Ajibu afunguka, Yondani akosolewa

Muktasari:

Imezoeleka wakati wa utambulisho nahodha uwashika began a mgeni rasmini ndiye anayepeana mkono na wachezaji pamoja na timu pinzani.

Dar es Salaam.Wakati kitendo cha beki na nahodha wa zamani wa Yanga, Kelvin Yondani kugomea kumpa mkono mrithi wake, Ibrahim Ajibu jana Jumamosi, baadhi ya nyota wa zamani wa Yanga wamesema kitendo hicho cha Yondani kimeonyesha utovu wa nidhamu.

Akizungumzia kitendo hicho, Ajibu alisema anadhani wachezaji wenzake walimshangaa kuwatambulisha kwa kuwashika mikono kwani mara nyingi hawafanyi hivyo.

"Si kaka yangu Yondani pekee aliyesita kunipa mkono, hata Dante pia, Yondani aliniambia hii mpya, sina shida na kaka yetu huyu, sisi ni wadogo zake na mengi tunajifunza kutoka kwake," alisema Ajibu.

Ingawa baadhi wamemkingia kifua nyota huyo wa Yanga, lakini wengine wamesema kwa tafsiri ya mashabiki hakikuonyesha picha nzuri baina ya beki huyo na Ajibu ambaye ndiye nahodha wa Yanga sasa.

Yondani aligoma kumpa mkono Ajibu wakati akiwatambulisha wachezaji wa Yanga mbele ya mgeni rasmi, Waziri wa Habari Sanaa, Utamaduni na Michezo, DK Harrison Mwakwembe kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam katika mechi dhidi ya Simba ambapo Yanga ilifungwa bao 1-0.

Beki wa zamani wa Yanga, Pan African, Bakari Malima alisema alichofanya Ajibu hakikuwa sahihi kuwapa wachezaji wenzake mkono.

“Yondani bahati nzuri ni mzoefu katika mpira angemsoma Ajibu kuwa amekosea na ambacho angekifanya angempa mkono tu, kisha baadae akamwambia mdogo wangu, ulichokifanya umekosea," alisema Malima.

Alisema kiuhalisia nahodha anapaswa kumtambulisha mchezaji mwenzake kwa mgeni rasmi kwa kumshika bega, na mgeni ndiye anampa mchezaji mkono, hivyo tayari Ajibu alikuwa amekosea, ila Yondani alipaswa kumsoma tu mchezaji mwenzake na asingetengeneza viulizo kwa mashabiki kwa kugoma kumpa mkono.

Mshambuliaji wa zamani wa Taifa Stars, Peter Tino alisema amekichukulia kitendo hicho kama utovu wa nidhamu kwa Yondani, kwani hata kama mwenzake alikosea hakupaswa kuonyesha vile mbele ya mgeni rasmi, angesubiri pembeni akamuelekeza Ajibu anavyopaswa kufanya.

Kiungo wa zamani Yanga, Ally Mayay alisema kitendo cha Yondani kugomea mkono wa Ajibu wala sio ishu hakukuwa na mpangilio mzuri upande wa Yanga katika utambulisho.

"Watu wanaweza kudhani labda ni sababu Yondani alikuwa nahodha akavuliwa na kupewa Ajibu, lakini sio kweli, nijuavyo nahodha anawatambulisha wachezaji kwa mgeni rasmi na mgeni ndiye anayewapa mkono wachezaji, lakini si nahodha kama alivyofanya Ajibu," alisema Mayay.