KMC yaikomalia Yanga ya Mkwasa Uwanja wa Taifa

Monday December 2 2019

Mwanaspoti-KMC-yaikomaliza-Yanga-Tanzania-Mkwasa-atulizwa-Ligi-Kuu-Bara-TFF-SimbaSC

 

Dar es Salaam. KMC imepunguza kasi ya kocha Charles Mkwasa baada kulazimisha sare ya bao 1-1 dhidi ya Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliofanyika jana kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Wakati Mkwasa akionekana anakwenda kupata ushindi wa nne mfululizo tangu apewe mikoba ya kuinoa timu hiyo, lakini hali ilijikuta ikibadilika dakika 93 baada ya KMC kupata penalti kutokana na beki Kelvin Yondani kumuangusha Hassana Kabunda kwenye eneo la hatari.

Yanga ndio ilitangulia kupata bao dakika ya 74 lililofungwa na Mrisho Ngassa kwa shuti akimalizia pasi safi ya kupenyeza kutoka kwa Patrick Sibomana.

KMC ambayo ilicheza vizuri zaidi kipindi cha pili na kuipa presha kubwa Yanga ilisawazisha bao hilo kwa njia ya Penalti iliyofungwa na Abdul Hillary na kuamsha shangwe katika benchi la timu hiyo.

Sare hiyo ni kama ushindi kwa KMC ambayo imefanya vibaya katika michezo mitatu mfululizo iliyopita kwa kupoteza yote licha ya kwamba hivi karibuni ilimtimua kocha wake Mganda Jackoson Mayanja.

Sare hiyo inaifanya Yanga kupanda hadi nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi baada ya kufikisha pointi 17 huku KMC ikiendelea kusalia bnafasi ya 17.

Advertisement

Mkwasa apunguzwa kasi

Sare hiyo ni kama imempunguza kasi Mkwasa ambaye  tangu apewe timu alinza kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ndanda, kisha akaichapa JKT Tanzania mabao 3-2 halafu kaifunga Alliance Fc mabao 2-1.

Kuonyesha kuwa alichukizwa na sare hiyo Mkwasa alipohojiwa alimlalamikia mwamuzi Heri Sasii kwa madai ya kuwazawadia penalti KMC ambayo haikuwa halali.

"Tunakubali matokeo na nafikiri pia uchovu wa wachezaji wangu ulichangia.Hata hivyo mwamuzi  hakutenda haki kwa kutoa penalti ambayo haikuwa halali"alisema Mkwasa.

 

Kwenye Uwanja wa Karume Mara, wenyeji Biashara United waliibuka na ushindi kwa kuichapa Ndanda bao 1-0 lililofungwa na Bright Obina dakika ya 22.

Advertisement