Ninja: Molinga kakosa watu sahihi

Muktasari:

Ninja pia alisema kwa namna alivyowaangalia wachezaji wa kigeni waliosajiliwa msimu huu, anaamini Yanga imelamba karata dume zaidi kwa Lamine Moro akidai ni bonge la beki ambaye ameona mchango wake mkubwa katika kuzuia mashambulizi akishirikiana na Kelvin Yondani na Ally Mtoni ‘Sonso’.

ABDALLAH Shaibu ‘Ninja’, beki wa zamani wa Yanga anayekipiga LA Galaxy, amekiangalia kikosi cha sasa cha Jangwani na kumchambua straika David Molinga, akidai amezungukwa na wachezaji wasio sahihi ndio maana anashindwa kufanya mambo ndani ya kikosi hicho.

Ninja aliyerejea nchini kwa mapumziko, alisema kwa jinsi alivyomwangalia Molinga amebaini ni mtu wa nipe nikupe na kutaka kulishwa zaidi ili awe na kazi moja tu ya kufunga mabao, lakini namna anaocheza nao ni kama wanamkosea vile.

Aliitolea ufafanuzi kauli yake, amekuwa akiifuatilia Yanga ikicheza na kumwona Molinga staili ya uchezaji wake ni ya kuhitaji msaada mkubwa mpaka afike langoni ama kutikisa nyavu kwa aina hiyo ni lazima awe na mtu wa kumlisha mipira ili kazi yake iwe ni kutupia nyavuni.

“Nadhani Molinga amekosekana watu wenye kasi ya kumlisha pasi za mwisho, kwani anaonekana sio mtu wa mambo mengi, lakini pia inawezekana hawezi kucheza kwa kiwango bila ya mtu wa kumpa mpira na yeye kurudisha yaani nipe nikupe,” alisema na kuongeza;

“Kwa staili yake ni ngumu kuliona lango akikutana na mabeki wanaojua kazi ya kukaba haswa, kwa upande wangu ndivyo nilivyomwona ni mchezaji mzuri na akipata mtu sahihi wa kucheza naye Yanga wanaweza kusahau kila kitu.”

Ninja pia alisema kwa namna alivyowaangalia wachezaji wa kigeni waliosajiliwa msimu huu, anaamini Yanga imelamba karata dume zaidi kwa Lamine Moro akidai ni bonge la beki ambaye ameona mchango wake mkubwa katika kuzuia mashambulizi akishirikiana na Kelvin Yondani na Ally Mtoni ‘Sonso’.

“Namkubali sana beki wa kati Moro (Lamine), yule jamaa anajua, ameendana na soka la Tanzania ndio maana akipangwa na Yondani anafanya vizuri akipangwa na Sonso anafanya maajabu vile vile,” alisema Ninja aliyeichezea Yanga kwa misimu miwili kabla ya kutimka Marekani anakocheza kwa mkopo.

Kuhusu mapungufu aliyoyaona kikosini, alisema eneo la straika na winga bado hakujakaa sawa na kutoa ushauri kwa Kamati ya Usajili kuboresha eneo hilo kwenye usajili wa dirisha dogo.

“Yanga ni klabu kubwa inayohitaji matokeo muda wote, ndio maana anahitajika straika anayeweza kulazimisha matokeo mazuri, pia asajiliwe winga matata ambaye atakuwa msaada ndani ya timu hiyo, kama ilivyokuwa kwa Simon Msuva kipindi cha nyuma. Hata hivyo ieleweke sina maana waliopo ni wabaya, ila wanahitajika watu wenye uwezo zaidi na ingekuwa nzuri wangesajili winga na mshambuliaji wa ndani, hao wa kigeni ni ngumu kuzoea ligi yetu kwa haraka.”

MKWASA ASHTUKA

Katika hatua nyingine Kocha Charles Mkwasa ameishtukia Iringa United na kuwaita wachezaji wake fasta kwa mazoezi yaliyoanza jana kabla ya wikiendi hii kusafiri hadi Kigoma kucheza mechi kadhaa za kirafiki kujiweka fiti kwa mchezo wao wa Kombe la FA utakaopigwa jijini Dar es Salaam.

Mkwasa alisema hawataki kilichowapata watani zao, Simba mbele ya Green Warriors na Mashujaa klatika michuano hiyo kiwakute nao, akidai licha ya ugeni wao, lakini hawaidharau Iringa ndio maana wanaanza maandalizi mapema ili kuhakikisha wanapata matokeo mazuri na kurahisisha kazi ya kukata tiketi yaCAF kwa mechi za kimataifa kupitia michuano hiyo.

“Tunajua michuano hii ni njia ya kutaka tiketi ya mechi za kimataifa, hivtyo hatutaki kufanya uzembe wowote, tumeanza mazoezi na tutaenda Kigoma kwa mechi kadhaa za kirafiki kabla ya kuja kuvaana na Iringa,” alisema Mkwasa aliyeichukua timu baada ya kuondolewa kwa Kocha Mwinyi Zahera kutoka DR Congo.