Yanga yaanza na kiungo fundi wa boli

Muktasari:
- Katika kuhakikisha kila kitu kinaendelea kuwa sawa, mabosi wa klabu hiyo wameamua kuvuka maji ya bahari na kwenda visiwani Zanzibar kwa ajili ya kunasa saini na kiungo mmoja matata anayejua boli, ambaye muda wowote kuanzia sasa anaweza kuwa mali ya Jangwani kwani mazungumzo ya pande zote yalikuwa hatua y mwishoni.
MABINGWA wa Kihistoria Yanga, kwa sasa imeanza hesabu mpya za kukisuka kikosi kipya kwa ajili ya msimu ujao, kwa nia ya kuhakikisha inaendelea pale ilipoishia msimu huu ilipotwaa mataji matano tofauti, ikiwamo kutetea ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho (FA) kwa mara ya nne mfululizo.
Katika kuhakikisha kila kitu kinaendelea kuwa sawa, mabosi wa klabu hiyo wameamua kuvuka maji ya bahari na kwenda visiwani Zanzibar kwa ajili ya kunasa saini na kiungo mmoja matata anayejua boli, ambaye muda wowote kuanzia sasa anaweza kuwa mali ya Jangwani kwani mazungumzo ya pande zote yalikuwa hatua y mwishoni.
Ndio, Yanga ipo katika hatua za mwisho za kumalizana na kiungo wa Mlandege anayesifika kukaba kwa nguvu katika eneo la kiungo.
Kiungo huyo, Abdulnasir Abdallah ‘Casemiro’ ni miongoni mwa viungo bora waliofanya vizuri katika Ligi Kuu ya Zanzibar msimu uliopita na haraka Yanga ikamvamia.
Yanga ilikuwa kwenye msako wa muda mrefu kutafuta kiungo mkabaji ikianza kujiandaa na maisha ya baadaye endapo mkongwe Khalid Aucho ataondoka.
Taarifa kutoka ndani ya Yanga ni kwamba uongozi wa timu hiyo ulikuwa kwenye hatua za mwisho kumalizana na klabu ya Mlandege.
Mwanaspoti linafahamu Yanga tayari imeshamalizana na Casemiro, lakini hatua pekee iliyosalia ni kumalizana na klabu yake.
“Tumeshamalizana na mchezaji ilikuwa muda mrefu kitu pekee kilichosalia ni kumalizana na klabu yake tutakubaliana tu hakuna shida,” kilisema chanzo hicho ambacho ni kigogo wa klabu hiyo aliyeongeza;
“Ni kiungo mzuri sana anajua kukaba lakini pia anaweza kupandisha mashambulizi kwa kuchezesha timu na jambo zuri ni kwamba umri wake ni mdogo.”
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 20 ni moja ya wachezaji vijana walioonyesha viwango bora katika Ligi Kuu ya Zanzibar na kuiwezesha timu yake kubeba ubingwa wa ligi hiyo na kutetea pia Kombe la Mapinduzi kwa msimu wa pili mfululizo.
Jana Mwanaspoti lilimtafuta Rais wa klabu ya Mlandege, Kamal Abdulsatar Haji, akisema: “Ni kweli tunakaribia kumalizana, nitafute kesho (leo) nitakupa taarifa kamili.”
Mbali na Yanga inaelezwa kuwa Azam ilikuwa ikimpigia hesabu kiungo huyo ambaye alikuwa gumzo katika Ligi Kuu ya Zanzibar msimu uliopita ambapo timu hiyo ilitwaa taji la nane la ligi hiyo.