Prime
Kishindo cha mwisho Dabi ya Kariakoo

Muktasari:
- Katika siku hizo 12, kuna mtego upo katikati ya vigogo wa soka nchini, Yanga na Simba ambao utaamua hatma yao msimu huu kwenye kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
KUTOKA Ijumaa ya Juni 13, 2025 siku ambayo Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) ilitangaza kuusogeza mbele mchezo wa Dabi ya Kariakoo na kusema utachezwa Jumatano Juni 25, 2025, kuna takribani siku 12.
Katika siku hizo 12, kuna mtego upo katikati ya vigogo wa soka nchini, Yanga na Simba ambao utaamua hatma yao msimu huu kwenye kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
Ifahamike kwamba, Juni 25 siku ambayo itachezwa Dabi ya Kariakoo kufunga msimu wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2024-2025, kutakuwa na kishindo kizito pale ambapo Yanga itaikaribisha Simba kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Kishindo hicho kitatokea kutokana na mbio za ubingwa zilivyo kwa timu hizo zilizotofautiana kwa pointi moja tu kwa sasa, Yanga ikiwa na pointi 73 kileleni, ikifuatiwa na Simba yenye 72 huku zote zikishuka dimbani mara 27.
Siku hiyo itatukumbusha ilivyokuwa mara ya mwisho mwaka 2012 ambapo Dabi ya Kariakoo ilichezwa siku ya mwisho ya kufunga msimu. Kwa wakati huo, Simba ilikuwa na uhakika wa kubeba ubingwa, hivyo ikautumia mchezo huo kusherehesha tafrija yao ikiichapa Yanga mabao 5-0. Ilikuwa Mei 6, 2012.
Safari hii, ni tofauti, hadi sasa bingwa hajajulikana, hivyo mchezo huo unaweza kutumika kuamua mshindi, jambo ambalo litaleta kishindo kizito kuanzia nje hadi ndani ya uwanja.
Ipo hivi; Ikienda hadi mwisho tofauti ya pointi ikibaki kuwa moja, tunaweza kushuhudia rekodi ikiwekwa kwa mashabiki kuujaza uwanja siku ya mchezo kwani kwa miaka ya hivi karibuni Dabi ya Kariakoo imekuwa haina mvuto mkubwa kiasi cha kuujaza uwanja, lakini safari hii, maajabu yatakuwapo.
Ukiachana na hilo, kupelekwa mbele kwa mchezo huo, kuna mtego mkubwa si kwa Simba na Yanga pekee, bali hata wapinzani wanaokutana nao hapa katikati kuelekea Juni 25.

NJIA YA UBINGWA
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga SC, wanalifukuzia taji la ligi hiyo kwa msimu wa nne mfululizo wakiwa kileleni baada ya mechi 27, wakishinda 24, kupoteza mbili na sare moja. Imefunga mabao 71 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 10.
Nyuma yake kuna Simba yenye pointi 72 zilizotokana na kucheza mechi 27, ushindi 23, sare tatu na kupoteza moja. Simba imefunga mabao 63 na kuruhusu 11.
Yanga inakabiliwa na mechi mbili za kimkakati kabla ya kukutana na Simba ambapo moja ni dhidi ya Tanzania Prisons, timu ambayo ipo kwenye mapambano ya kuepuka kuangukia kucheza mechi za mtoano za kujinasua na janga la kushuka daraja. Kisha itamalizana na Dodoma Jiji.
Katika mchezo dhidi ya Tanzania Prisons ambao ndiyo unaofuatia Juni 18 mwaka huu, Yanga itasafiri hadi Mbeya kukabiliana na Wajelajela hao kwenye Uwanja wa Sokoine jijini humo ambapo mara ya mwisho uwanjani hapo Yanga ilishinda 2-1, ilikuwa Februari 11, 2024. Lakini duru la kwanza msimu huu Yanga ikiwa mwenyeji ilishinda 4-0.
Rekodi zinaonyesha Yanga ni wababe mbele ya wapinzani wao hao hivyo kuifanya timu hiyo kuwa na asilimia kubwa ya kushinda ingawa Tanzania Prisons kipindi hiki cha mwishoni imeamka chini ya kocha Aman Josiah ambapo imeshinda mechi nne mfululizo.
Kiwango hicho kizuri cha Tanzania Prisons, kinaufanya mchezo huu kuwa na sura tofauti, Yanga inahitaji pointi tatu za kuendelea kuwa kileleni, wapinzani wao wanazitaka pointi hizo ili kupanda nafasi kutoka 13 waliyopo sasa ili kutoka kwenye mstari wa kucheza mechi za mtoano.

