Mbao FC yakamilisha kikosi kazi Ligi Kuu

Mwanza. Klabu ya Mbao FC imehitimisha usajili wake kwa kumnasa Kipa wa Majimaji FC, Hashim Mussa kwa kandarasi ya miaka miwili kuitumikia timu hiyo katika msimu ujao wa Ligi Kuu.

Mussa anakuwa mchezaji wa Saba kutua Mbao akiungana na Elias Zamfuko (African Lyon), Peter Mwangosi (Njombe Mji) Emanuel Mtumbuka (Dodoma FC) na Evarigestus Mujwahuki kutoka Mwadui FC.

Wengine ni Pastory Athanas kutoka Kagera Sugar na Raphael Siame aliyetoka Njombe Mji na wote hao wakisaini mkataba wa miaka miwili kuichezea timu hiyo.

Mwenyekiti wa Klabu hiyo, Solly Njashi alisema kuwa Kipa Mussa ndiye anawafungia zoezi la usajili na kwamba wachezaji wote wanaamini wataisaidia timu hiyo kufanya vizuri.

Alisema kuwa kwa sasa kazi iliyobaki ni ya benchi la ufundi kuhakikisha timu inapata matokeo mazuri na kwamba uongozi utatoa sapoti ya aina yoyote ili kufikia malengo.

“Usajili unafungwa leo usiku (jana)na sisi tumekamilisha wachezaji saba ambao Benchi la Ufundi lilipendekeza hivyo, kwa hiyo kazi iliyobaki ni kwa makocha kutimiza majukumu yao tutatoa sapoti ya kutosha,” alisema Njashi.

Mwenyekiti huyo aliwataka wadau wa soka jijini hapa kuacha kubeza jitihada za viongozi wa klabu na kwamba watoe sapoti ili kuziwesha timu kufanya vizuri.

“Lakini pia kuna baadhi ya wadau wanaoongea tu bila hata kusapoti chochote hawa wanatuumiza, wangekuwa wanasaidia timu zetu ingekuwa vizuri tofauti na wanavyofanya,”alisema Njashi.