Kocha Mbao FC aweka rekodi Ligi Kuu

Mwanza. Kocha wa Mbao FC, Amri Said ‘Stam’ ameweka rekodi mpya katika kikosi hicho katika mashindano ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Said amevunja rekodi ya aliyekuwa kocha wa Mbao Ettiene Ndayiragije, aliyejiunga na timu ya KMC ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Mbao imeweka rekodi ya kuongoza Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya kwanza tangu ilipopanda daraja msimu 2016-2017.

Mbao yenye maskani Wilaya ya Ilemela, Mwanza ipo kileleni kwa pointi saba baada ya kushinda mechi mbili na kutoka sare moja.

Akizungumzia mjini hapa jana, Said alisema mbali na kupata matokeo mazuri katika mechi tatu, ana safari ndefu ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.

“Bado tuna kazi ngumu ya kusaka pointi tatu katika mechi zinazofuata ili tujiweke katika nafasi nzuri, kwa sasa sifikirii ubingwa,” alisema Said.

Timu hiyo ilianza vyema msimu mpya, baada ya kuilaza Alliance bao 1-0, ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Stand United kabla ya kutoka suluhu na Singida United.

 

 

 

Msimu wa kwanza Mbao ilicheza mechi nne na kuambulia pointi moja kwa kutoka sare ya bao 1-1 na Stand United, ilifungwa na Mwadui bao 1-0 ilichapwa na Mbeya City mabao 4-1 kabla ya kunyukwa na African Lyon 3-1.

Msimu uliopita ilivuna pointi nne katika mechi nne ikianza kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar, ilifungwa na Singida United mabao 2-1, ilichapwa na Mtibwa Sugar 2-1 kabla ya kutoka sare 2-2 na Simba.