Prime
Kocha Hamdi avunja ukimya, aanika ukweli kuondoka Yanga

Muktasari:
- Kocha huyo raia wa Algeria, juzi usiku alitamabulishwa na klabu ya Ismalia ya Misri, ikiwa ni siku chache tangu atwae ubingwa wa Kombe la Shirikisho (FA) kwa kuifunga Singida Black Stars kwa mabao 2-0 baada ya awali kuifunga Simba kwa idadi kama hiyo katika Dabi ya Kariakoo iliyopigwa Juni 26.
SIKU chache tu tangu aiwezeshe Yanga kubeba mataji mawili kwa mpigo kati ya matatu aliyotwaa tangu alipojiunga nayo Februari 4 mwaka huu, kocha Miloud Hamdi amewafanya sapraizi mashabiki wa klabu hiyo, huku akifunguka kila kitu kuhusu maisha akiwa Jangwani na safari nzima anayoenda kuanza akiwa Misri.
Kocha huyo raia wa Algeria, juzi usiku alitamabulishwa na klabu ya Ismalia ya Misri, ikiwa ni siku chache tangu atwae ubingwa wa Kombe la Shirikisho (FA) kwa kuifunga Singida Black Stars kwa mabao 2-0 baada ya awali kuifunga Simba kwa idadi kama hiyo katika Dabi ya Kariakoo iliyopigwa Juni 26.
Hamdi aliyeitumikia Yanga kwa muda wa siku 148, ikiwa sawa na miezi minne na siku 28 au wiki 21 na siku moja tangu alipoajiriwa na kutambulishwa Februari 4 hadi juzi Jumatano alipoibukia Ismailia, ameipa timu hiyo ubingwa wa Kombe la Muungano, Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho.
Kocha huyo raia wa Algeria mwenye umri wa miaka 54, ametambulishwa juzi usiku kuwa kocha mkuu wa Ismailia inayoshiriki Ligi Kuu ya Misri, ikiwa ni siku chache tu tangu alipoiwezesha Yanga kutetea ubingwa wa Kombe la Shirikisho kwa kuifunga Singida BS kwa mabao 2-0 na wiki moja tangu ainyoe Simba pia kwa mabao 2-0 katika kiporo cha Dabi ya Kariakoo kilichochezwa Juni 25.
Ameondoka Yanga akiwa ameiongoza katika mechi 13 za Ligi Kuu Bara akishinda 12 na kutoka sare moja, huku akivuna jumla ya mabao 41 na kufungwa matatu tu, mbali na mechi za Kombe la Shirikisho na zile za Kombe la Dunia ambazo kote alifanya mambo mwanzo mwisho akiandika rekodi tamu katika kipindi cha muda mfupi tangu ajiunge na timu hiyo akitokea Singida Black Stars.
Akizungumza na Mwanaspoti, Hamdi alisema hakutarajia kuitema Yanga, isipokuwa kitendo cha mabosi wa klabu hiyo kumkaushia kuanza naye mazungumzo wakati mkataba ukiwa umemalizika, ilimfanya asisite mara mbili mara ofa ya Wamisri ilipotua mezani kwake.
Kocha huyo aliyepewa mkataba wa mwaka mmoja na Ismailia, alisema kipaumbele chake kilikuwa ni kuendelea kubaki ndani ya Yanga lakini hakukuwa na ofa yoyote kwa mabosi hao wa Jangwani.
Alifichua mbali na ofa ya Ismaily, lakini alikuwa na nyingine ya US Monastri ya Tunisia na ES Setif ya Algeria na klabu nyingine za Afrika Kusini, lakini alikuwa akitamani kuendelea kubaki Yanga, ila kwa vile hakukuwa na mazungumzo yoyote na uongozi hadi alipoamua kuondoka nchini.
“Nimefurahi kuwa sehemu ya kikosi cha mafanikio mataji matatu ndani ya muda mchache nikiwa na timu yenye CV kubwa kama Yanga ni furaha kubwa kwangu naamini timu hiyo ina uongozi bora na kikosi imara itatwaa sana mataji ya ligi hiyo,” alisema Hamdi na kuongeza;
“Ulikuwa msimu bora kwangu ndani ya Yanga nimejifunza mambo mengi sana na nilikuwa na ushirikiano mzuri kuanzia viongozi wachezaji hadi mashabiki nawatakia mafanikio mema kwa msimu ujao naamini bado wataendeleza ushindani wana uongozi imara na timu bora.”
Hamdi alisema mafanikio aliyoyapata ndani ya Yanga yametokana na ubora wa timu na uongozi sahihi ambao umewekeza nguvu ndani na nje ya uwanja kuhakikisha timu hiyo inafikia mafanikio, huku akiishukuru Yanga kwa kumpa nafasi na kumuamini alichokifanya ni sehemu ya uaminifu aliopewa.
Ukiacha kuiongoza Yanga katika mechi 13 na kushinda 12 ikitoka sare moja, pia aliiongoza timu hiyo katika mechi tano za Kombe la Shirikisho kuanzia hatua ya 32 Bora hadi fainali akishinda zote akivuna mabao 17 na kufungwa moja tu.
Katika Kombe la Muungano, kocha huyo aliiongoza Yanga kucheza mechi tatu akishinda zote, akianza kwa kuifunga KVZ kwa mabao 2-0, kisha kuing’oa Zimamoto kwa penalti 3-1 baada ya sare ya 1-1 ya dakika 90 na katika fainali ikaichapa JKU kwa bao 1-0 na kutwaa ubingwa.
Hii ikiwa na maana katika siku 148 alizoiongoza Yanga kama kocha mkuu, Hamdi amecheza jumla ya mechi 21 za mashindano yote, ikishinda 19 na kutoka sare mbili ikiwamo ile na nusu fainali ya Kombe la Muungano kabla ya kuvuka kwa penalti kwenda fainali na ile ya JKT Tanzania.
Hamdi anakuwa kocha wa pili mfululizo kuondoka Yanga ndani ya muda mfupi baada ya Sead Ramovich aliyechukuliwa na CR Belouizdad ya Algeria aliyempokea Miguel Gamondi aliyetimuliwa Jangwani licha ya kuandika rekodi ya kuifikisha timu makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa misimu miwili mfululizo.