Huku Molinga,kule Mhilu patamu!

Muktasari:

Katika mechi mbili za Ligi Kuu, Yanga ilishinda jijini Dar es Salaam mabao 3-0 mechi iliyopigwa Oktoba 20, mwaka jana kabla ya kushinda tena jijini Mwanza bao 1-0 katika mechi iliyopigwa Machi 2, mwaka huu kwa bao la Amissi Tambwe na wiki mbili baadaye kuvaana katika robo fainali ya Kombe la FA na kuinyoosha kwa mikwaju ya penalti.

KOCHA Charles Boniface anatarajiwa kufanya mabadiliko machache kwenye kikosi cha Yanga katika pambano lao la kiporo dhidi ya Alliance FC huku, David Molinga akiachiwa msala wa kuendeleza rekodi za kocha huyu, lakini kule Kaitaba, Buboka, Yusuf Mhilu amepania kuipaisha Kagera Sugar kileleni.

Kama hujui ni kwamba leo Ijumaa kuna mechi mbili za viporo vya Ligi Kuu Bara, Yanga wakiwa jijini Mwanza kumalizana na Alliance inayouguza kipigo cha mabao 5-0 kutoka kwa Azam FC, lakini kule Kaitaba wenyeji Kagera Sugar wataikaribisha Ndanda FC inayochechea.

Ushindi wa aina yoyote wa Kagera utamaanisha watakwea kileleni na kuwaengua Simba ambao kwa sasa wanakula shushu katika ligi hiyo wakisubiri pambano lao na watani wao, Yanga, litakalopigwa Januari 4, mwakani. Kagera walikwama kuiengua Simba kwenye mechi iliyopita baada ya kufumuliwa mabao 3-1 na wa Mtibwa Sugar na mastraika wake, Awesu Awesu na Yusuf Mhilu wameapa kufanya kweli kwa nia ya kutaka kumaliza mwaka wakiwa kileleni mwa msimamo.

Mhilu aliyewahi kuichezea Yanga na Ndanda, mpaka sasa amefunga mabao matano, ikiwa ni matatu pungufu na aliyonayo kinara wa orodha ya wafungaji, Meddie Kagere wa Simba mwenye manane, wakati Awesu akitupia kambani mabao manne.

Tuanze na pambano la Yanga. Mabingwa hao wa kihistoria wataivaa Alliance kwenye Uwanja wa CCM Kirumba wakiwa na kumbukumbu ya kuwatambia wapinzani wao katika mechi tatu walizokutana tangu timu hiyo ya jijini Mwanza ipande daraja msimu uliopita.

Katika mechi mbili za Ligi Kuu, Yanga ilishinda jijini Dar es Salaam mabao 3-0 mechi iliyopigwa Oktoba 20, mwaka jana kabla ya kushinda tena jijini Mwanza bao 1-0 katika mechi iliyopigwa Machi 2, mwaka huu kwa bao la Amissi Tambwe na wiki mbili baadaye kuvaana katika robo fainali ya Kombe la FA na kuinyoosha kwa mikwaju ya penalti.

Katika mechi hiyo timu zote zilimaliza dakika 90 zikiwa sare ya 1-1 kabla ya Yanga kuibuka washindi wa penalti 4-3, lakini kipindi hicho ikiwa na Kocha Mwinyi Zahera aliyefurushwa na nafasi yake kuchukuliwa na Mkwasa.

Mkwasa alianza kibarua dhidi ya Ndanda FC na kushinda kwa bao 1-0, kisha kuizima JKT Tanzania kwa mabao 3-2 jijini Dar es Salaam na leo itakuwa ya tatu kwake akiwa na kiu ya kuendelea kukusanya pointi ili kuitoa Yanga maeneo ya chini.

Yanga ipo nafasi ya 15 ikiwa na alama 13 na ikishinda leo itapanda hadi ya 12 na kuishusha Polisi Tanzania, japo Yanga ina michezo pungufu.

Kocha Mkwasa alikiri wanajua wana mchezo mgumu, kwa vile wenzake wametoka kupokea kichapo kinono, lakini ameliandaa jeshi lake kuhakikisha wanatoka Kirumba na alama tatu.

Mkwasa alisema ametua na kikosi cha wachezaji 18 anaoamini watashinda na kuendeleza rekodi ya ushindi kwa Alliance. “Tunajua mchezo hautakuwa rahisi, lakini tumejipanga kuhakikisha tunaendelea kupata matokeo mazuri, hatuwabezi ila tunawaheshimu na tutaingia uwanjani kupambania alama tatu,” alisema.

Mmoja wa wachezaji atakayekosekana ni Mapinduzi Balama aliyesajiliwa Yanga kutokea Alliance msimu huu, hivyo eneo la kiungo litakuwa na sura nyingine, lakini safu ya ushambuliaji itamtegemea David Molinga mwenye mabao matatu akiwa kinara wa mabao wa Yanga, Juma Balinya na Patrick Sibomana.

Nahodha wa Yanga, Papy Tshishimbi alisema: “Sisi tuko vizuri na tumejipanga kushinda mchezo huo ambao ni muhimu kwetu, tutakuwa makini kwa sababu wapinzani siyo wabaya.”

Kwa upande wa Alliance beki na nahodha, Siraji Juma alisema wamejipanga kupata ushindi utakaowafanya wapate nguvu mpya baada ya kufungwa mchezo uliopita.

Katika mchezo wa leo, Alliance inayokamata nafasi ya 11 ikiwa na alama 11 baada ya kucheza mechi 12 itaendelea kuwakosa nyota wake wanne wanaotumikia adhabu zao tofauti kutokana na utovu wa nidhamu akiwamo Kipa John Mwanda na Israel Patrick waliofungiwa mechi tano na Bodi ya Ligi kwa vitendo vya kihuni walivyovifanya walipocheza na na Mbeya City.

Adhabu za wachezaji hao zinamalizika leo, huku Six Mwasekaga na Athanas Mdamu walisimamishwa na uongozi kwa muda wa mwezi mmoja kwa kutoroka kambini na jambo hilo la kuwakosa nyota hao kocha wa timu hiyo, Kessy Mziray alikiri ni changamoto kwao.

Kocha Mziray alisema anashukuru wachezaji waliopo wana uwezo wa kupambana ili kupata matokeo mazuri. “Ni pengo kubwa kwetu, lakini naamini hatutafungwa tena kwani beki wangu Geofrey Luseke aliyekuwa na kadi tatu za njano amerejea, hivyo tutapambana,” alisema.

MHILU NA KAGERA

Mbali na pambano hilo la jijini Mwanza, Mhilu aliyefunga moja ya mabao mawili wakati Kagera ikilala ugenini katika mechi ya mwisho dhidi ya Ndanda wakati huo akiichezea timu hiyo, amesema anajua mechi itakuwa ngumu, lakini kiu ni kuendeleza rekodi ya mabao na wanataka kuwa kileleni mwa msimamo.

Kagera ina pointi 23 na kama ikishinda itafikisha 26, moja zaidi ya walizonazo vinara Simba wanaoongoza msimamo wakiwa na pointi 25 baada ya mechi 10.

Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime alisema: “Tuombe uzima na afya njema, tumejipanga kutorudia makosa, nimewaandaa kisaikolojia wachezaji na tunachohitaji ni kwenda mapumziko tukiwa kileleni.”