Hakufai Kanda ya Ziwa sio salama kwa makocha

Muktasari:

Presha imeongezeka kwa viongozi wengi wa timu baada ya Bodi ya Ligi (TPLB) kutangaza hali ya hatari katika kupunguza idadi ya timu za TPL kutoka 20 hadi 16, hivyo imekuwa rahisi kwa viongozi kuchukua hatua mapema kubadilisha mabenchi yao ya ufundi ili kukimbizana na hali halisi ya mambo yalivyo ndani ya timu zao.

LIGI Kuu imeendelea kushika kasi kwa namna yake. Lakini upepo umekuwa tofauti kwa timu za Kanda ya Ziwa kuwafungashia virago makocha wao kutokana na kupata matokeo mabaya kwenye Ligi Kuu na zile za FDL zinazotaka kupanda TPL.

Presha imeongezeka kwa viongozi wengi wa timu baada ya Bodi ya Ligi (TPLB) kutangaza hali ya hatari katika kupunguza idadi ya timu za TPL kutoka 20 hadi 16, hivyo imekuwa rahisi kwa viongozi kuchukua hatua mapema kubadilisha mabenchi yao ya ufundi ili kukimbizana na hali halisi ya mambo yalivyo ndani ya timu zao.

Kati ya timu zilizoanza kufanya maamuzi magumu ni pamoja na zile za Kanda ya Ziwa kwa kufumua mabenchi ya ufundi mapema, kuanzia zile za Ligi Kuu hadi zile za Ligi Daraja la Kwanza (FDL), tayari zimefanya mapinduzi ili kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri zaidi katika ligi zao.

MBAO FC- MAKOCHA 7

Timu hiyo ilipanda Ligi Kuu msimu wa mwaka 2016/17 kufuatia maamuzi ya Kamati ya Nidhamu ya TFF yaliyotolewa Aprili, 2016 ya kuzishusha daraja timu nne kutoka Kundi C baada ya kukutwa na hatia ya upangaji matokeo. Mbao FC ilipanda Ligi Kuu, sambamba na African Lyon na Ruvu Shooting ya Mkoa wa Pwani.

Mbao FC ilishika nafasi ya kwanza Kundi C kwa kuwa na pointi 12 baada ya kufutwa kwa matokeo ya timu za Geita Gold, Polisi Tabora, JKT Oljoro na JKT Kanembwa zilizokumbwa na mkasa huo wa upangaji matokeo.

Mpaka sasa timu hiyo imepita mikononi mwa makocha sita kwenye Ligi Kuu ukianchana na yule aliyeipandisha, ilianza na Etienne Ndayiragije aliyekaa msimu mmoja na nusu, kisha akafungashiwa virago na sasa anatesa pale Azam FC akitokea KMC huku akipewa jukumu la kukiongoza kikosi cha Taifa Stars. Alipoondoka nafasi yake ikienda kwa Novatus Fulgence ambaye kwa sasa yupo Gwambina FC.

Baada ya hapo timu ikawa mikononi mwa Amri Said ‘Stam’ aliyedumu kwa mechi saba pekee, kisha Ali Bushiri akabebeshwa zigo ambalo hakuweza kufika nalo mbali na kulimwaga kwa Salum Mayanga ambaye mambo hayakumuendea vyema akamuachia, Hemed Morocco anayeendelea kupambana nalo hadi sasa.

ALLIANCE FC - MAKOCHA 4

Ni timu mojawapo inayotumika kuzalisha vipaji vya soka kwenye akademi yake. Huu ni msimu wake wa pili kwenye Ligi Kuu ambapo ilipandishwa na Kocha Mbwana Makata ambaye alifungashiwa virago na kwenda kuitumikia Polisi Tanzania ambayo kwa sasa inatesa Ligi Kuu ingawaje, Makata yuko Dodoma FC.

Baada ya Makata kuondoka, uongozi ukamleta, Hamsin Malale ambaye maisha yake yalianza vyema lakini baadaye upepo ukabadilika na kazi akakabidhiwa Athuman Bilali ‘Billo’, kocha huyo ndio alikuwa wa kwanza kuonyeshwa mlango wa kutokea msimu huu ikiwa ni baada ya kuiongoza timu yake katika mchezo mmoja pekee na kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Mbao FC katika Uwanja wa CCM Kirumba Agosti 24 .

Nafasi yake ikachukuliwa na Kessy Mzirai akisaidiwa na Habibu Kondo aliyetokea Mwadui FC pamoja na Dady Gilbert.

