Mo atuliza presha Simba

Muktasari:

  • Simba inacheza na Ihefu kesho Jumamosi kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara likiwa ndiyo kombe pekee ambalo timu hiyo imebakiza msimu huu, baada ya kutupwa nje kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ilipochapwa jumla ya mabao 3-0 na Al Ahly, lakini siku nne mbele ikatolewa kwenye Kombe la FA kwa mikwaju ya penalti 6-5 na Mashujaa.

Wakati timu ya Simba ikiwa imebakiza kuwania kombe moja tu msimu huu, Rais wa Heshima wa klabu hiyo, Mohamed Dewji ‘Mo’ amewasiliana na benchi la ufundi na wachezaji wote wa timu hiyo, akitaka utulivu kwanza.

Simba inacheza na Ihefu kesho Jumamosi kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara likiwa ndiyo kombe pekee ambalo timu hiyo imebakiza msimu huu, baada ya kutupwa nje kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ilipochapwa jumla ya mabao 3-0 na Al Ahly, lakini siku nne mbele ikatolewa kwenye Kombe la FA kwa mikwaju ya penalti 6-5 na Mashujaa.

Msimu huu hadi sasa Simba imetwaa Ngao ya Jamii pekee, ikiwa imeachwa pointi saba na watani wao wa jadi, Yanga, lakini ikiwa na mchezo mmoja mkononi baada ya kucheza michezo 19.

Chanzo cha uhakika kutoka ndani ya Simba, kimeliambia Mwanaspoti kuwa, baada ya timu hiyo kupoteza dhidi ya Mashujaa, Mo alimpigia kila mmoja simu akitaka kufahamu tatizo ni nini, lakini akitaka utulivu.

Hivi karibuni lawama nyingi zimekuwa zinaelekezwa kwa mwekezaji huyo kuwa amekuwa hatoi fedha za kuiendesha timu hiyo, lakini kwenye mazungumzo yake amekanusha ishu hiyo.

“Alianza kuwapigia makocha walipofika Singida, ambapo alizungumza nao kwa dakika 45, huku akiwaeleza mipango yake ndani ya Simba, lakini akisema amekuwa akitoa fedha za usajili tofauti na inavyoelezwa na mashabiki.

“Aliwataka kurejea kwenye taarifa ya mkutano mkuu ambayo ilionesha kiasi ambacho mwaka jana alitoa kwa ajili ya usajili na kusema kuwa msimu huu ameendelea kufanya hivyohivyo kama ambavyo imekuwa desturi yake,” kilisema chanzo hicho.

Hata hivyo, inaelezwa kulikuwa na baadhi ya mazungumzo kati yake na benchi ambapo wengine walimueleza kuwa kuna baadhi ya wachezaji waliosajiliwa ambao hawana kiwango sahihi, ambapo alisema hafanyi usajili na anafahamu kuna sehemu za kuboresha.

“Alielezwa kuhusu baadhi ya wachezaji kuwa hawapo vizuri na hawaendani na kasi ya Simba, lakini alionekana kulifahamu jambo hilo ingawa alisema yeye amekuwa hafanyi usajili kwenye timu hiyo, bali anatoa fedha za usajili ikihitajika.

“Alisema anapoelezwa kuhusu ripoti ya kocha na kitu gani kinatakiwa huwa anatajiwa kiasi cha fedha cha mchezaji huyo na kutoa fedha kwa kuwa hawezi kufuatilia kama anaweza kuisaidia Simba au la na siyo jukumu lake.”

Inaelezwa kuwa baada ya kumalizana na mabosi wa benchi la ufundi akiwataka wafanye kila wanachoweza kuhakikisha wanashinda michezo ijayo ya ligi bila kujali matokeo ya wapinzani wao, pia alizungumza na mchezaji mmoja mmoja wa timu hiyo.

“Mo alizungumza pia na wachezaji kama sehemu ya kuwapa morali na kuwaeleza jinsi ambavyo amekuwa akiunga mkono timu hiyo na anataka kuona wanapambana mpaka mwisho,” kilisema chanzo hicho cha uhakika.

Hata hivyo, baada ya hapo alizungumza na baadhi ya watu wa Simba wakiwemo viongozi wa zamani akitaka kila mmoja kuwa na umoja kwa wakati huu ambao timu inaelekea kumalizia msimu, lakini kukiwa na mchezo wa dabi siku chache zijazo.

“Tunasikia pia aliwapigia baadhi ya viongozi wa zamani na wanachama wenye ushawishi mkubwa kuhakikisha wanaiunga mkono timu kwa sasa,” kilisema chanzo hicho.

Aliyewahi kuwa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori, amethibitisha hilo kupitia ukurasa wake wa Instagram jana baada ya kuandika kuwa amezungumza na Mo Dewji na mashabiki wasiwe na wasiwasi timu bora zaidi inakuja.

“Safari ya Simba mpya ilianza mwaka 2018, safari ambayo mpaka sasa haijakamilika! Mategemeo ya kila Mwana-Simba ni kuwa baada ya mabadiliko ya katiba ya mwaka huu (2024) Januari, Serikali itakamilisha mchakato huo hivi karibuni,” ujumbe huo uliendelea kwa kusema;

“Katika kipindi hiki cha miaka 6 ya Simba mpya, timu imepiga hatua kubwa kimaendeleo kama ifuatavyo; 1. Kutoka katika timu isiyojulikana ni ya ngapi Afrika (unranked) mpaka namba 5 Afrika, 2. Kutoka bajeti ya Sh 3 bilioni mpaka bajeti ya zaidi ya Sh 20 bilioni.

“3. Timu imechukua ubingwa wa Tanzania mara nne, 4. Ubingwa wa FA mara tatu, 5. Ngao ya jamii mara nne, 6. Robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara nne, 7. Robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika mara moja, 8. Ushiriki wa African Football League katika timu nane bora Afrika, 9. Viwanja vyake vya mazoezi.”

Magori hakuishia hapo, ameendelea kwa kusema: “10. Timu ya wanawake Simba Queens kuchukua ubingwa mara tatu, 11. Timu ya wanawake Simba Queens kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa kwa Wanawake Afrika.”

Alisema mafanikio hayo katika kipindi cha miaka sita siyo madogo kwa namna yoyote ile huku akidai hakuna timu yoyote Tanzania iliyowahi kufikia mafanikio hayo.

“Hongera Mo Dewji, Bodi ya Simba na Menejimenti ya Klabu, Walimu, Wachezaji na kila Mwana-Simba. Nafahamu hamu ya Wanasimba ni kurudisha ufalme wetu hapa nyumbani na kuvuka hatua ya robo fainali kwenye michuano ya CAF.

“Naomba niwahakikishie baada ya mazungumzo na Rais wa Heshima wa Klabu, Mohamed Dewji naomba niwatoe hofu kuwa Mo hajawahi kuiacha Simba na hataiacha Simba na kuanzia sasa atashirikiana na uongozi kujipanga upya kurudisha heshima ya Simba na kuzidi kuimarika.” Ilimalizia taarifa hiyo.