MO abeba dili la Ajibu

Muktasari:

  • Ajibu aliyeifungua Yanga jumla ya maba 13 tangu ajiunge nayo akitokea Simba msimu uliopita inaelezwa hana tatizo la kurejea Msimbazi ambapo inaelezwa sharti lake kubwa ni mazungumzo yake kufanyika moja kwa moja na MO kitu ambacho sasa kipo katika hatua za mwisho.

MASHABIKI wa Simba wakiwa bado wamejawa na furaha baada ya chama lao kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huenda raha ikaongezea zaidi kufuatia taarifa za vigogo wa klabu hiyo kuwapo mbioni kumrejesha mchezaji wao wa zamani, Ibrahim Ajibu kikosini kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.

Utamu zaidi ni kitendo cha bilionea wa klabu hiyo, Mohammed ‘MO’ Dewji, akiwa ameliingilia kati dili la kiungo huyo mshambuliaji, akitaka mwenyewe kusimamia shoo ya mchezaji huyo kurejea Msimbazi.

Si mnajua Ajibu hakuambatana na timu yake kwenda Iringa ilipoifuata Lipuli ya huko na kuchezea kichapo cha bao 1-0? Sasa imebainika kumbe nyota huyo akili yake yote kwa sasa ni mipango ya kutua Msimbazi na utamu zaidi ni dili lake lipo mezani kwa Bilionea MO Dewji.

Taarifa kutoka ndani ya Simba zinasema klabu hiyo, inataka kumrudisha nahodha huyo wa Yanga baada ya kuona kazi yake katika mkataba wake wa miaka miwili unaomalizika mwishoni mwa msimu huu na Wana Jangwani hao.

Anayesukuma usajili ni huo ni namba moja mwenyewe, yaani Bilionea MO Dewji ambaye anakubali vilivyo vitu vya Ajibu akijipanga kumsainisha mkataba mapema kabla ya ligi haijamalizika msimu huu.

“Ishu ya Ajibu ipo hivi, hajasaini lakini anaendelea na mazungumzo na MO sishangai unaponiambia hakusafiri na timu yake (Yanga) ili aendelee na mazungumzo ya kufanikisha usajili huo,” alifichua mmoja wa vigogo wa Simba.

Ajibu aliyeifungua Yanga jumla ya maba 13 tangu ajiunge nayo akitokea Simba msimu uliopita inaelezwa hana tatizo la kurejea Msimbazi ambapo inaelezwa sharti lake kubwa ni mazungumzo yake kufanyika moja kwa moja na MO kitu ambacho sasa kipo katika hatua za mwisho.

“Jamaa hana tatizo kabisa la kurudi Simba, ila amesisitiza anataka mazungumzo yake yafanyike chini ya usimamizi wa MO kama mambo yataenda kama yanavyokwenda sasa inawezekana akasaini mapema kabla ya ligi haijamalizika.”

Hata hivyo, inaelezwa ndani ya Simba baadhi ya vigogo wanadaiwa kutokubaliana sana na dili hilo ingawaje wanatambua uwezo wa kiungo huyo mshambuliaji, wakiwa na hoja kwamba licha ya kipaji chake lakini ana usumbufu ambao wasingependa kuupata tena kama misimu mitatu waliyokuwa naye kikosini.

Ajibu ambaye kwa misimu wake wa mitano kucheza Ligi Kuu akizitumikia Simba na Yanga, amefunga jumla ya mabao 39, yakiwamo 25 aliyotupia akiwa Msimbazi ndiye kinara wa kuasisti kwa sasa katika Ligi Kuu Bara akihusika na mabao 16, huku akifunga mabao sita akishika nafasi ya tatu ya wafungaji bora wa klabu hiyo msimu huu akitanguliwa na Heritier Makambo na Amissi Tambwe. Makambo ana mabao 12, huku Tambwe akifunga manane.

Gumzo kubwa kwa wikiendi iliyopita pale Uwanja wa Taifa wakati Yanga ikishinda 2-1 dhidi ya KMC ni kitendo cha Ajibu kutokea benchi na kisha kupiga krosi moja matata ambayo iliisaidia timu yake kupata bao la pili na la ushindi ikisindikizwa wavuni na beki Ali Ali, kwani alionekana kama anaonyesha ishara ya kuaga akiwapungia mashabiki wa Yanga huku pia akikivua kitambaa chake cha unahodha akiwanyooshea mashabiki hao kwa kuwapungia.

Mshambuliaji huyo amekuwa mgumu kuweka bayana ishu yake ya kutaka kurejea Msimbazi, ni kama alivyokuwa wakati wa usajili wake wa kujiunga na Yanga kutoka Simba.

Ajibu alichuna alipohusisha na dili hilo akipishana na kiungo mwingine, Haruna Niyonzima ambapo Mwanaspoti lilikuwa la kwanza kuripoti taarifa za mastaa hao na baadaye dili za nyota hao zote zikatiki.