Billali ambaye anatamba na jina la ‘Bilo’ aliingia katika kikosi hicho akichukua nafasi ya Malale Hamsini ambaye siku za hivi karibuni alionekana kwenye benchi la ufundi la Timu ya Ndanda FC.

Hivyo mabadiliko hayo yanaweza yakawasaidia au yakazidi kuiharibu timu kwa kuwa asilimia kubwa ya usajili wa wachezaji ulifanywa na kocha huyo aliyeondoka kutokana na matakwa yake.

Mchezo mmoja sio kipimo tosha kwa kumpima mtu kama amefeli au amefaulu kazi yake, uongozi wa Alliance FC ulifanya haraka kubadilisha benchi lake la ufundi kwani hata baada ya kuondoka kwa Billo, bado timu hiyo inasuasua. Katika michezo mitatu iliyocheza imeshinda mchezo mmoja na kutoa sare mmoja na kufungwa mmoja na mpaka sasa inakamata nafasi ya 11 kwenye msimamo wa TPL.

Hata hivyo, baada ya kuondoka, Bilo anafafanua kuwa yeye ndiye aliyeachana na timu hiyo baada ya kuona anaingiliwa majukumu yake ya ufundishaji.

PAMBA FC- MAKOCHA -3

Unapozungumzia timu kongwe kwenye hapa Tanzanaia ni pamoja na Pamba FC. Timu hii ipo nafasi ya sita kwenye Ligi Daraja la Kwanza baada ya kuvuna alama sita katika michezo minne.

Msimu uliopita iliachana na Yusuph Khamis ‘Sumbu’ kwa sababu mbalimbali na kumchukua Ally Kisaka amabaye kwa sasa anakinukisha pale Stand United, kwani alipoondoka, Muhibu Kanu akachukua nafasi.

Msimu huu, Kanu ameiongoza, Pamba FC katika mchezo mitatu pekee, katika mchezo uliopita dhidi ya Gipco ililala 2-0 pale Geita yaliyofungwa na Ruben Emmanuel pamoja na Nelson Richard, timu ilikuwa chini ya Kocha Venance Kazungu anayeendelea kulisukuma gurudumu hilo.

BIASHARA - MAKOCHA 3

Ilifanikiwa kupanda Ligi Kuu msimu wa 2018/19 ikiwa chini ya Kocha Amani Josiah alipoondolewa nafasi yake ilichukuliwa na Hitima Thierry ambaye kwa sasa anakinoa kikosi cha Namungo FC baada ya kufanikiwa kuipandisha Ligi Kuu akisaini mkataba wa miaka miwili kwa watoto hao kutoka Mji wa Ruangwa, Lindi.

Kuondoka kwa Hitimana kulifungua mlango kwa Amri Said ‘Stam’ kuziba nafasi hiyo ndani ya timu hiyo. Baada ya kuchana na Stam hadi leo uongozi unamsaka kocha wa kuziba nafasi yake na hapo ndio utagundua viongozi wengi hufanya maamuzi bila ya kujiandaa.

SINGIDA UNITED- MAKOCHA 7

Ukiachana na timu za Kanda za Ziwa, sehemu nyingine ambayo sio salama kwa makocha ni Singida United. Hadi sasa imebadilisha makocha mara saba.

Ilianza na Fred Felix ‘Minziro’ aliyeipandisha Ligi Kuu msimu wa mwaka 2017/18. Akafungashiwa virago nafasi yake ikachukuliwa na na Hans van der Pluijm aliyekuwahi kuinoa Yanga.

Baadaye Pluijm akaacha na timu hiyo na kujiunga na Azam FC. Nafasi ikamwangukia Hemed Morocco kuziba nafasi.

Naye pumzi ikamuishia njiani na Msebria, Dragan Popadic alikuja kuliongoza jahazi. Kuondoka kwake kuliwapa nafasi wazawa kuliongoza benchi la ufundi akiwemo, Shadrack Nsajigwa kabla ya kurudi kwa mara nyingine, Minziro hadi kumalizika kwa msimu uliopita.

Msimu huu ukawa mbaya kwake kuiongoza timu hiyo, baada ya michezo mitatu tu, Septemba 25 uongozi wa Singida United ukaachana naye na nafasi yake kuchukuliwa na aliyekuwa Kocha wa Mbeya City, Mnyarwanda Ramadhan Swanzurwimo.