Kazi ipo... Huu mziki wa Ajibu wamtesa mbrazili

Tuesday October 15 2019

 

By Mwandishi wetu

MSHAMBULIAJI wa Simba, Ibrahim Ajibu amesema ni mapema kumkosoa Mbrazil, Wilker Da Silva aliyecheza naye mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi Bandari FC ya Kenya na waliibuka na ushindi bao 1-0.

Wawili hao walianza pamoja kwenye mchezo huo na Wilker alishindwa kuendana na kasi ya Ajibu kwenye eneo la ushambuliaji Ajibu akicheza namba kumi na Wilker (9).

Akizungumza na Mwanaspoti, Ajibu alisema Mbrazil huyo ametoka kuwa majeruhi hivyo, isingekuwa rahisi kuendana na kasi yake na kushindwa kufunga bao ndani ya dakika alizopewa.

“Nilicheza namba 10 yeye alicheza tisa kama mshambuliaji wa mwisho, nilijitahidi kufanya majukumu yangu kama nilivyoambiwa na kocha, lakini hakukuwa na mtu wa kumalizia mipira mingi niliyoitengeneza.

“Baada ya mabadiliko, nafasi yake nilicheza mimi, niliyokuwa nacheza alicheza Sharaf Shiboub na nafasi yake ikachezwa na Said Ndemla, tulicheza kwa kuelewana na kila mmoja alikaa sehemu anayotakiwa kwa wakati.

“Jukumu la mshambuliaji wa mwisho ni kuhakikisha anakaa eneo sahihi ili aletewe mipira na kumaliza kazi,” alisema.

Advertisement

Kuhusu kutoonekana mara kwa mara kama ilivyokuwa wakati akichezea Yanga, Ajibu alisema:

“Nashindwa kuonekana bora Simba kwa sababu sipati nafasi ya kuanza, pia wanacheza mipira ya chini na kwa kasi ndogo kitu ambacho kinachelewesha kufanya kazi yangu ya mwisho na hata nikiifanya natakiwa kucheza na Meddie Kagere au John Bocco ambao, wanaweza kucheza mipira ya aina yote juu na chini.

Wakati huo huo, Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Ausems alisema: “Nilisema huu ni mchezo kuangalia ubora na utimamu wa wachezaji ambao, huwa hawapati nafasi mara nyingi, Ajibu kwenye mchezo dhidi ya Bandari ameonyesha kitu tofauti.”

Wadau wamchambua Mbrazil

Mwanasoka wa zamani na mchambuzi wa soka nchini, Ally Mayai alisema wachezaji wa kigeni waliosajiliwa Simba walikuja kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa, hivyo viwango vyao ilibidi viwe vikubwa tofauti na wazawa.

“Wilker hajaonyesha utofauti kwa Bocco wala Kagere, msimu uliopita tuliona kabisa Emmanuel Okwi, Kagere walikuwa wakimpa changamoto Bocco na ndio kitu ambacho Wilker anatakiwa awe nacho lakini kwake amekuwa wa kawaida sana,” alisema.

“Yule beki wa kati (Tairone) ni mlinzi mwenye uwezo wa kujua kucheza na mechi, anaruka mipira ya juu vizuri, pia anajua namna ya kuanzisha mashambulizi, kikubwa ana misingi mizuri ya ulinzi kuhakikisha washambuliaji hawapiti,” alisema.

Advertisement