Simba SC yaitumia salamu Yanga kwa kuichapa KMC

Muktasari:
Ushindi huo unamfanya kocha mpya wa Simba, Sven kuendeleza rekodi ya ushindi katika michezo mitatu aliyoiongoza timu tangu alipochukua mikoba Partick Aussems
Dar es Salaam. Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba wameitumia salamu Yanga baada ya kuichapa KMC mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Mabao ya Deo Kanda katika dakika ya 46 na Mbrazil Gerson Fraga katika dakika 90 yametosha kuipa Simba pointi tatu na kuendelea kujikita kileleni mwa ligi kwa pointi 31 na kujiweka vizuri kuelekea katika mchezo wa watani wa jadi dhidi ya Yanga utakaofanyika Jumamosi ijayo.
Ushindi huo unamfanya kocha mpya wa Simba, Sven kuendeleza rekodi ya ushindi katika michezo mitatu aliyoiongoza timu tangu alipochukua mikoba Partick Aussems.
Katika mchezo huo KMC iliyocheza kwa kujilinda vizuri katika kipindi cha kwanza ilipoteza uelekea mwanzoni mwa kipindi cha pili kwa kuruhusu bao la mapema la Deo Kanda aliyemalizia kwa shuti la chini krosi ya Hassan Dilunga.
Baada ya bao hilo Simba walichangamka na kuongeza mashambulizi, lakini KMC ilionekana kurudi mchezoni na kuongeza umakini katika kujilinda chini ya kipa wake Jonathan Nahimana.
Kiungo Mbrazili Gerson Fraga alifunga bao lake kwanza la Ligi Kuu akiwa na Simba kwa kuunganisha krosi Francis Kahata kwa shuti kali la chini akiwa nje ya eneo 18 katika dakika ya 90+3 likiwa ni bao la pili la Simba.
Kiungo wa Simba, Hassan Dilunga alipata wakati mgumu dakika 45 za kipindi cha kwanza kutokana na mara kwa mara kupigiwa kelele na mashabiki.
Dilunga ambaye ameanza mchezo wa leo amekuwa na uamuzi wa taratibu pindi anapokuwa na mpira au kufanya uamuzi mengine ambayo yamekuwa yakiwashangaza hata wenzake uwanjani.
Dakika ya 15 alipokea pasi kutoka kwa Muzamiru Yassin, lakini akajikuta akichelewa kumpasia Ibrahim Ajib aliyekuwa katika eneo zuri la kufunga na kujikuta akupokinywa mpira huo na mabeki wa KMC hivyo kuamsha kelele kwa mashabiki wa Simba wakimzomea.
Pia dakika ya 33 akiwa katika nafasi ngumu ya kufunga alijikuta akipiga shuti na mpira kutoka nje Jambo lililowafanya mashabiki wa Simba kuanza kumpigia kelele na wengine kumzomea wakisema'Toa huyo…toa huyo.'.
Hata hivyo kocha was Simba hakusikiliza kelele hizo na aliendelea kumuacha uwanjani mchezo huo akiamini kuwa anaweza kufanya Kama alichofanya Katika mchezo uliopita dhidi ya Lipuli ya Iringa ambao Simba ilishinda mabao 4-0.
Katika mchezo huo Dilunga alianza ovyo lakini kadri muda ulivyokuwa ukienda alitulia na kufunga mabao mawili huku akiisaidia timu yake kupata ushindi