Pamba yarejea kwa straika Mzenji

Muktasari:
- Pamba ilianza harakati hizo tangu Januari 2025 za kumpata mshambuliaji huyo, ingawa hazikuweza kuzaa matunda, baada ya kuelezwa alisaini mkataba pia na Yanga, jambo lililosababisha dili lake kufa na kubaki Mlandege ili kumalizia msimu huu.
BAADA ya mabosi wa Pamba Jiji FC kumkosa mshambuliaji wa Mlandege, Abdallah Iddi ‘Pina’, katika dirisha dogo la Januari 2025, inaelezwa wameanza tena harakati hizo upya, ili kuhakikisha msimu ujao anakichezea kikosi hicho cha ‘TP Lindanda’.
Pamba ilianza harakati hizo tangu Januari 2025 za kumpata mshambuliaji huyo, ingawa hazikuweza kuzaa matunda, baada ya kuelezwa alisaini mkataba pia na Yanga, jambo lililosababisha dili lake kufa na kubaki Mlandege ili kumalizia msimu huu.
Katika msimu huu wa 2024-025, Pina ameonyesha kiwango kizuri akiwa amemaliza Ligi Kuu ya Zanzibar akiwa mfungaji bora, baada ya kutupia mabao 21 na kuivunja rekodi ya aliyekuwa mshambuliaji wa KVZ, Seleman Mwalimu ‘Gomez’ aliyefunga 20.
Gomez anayeichezea Wydad Casablanca ya Morocco kwa sasa, alifunga mabao 20 msimu uliotangulia akiwa na KVZ na kuzivutia timu mbalimbali, kabla ya kunaswa na Singida Black Stars, kisha kucheza Fountain Gate kwa mkopo.
Mbali na kuibuka mfungaji bora, Pina ameiwezesha Mlandege kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Zanzibar, baada ya kumaliza na pointi 62 sambamba na KVZ, lakini zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa yaliyochangia kuhitimisha msimu kibabe.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Pamba, Peter Juma Lehhet, alisema wanapambana kuangalia maeneo muhimu ya kuboresha kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao, kutokana na ripoti iliyowasilishwa mezani kwao na benchi la ufundi.
“Hiki ni kipindi ambacho ni kigumu sana kwa sababu mbali na ushawishi wa mchezaji unayemuhitaji ni lazima uwe pia na fedha, hatuwezi kusema wazi tunamuhitaji nani hadi pale tutakapokamilisha, lengo ni kutoharibu mipango yetu,” alisema.
Mabosi wa Pamba wanapambana kupata saini ya nyota huyo mapema iwezekanavyo kutokana na timu nyingi kumuhitaji, kwa lengo la kwenda kutengeneza pacha kali na mshambuliaji, Mkenya Mathew Tegisi Momanyi aliyefunga mabao saba ya Ligi Kuu Bara.