Wakati Yanga ikikabiliana na Prisons, Simba nayo itakuwa mgeni wa KenGold, timu nyingine kutoka Mbeya huku mchezo huo uliopangwa kufanyika Juni 18, unatarajiwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Majimaji uliopo mkoani Ruvuma.
Duru la kwanza Simba nyumbani ilishinda 2-0, pia KenGold mechi tano za mwisho imepoteza zote na kuifanya timu hiyo kuwa na nafasi ndogo ya ushindi mbele ya Simba.
Hesabu zilizopo katika mechi hizo mbili, Yanga na Simba kila moja inahitaji ushindi ili kuendelea kuufukuzia ubingwa, lakini pia Prisons nayo inautolea macho ikipambana kutoka kule chini ingawa imepoteza mechi zote tano mfululizo dhidi ya Yanga. KenGold imeshuka daraja, haina cha kupoteza lakini inaweza kuwa sehemu ya nyota wa kikosi hicho kuonyesha ubora wao kujitengenezea soko kuelekea msimu ujao. Lolote linaweza kutokea.
Baada ya hapo, Juni 22 Yanga na Simba zote zitakuwa nyumbani katika mechi za mzunguko wa 30. Yanga itaikaribisha Dodoma Jiji ambapo duru la kwanza ikiwa ugenini ilishinda kwa mabao 4-0.
Rekodi zinaonyesha Yanga imeichakaza Dodoma Jiji mara nane kati ya mechi tisa walizokutana kwenye ligi, huku moja ikiwa sare. Rekodi hiyo nzuri kwa Yanga inaibeba kuelekea mchezo huo muhimu wa kulisaka taji.

Simba nayo itaikaribisha Kagera Sugar, duru la kwanza ugenini Simba ilishinda 5-2, huku mechi zao tano za mwisho baina yao, Simba imeshinda tatu na sare mbili. Mara ya mwisho Kagera iliifunga Simba Januari 26, 2022 bao 1-0 ikiwa nyumbani Kaitaba, lakini ugenini dhidi ya Simba, ilipata ushindi mara ya mwisho Mei 19, 2019 kwa bao 1-0.
AHOUA, MZIZE, DUBE VITA NYINGINE
Ukiweka kando mbio za ubingwa, kuna vita nyingine inayowahusu Simba na Yanga katika kuwania tuzo ya ufungaji bora.
Kwa sasa Jean Charles Ahoua wa Simba anaongoza chati ya ufungaji akiwa na mabao 15, akifuatiwa na wachezaji wa Yanga, Prince Dube na Clement Mzize ambao kila mmoja anayo 13. Tofauti ikiwa ni mabao mawili pekee.
Nyota hao watatu wana kazi kubwa ya kufanya katika mechi tatu zilizosalia ili kuweka ufalme mpya baada ya msimu uliopita tuzo hiyo kubebwa na Stephane Aziz KI aliyekuwa Yanga kabla ya hivi karibuni kutimkia Wydad ya Morocco.

CAMARA NA DIARRA NAO
Hapa kuna vita nyingine inayowahusu Simba na Yanga kupitia makipa wao, Moussa Camara na Djigui Diarra.
Makipa hao wanapigana vikumbo kuhakikisha wanamaliza ligi na clean sheet nyingi na kujitengenezea nafasi ya kushinda tuzo ya kipa bora ambapo mechi tatu zilizobaki zitaamua jambo.
Kwa sasa Camara anaongoza akiwa na clean sheet 17, wakati Diarra akikusanya 15. Katika mechi tatu zilizobaki, Camara anahitaji mbili tu kumaliza bila ya kuruhusu bao ili kuweka ufalme mpya wakati Diarra ana jukumu la kuhakikisha zote tatu anatoka na clean sheet kisha kumuombea mabaya mwenzake.
Diarra msimu uliopita alimaliza ligi na clean sheet 14 nyuma ya kinara Ley Matampi aliyekuwa Coastal Union. Kabla ya hapo, Diarra alikuwa kipa bora wa Ligi Kuu Bara kwa msimu miwili mfululizo.

