kagere.

JICHO MOJA
Kagere anasema aina yake ya kushangilia kwa kuziba jicho moja imekuwa ikizua maneno kutoka kwa baadhi ya watu miongoni mwao wakiwamo wanaoihusisha na imani potofu, jambo ambalo si kweli akisisitiza kuwa kila mtu ana haki ya kuzungumza atakalo. “Kwangu kushangilia kwa kuziba jicho moja hiyo ni aina binafsi ya ushangiliaji kama ambayo nimekuwa nikishangilia kwa mtindo mwingine, kwa maana hiyo wala sijali hayo maneno ya watu,” anasema Kagere ambaye mpaka sasa katika ligi amefunga mabao manane.

KUONDOKA KWA AUSSEMS
Kagere anasema kwa upande wake Aussems ni miongoni mwa makocha wazuri ambao amewahi kufundishwa nao na hata muda wote alivyokaa nae katika kikosi cha Simba wameishi vizuri kwa misingi ya kufanya kazi wakitegemeana. “Aussems licha ya kwamba ni kocha mzuri lakini ameshaondoka, mimi ni mfanyakazi natakiwa kufanya kazi na kocha mwingine yeyote ambaye atakuja kuchukua nafasi hiyo.”