Yanga yamtupia virago Ajibu kweupe

Muktasari:

Ajibu anaondoka Yanga akiwa ameacha historia ya kuwa mchezaji aliyetoa pasi nyingi za mabao msimu uliopita na kufunga mabao saba.

Dar es Salaam. Yanga imempa mkono wa kwaheri nahodha wake Ibrahim Ajibu kwa kumtakia maisha mema huko aendako baada ya kushindwa kufikia naye makubaliano ya kumuogezea mkataba mpya.

Ajib alijiunga na Yanga akitokea Simba kwa mkataba wa miaka miwili utakaofikia tamati Juni 30 mwaka.

Akizungumza Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Fredrick Mwakalebela alisema wanatambua uwezo wa Ajibu na walitamani kuona anaendelea kucheza katika klabu yao, lakini mwenye uamuzi ya kuendelea au kutoendelea ni mchezaji mwenyewe.

"Tumefanya mazungumzo na mchezaji huyo kwa muda mrefu sana, lakini ameshindwa kuonyesha nia ya kutaka kusalia kikosini kwetu tunamtakia kila lenye heri huko aendapo na kama hatapata nafasi basi milango bado ipo wazi."

"Hakuna timu siyotaka kufanya kazi na Ajibu kutokana na uwezo alionao, lakini hatuwezi kumlazimisha mkataba wake na sisi unamalizika mwishoni mwa mwezi huu hivyo hakuna ulazima wa kuendelea kumshikiria wakati kuna timu zinamuhitaji tunamuachia," alisema Mwakalebela.

Mapema hivi karibuni Ajibu aliuambia mtandao huu kuwa hajatia saini Simba wala Yanga kama inavyodaiwa na baadhi ya wadau nchini.

Nahodha huyo wa Yanga alisema taarifa zinazomuhusisha kuwa ametia saini mkataba wa awali na klabu ya Simba hazina ukweli.

“Sijatia saini mkataba wa awali na mkubwa na Simba. Sijasaini Simba kama inavyoelezwa, wala Yanga ingawa niko tayari kucheza timu yoyote ile hata Yanga kama tutaelewana,"alisema Ajibu.

Ajibu hadi sasa haijajulikana anatua katika klabu gani ni baada ya kuhusishwa na TP Mazembe aliyokata kujiunga nayo kwa kushindwa kufikia makubaliano na mabingwa hao wa DR Congo.

Kocha Mwinyi Zahera alisema Ajibu hakuwa katika mipango kwa usajili wa msimu ujao kwa kuwa alikuwa mbioni kujiunga na TP Mazembe ya DR Congo.

"Nilisikia anakwenda TP Mazembe sikumjumuisha katika orodha yangu ya wachezaji ambao nitakuwa nao msimu ujao,"alisema Zahera.