SIKU 10 NGUMU YANGA
Inafahamika Simba kwa sasa inawania taji moja pekee la ligi inalolipigania katika siku saba kuanzia Juni 18 hadi Juni 25, lakini watani zao wa jadi wanayo mawili wakipambana kuyatetea.
Yanga imeingia fainali ya Kombe la FA ikienda kucheza dhidi ya Singida Black Stars, Juni 28 mwaka huu kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Mchezo huo wa fainali utachezwa siku tatu baada ya kufanyika mechi ya Dabi ya Kariakoo ambayo inaweza kuwa ndiyo ya kuamua bingwa wa ligi kama mambo yakienda kama yalivyo sasa.
Kabla ya Yanga kuwa na siku hizo ngumu za uamuzi kwa kucheza mechi nne, Simba imepitia kipindi hicho ilipokuwa ikishiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu ambapo ilikabiliwa na siku 14 ikishuhudiwa ikiyatema makombe mawili baada ya kucheza mechi nne.
Hiyo ilianzia Mei 17, 2025 ilipocheza fainali ya kwanza ugenini katika Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane na kufungwa 2-0, kisha marudiano Mei 25 ikatoka sare ya 1-1 na kufanya matokeo ya jumla kupoteza kwa 3-1.
Baada ya hapo, Mei 28 ikakabiliana na Singida Black Stars katika mechi ya ligi, ikashinda 1-0, kisha Mei 31 ikafungwa 3-1 na Singida Black Stars kwenye nusu fainali ya Kombe la FA na kupoteza kombe la pili.
Yanga kwa sasa ina siku 10 kuanzia Juni 18 hadi Juni 28 za kupambania makombe mawili ambayo inayashikilia baada ya kuyatwaa msimu uliopita.
Safari ya kwanza inaanzia kwenye ligi kwa kucheza mechi tatu dhidi ya Tanzania Prisons (Juni 18), Dodoma Jiji (Juni 22), Simba (Juni 25) na Singida Black Stars (Juni 28).

WASIKIE MAKOCHA
Kocha Mkuu wa Yanga, Miloud Hamdi amesema: “Tuna jukumu la kutetea ubingwa wa ligi, hiki ni kitu ambacho hakiepukiki, tunajituma ili kuhakikisha ubingwa huu tunaendelea kuushikilia, nafahamu ligi ni ngumu lakini kama Yanga hatutakiwi kuogopa kwa kuwa nia na ubora wa kufanya hayo tunao, tutafanya kila linalowezekana kuchukua ubingwa huu na ule wa Kombe la FA.
“Nawashukuru sana viongozi wangu wako karibu sana na timu lakini muhimu kuliko wote ni mashabiki wetu, kila unapopita sehemu au tunapoingia uwanjani ukiona ule umati uliovaa jezi za njano na kijani akili yako inausukuma moyo kwamba una deni kwa hawa watu waliokuja kuwapa nguvu.”
Kocha wa Simba SC, Fadlu Davids, ambaye alichukua mikoba mwanzoni mwa msimu huu, ameweza kuibadili timu hiyo na kuipa mwonekano mpya.
Amesema: “Tuna mechi ambazo kwetu ni kama fainali. Hatuwezi kujiamini sana wala kuangalia wapinzani wetu wanavyofanya. Tunapaswa kuhakikisha tunashinda kila mchezo. Hakuna nafasi ya kupumzika. Huu ndio wakati wa kuonyesha tabia ya mabingwa.”
Fadlu amesisitiza kuwa hata mechi dhidi ya timu zilizo nafasi za chini KenGold na Kagera Sugar ambazo tayari zimeshuka daraja haziwezi kupuuzwa kwani kila mechi ni mtihani.