Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Safari ya jasho, machozi na damu ya KMC katika Ligi Kuu Tanzania Bara

Muktasari:

Zipo sababu kadhaa ambazo zinaonekana kuiangusha KMC katika sehemu kubwa ya mechi za mwanzoni mwa msimu ambazo baada ya kufanyiwa kazi, timu hiyo imerudi katika mstari kwa sasa

Dar es Salaam.KMC haikuwa na mwanzo mzuri katika msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara na mwenendo wake ulikuwa wa kusuasua katika mashindano mbalimbali iliyoshiriki.

Nuksi kwa KMC ilionekana kuanzia katika hatua ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo ilijikuta ikitolewa na AS Kigali kwa kipigo cha jumla cha mabao 2-1.

Licha ya kutoka sare ya bila kufungana ugenini huko Kigali, Rwanda, KMC ilijikuta ikipoteza mchezo wa marudiano uliochezwa katika Uwanja wa Taifa hapa jijini kwa mabao 2-1 na kutupwa nje ya mashindano hayo.

Ikionekana pengine ugeni wa ushiriki katika mashindano ya kimataifa ndio umewagharimu hadi kupelekea waondolewe mapema katika mashindano ya kimataifa, timu hiyo iliendelea kusuasua katika mechi za mwanzoni za Ligi Kuu.

Haikushangaza kuona nyakati fulani ikiwepo katika nafasi ya pili kutoka mkiani jambo ambalo wengi hawakutegemea kuona likitokea kwa timu hiyo hasa kutokana na uwekezaji ambao imefanya pamoja na ubora wa wachezaji wanaounda kikosi chake.

Lakini hata hivyo imeonekana kuimarika katika siku za hivi karibuni ambapo imecheza michezo minne mfululizo bila kupoteza ikishinda miwili na kutoka sare miwili, imefunga mabao tisa na imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili tu.

Zipo sababu kadhaa ambazo zinaonekana kuiangusha KMC katika sehemu kubwa ya mechi za mwanzoni mwa msimu ambazo baada ya kufanyiwa kazi, timu hiyo imerudi katika mstari kwa sasa.

Mabadiliko ya benchi la ufundi

Mara baada ya msimu uliopita, aliyekuwa kocha wa KMC, Etienne Ndairagije aliachana na timu hiyo na kujiunga na Azam FC jambo ambalo liliulazimu uongozi wa timu hiyo inayomilikiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kusaka kocha mpya ambapo ilimleta Jackson Mayanja kutoka Uganda.

Kwa bahati mbaya kundi kubwa la wachezaji wa KMC lilionekana kutomudu mbinu za kocha Mayanja ambaye sio muumini wa soka la kumiliki mpira na pasi nyingi kama ilivyo kwa Ndairagije jambo ambalo liliwafanya wapate wakati mgumu mwanzoni.

Na hata walipoachana na Mayanja, benchi la ufundi lilibakia mikononi mwa aliyekuwa kocha msaidizi, Ahmad Ally ambaye hata hivyo viatu hivyo vilionekana kuwa ni vikubwa kwake kuvivaa.

Lakini tangu alipokuja kocha Haruna Harerimana raia wa Burundi ambaye ametokea Lipuli FC ya Iringa, KMC inaonekana kurudi katika utamaduni na staili yake ambayo imezoea na angalau imeonekana kupata nafuu.

Kocha Harerimana aliliambia gazeti hili kuwa kulikuwa na kasoro kadhaa ambazo amezifanyia marekebisho hadi timu hiyo imeanza tena kuwa tishio.

“Kikosi ni kizuri na kuna udhaifu kidogo ambao ulikuwepo lakini tunaendelea kuufanyia kazi na naamini tutakuwa imara zaidi kadri siku zinavyozidi kwenda mbele kwani sio jambo la kulikamilisha ndani ya siku moja,” alisema kocha huyo.

Majeruhi

KMC ilianza msimu ikikabiliwa na changamoto ya majeraha kwa wachezaji wake hivyo kujikuta ikicheza idadi kubwa ya mechi bila ya uwepo wa wachezaji wengi muhimu hasa wale wa nafasi ya ushambuliaji.

Charles Ilanfya, Hassan Kabunda, Salim Aiyee, Yusuph Ndikumana, James Msuva, Cliff Buyoya na Ramadhani Kapera wote walikumbana na majeraha ambayo yaliwafanya wakose idadi kubwa ya mechi za mwanzoni.

Hilo liliwahi kulalamikiwa na kocha Mayanja kabla hajaachana na timu hiyo akidai kwa kiasi kikubwa majeruhi ya wachezaji wake yalimgharimu.

“Niliikuta timu ina kundi kubwa la wachezaji walio majeruhi na wengine hawakuwa fiti jambo lililonilazimu kuanza programu huku nikiwakosa idadi kubwa lakini pia ratiba ya mashindano ikawa inatubana hivyo tukajikuta tuna namba ndogo ya wachezaji na dirisha la usajili lilikua limeshafungwa,”  alisema Mayanja.

Kuporomoka viwango vya wachezaji

Baadhi ya wachezaji walipoteza fomu ambayo walikuwa nayo msimu uliopita wakiwemo wale waliokuwemo kikosini na hata wale waliosajiliwa katika kipindi cha usajili wa dirisha kubwa.

Mfano wa wachezaji hao ni Vitalis Mayanga, George Sangija, Melly Sivilwa, Rehani Kibingu, Besala Bokungu na Aaron Lulambo.

Migogoro ya ndani

Inadaiwa kuwa ndani ya uongozi wa KMC kulikuwa na migogoro baina ya viongozi ambayo ilipelekea baadhi yao kuhujumu timu katika baadhi ya mechi.

Mgongano wa kimaslahi ambao unatajwa kuwepo kwa baadhi ya viongozi wa KMC, unaelezwa kuwa umechangia kiasi fulani kwa timu hiyo kufanya vibaya ingawa hilo limekanushwa na timu hiyo.

“Hakuna ukweli wa taarifa hizo na ni uzushi tu.

Kilichotokea ni kwamba timu ilikuwa na changamoto za kiufundi na sio kwamba ilikuwa inafanya vibaya kwa sababu ya migogoro. Lakini kwa sasa mnaona imeanza kuimarika na tunaamini itafanya vizuri zaidi,” alisema Mtendaji Mkuu wa Klabu hiyo, Walter Harrison.